24.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 27, 2023

Contact us: [email protected]

Mali za CCM bado kaa la moto

Na GRACE SHITUNDU, DAR ES SALAAM

KUNA kila dalili zinazoonyesha kuwa mwafaka kuhusu mali za Chama Cha Mapinduzi (CCM) bado haujafikiwa, baada ya Baraza la Wadhamini kutangaza kufanya uhakiki mwingine nchi nzima.

Hatua hiyo imekuja ikiwa imepita miezi sita tangu ripoti ya Tume ya uhakiki wa mali za CCM iliyokuwa ikiongozwa na Dk. Bashiru Ally  (ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Chama hicho), kukabidhiwa kwa Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Dk. John Magufuli.

Kamati hiyo ilichukua muda wa miezi mitano kukamilisha kazi hiyo kwa kukusanya taarifa, kuhakiki na kuchambua nyaraka zenye maelezo kuhusu idadi, aina na hali ya mali zinazomilikiwa na kusimamiwa na chama hicho.

Pia iliangalia vyanzo vya udhaifu wa mifumo na taratibu za usimamizi wake, ilikusanya ushauri mbalimbali na kutoa mapendekezo ya mikakati na namna ya kusimamia mali hizo.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili sababu za kufanya uhakiki mwingine, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini, Anna Abdallah, alisema ripoti ya kwanza ya Tume ya Dk. Bashiru haikuweza kuzifikia mali zote za chama hicho.

Alisema mali zote za CCM kwa mujibu wa Katiba zinasimamiwa na Baraza la Wadhamini, ambalo ndilo lenye mamlaka ya kuzihakiki, kuzithibitisha na kuzirasimisha.

“Kama kuna mambo yatatakiwa kuangaliwa upya tutasema, lakini sasa ni lazima tuzipitie kwa kuzihakiki ili kurasimisha mali zilizopitiwa na Tume sambamba na zile ambazo hazikupitiwa na Tume.

“Kile hakikuwa kikao cha chama, na wale walikuwa tu wametumwa kufanya ile kazi, sasa imeletwa kwa wenye mali na ndiyo maagizo ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), kwamba hayo mambo yapelekwe rasmi kwenye Baraza la Wadhamini,” alisema.

Alisema Tume iliyoongozwa na Dk. Bashiru haikupita kila mahali, hivyo ilichokifanya ilikuwa kama ‘sample’ tu.

“Kwa hiyo tutapitia hiyo ‘sample’ na yale yote yaliyobaki, yaani mali ambazo hazijapitiwa na tume…tumejipanga vizuri na makao makuu ya chama yameshapeleka wataalamu kila mahali kila mkoa.

“Wataalamu hao wamepitia mali zote zote zilizopitiwa na Tume na zile ambazo hazikupitiwa kwa kufanya ziara nchi nzima,” alisema.

Alisema katika kuhakiki wataigawa nchi kwa kanda nane, ambapo kila mjumbe atakwenda kanda moja na atakutana na kamati za siasa za mikoa ili kulinganisha kile watakachokiona na ripoti iliyoandikwa ya kamati iliyoongozwa na Dk. Bashiru.

Mwanzoni wa wiki hii Mwenyekiti huyo akinukuliwa na gazeti moja la kila siku (sio Mtanzania), alisema baraza hilo limetoa maagizo sita, ili kuimarisha udhibiti wa mali za chama hicho.

Alisema miongoni mwa maagizo hayo ni kubatilisha makubaliano yote yaliyohusisha uhamishaji wa miliki za mali za CCM kwenda kwa watu wengine pasipo kuzingatia taratibu muhimu, ikiwa ni pamoja na uthaminishaji sahihi wa mali husika.

Pia agizo lingine ni kutaka kuanzia sasa mali zote za CCM ziandikishwe kwa jina la Baraza hilo na si ngazi za utawala za chama na taasisi zake.

Alisema agizo jingine ni kuhakikisha kuwa ifikapo Oktoba mwakani ardhi, mashamba na mali nyingine zote za CCM ziwe zimerasimishwa na kuwa na hatimiliki.

Aidha, alisema kuanzia sasa masuala ya mashtaka kuhusu mali za CCM linalotakiwa kushtakiwa ni Baraza la Wadhamini na si vinginevyo.

Jingine ni kwamba Baraza limeamua kuanzia sasa CCM iwe mfano wa ulipaji wa majengo, ardhi na mali zake zote nchini.

Pia alisema baraza limekasimu madaraka yake kwa kamati za siasa za mikoa na hivyo masuala yote ya mali, isipokuwa miradi mikubwa itakuwa chini ya kamati hizo na wala si za matawi, kata, wilaya au taasisi zake.

Akifafanua katika hilo, alisema miradi mikubwa itakuwa chini ya Baraza la Wadhamini moja kwa moja.

Mei 21 mwaka huu, wakati wa Dk, Bashiru akikabidhi ripoti kwa Rais Magufuli, alisema Tume yake ilibaini uwepo wa upotevu mkubwa wa mali za CCM uliosababishwa na mikataba mibovu, ubadhirifu, wizi, usimamizi mbaya wa mali, utapeli na ukosefu wa maadili katika uendeshaji wa miradi.

Dk. Bashiru alisema pamoja na mambo mengine, Tume iliangalia vyanzo vya udhaifu wa mifumo na taratibu za usimamizi wa mali, lakini pia ilikusanya ushauri mbalimbali na kutoa mapendekezo ya namna ya kuzisimamia.

Alisema uhakiki huo ulifanyika kwa kutembelea maeneo yenye mali za CCM, kuwahoji watu mbalimbali, wakiwamo viongozi waliohusishwa na mali zilizokuwa zikihakikiwa, upitiaji wa nyaraka na kufuatilia uhalisia katika ofisi za mamlaka husika, kufanya uchambuzi wa taarifa na kutoa mapendekezo,” alisema.

Kwa upande wake, Rais Magufuli  aliwaagiza wajumbe wa sekretarieti ya CCM waliohudhuria wakati uwasilishwaji wa ripoti hiyo kuanza kufanyia kazi baadhi ya mambo yaliyo ndani ya uwezo wao na  kwamba masuala mengine yataamuliwa na vikao vikuu vya Chama hicho.

Uamuzi wa Rais Magufuli kuunda Tume hiyo iliyoongozwa na Dk. Bashiru na hata kutoa ripoti yake ilionekana kupeleka joto kubwa ndani ya chama hicho, kutokana na kuwapo kwa taarifa kuwa, wapo baadhi ya wana CCM walioingia mikataba mibovu kwenye mali hizo, lakini kujimilikisha na hata wengine kuziuza pasipo kufuata utaratibu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,213FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles