29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 18, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Mali za magendo zitakazokamatwa nchini kutaifishwa – TRA

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Forodha huku Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Juma Mwenda, akituma onyo kali kwa wale wanaojihusisha na biashara ya mali za magendo.

Akizungumza leo, Januari 26, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho hayo, Kamishna Mwenda alisisitiza kuwa mali yoyote ya magendo itakayokamatwa ikiingizwa nchini itataifishwa, huku wahusika wakikabiliwa na hatua kali za kisheria.

“Idara ya Forodha ipo imara kupambana na uingizaji wa mali za magendo kwa kuweka udhibiti madhubuti kwenye bandari, viwanja vya ndege, na mipakani. Hatua hizi zinalenga kudhibiti vitendo vya magendo vinavyodhoofisha uchumi wa nchi yetu,” amesema Mwenda.

Kamishna Mkuu Mwenda alieleza kuwa Tanzania imeboresha mfumo wa Forodha wa TANCIS (Tanzania Customs Integrated System), ambao sasa unafanya kazi kwa ufanisi zaidi. Mfumo huo umeunganishwa na taasisi 36, na unatarajiwa kupunguza muda wa uondoshaji mizigo bandarini, mipakani, na kwenye viwanja vya ndege.

“Uboreshaji wa mfumo wa TANCIS ni suluhisho kwa changamoto zote za kiforodha, na utaimarisha biashara kwa haraka, huku ukichangia kuimarisha uchumi wa wananchi mmoja mmoja,” ameongeza.

Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Edward Urio, alisifu mfumo wa TANCIS kwa kuleta uwazi na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.

“Tunaamini mfumo huu utaongeza uwazi na ufanisi, na ni tiba ya matatizo ya kiforodha katika uondoshaji shehena bandarini, mipakani, na kwenye viwanja vya ndege,” amesema Urio.

Kwa upande wake, Kamishna wa Forodha, Bw. Juma Bakari, alisema kuwa mfumo mpya wa TANCIS umeimarika zaidi tangu kuanzishwa kwake mwaka 2014, na sasa utaongeza tija na kurahisisha biashara.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Forodha Itatekeleza Dhamira Yake ya Usalama na Ustawi”. Kaulimbiu hii inasisitiza jukumu la forodha katika kuhakikisha usalama wa bidhaa na kukuza ustawi wa kiuchumi.

Katika maadhimisho haya, TRA imeonyesha dhamira yake ya kuhakikisha biashara halali zinastawi na kuimarisha ukusanyaji wa mapato, huku ikionya vikali wale wanaojihusisha na uingizaji wa mali za magendo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
594,000SubscribersSubscribe

Latest Articles