27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Malengo yanaweza kubadili tabia ya mtoto

Na CHRISTIAN BWAYA

Mwanangu wa miaka saba alikuwa na tatizo la kupenda sana kununua vitu vitamu. Kila siku alikuwa ombaomba wa chochote kinachomtosha kwenda dukani. Sikupenda tabia hii. 

Mbali na kuharibu meno yake, kulikuwa na tatizo la kutokujizuia. Ilifika mahali tunagombana kwa sababu tu hajapata chochote kukidhi hamu yake ya kununua ‘ice cream’, ‘chocolate’ na vinavyofanana na hivyo. Jitihada za kubadili tabia hii ya kupenda vitu visivyo na faida kwake hazikuzaa matunda. 

Nikaona nijaribu mbinu nyingine. Siku moja jioni nikamrushia swali;  ‘Ungekuwa na hela zako mwenyewe ungetaka kufanya nini mwezi wa 12 mwakani?’ Swali gumu. Aliomba ufafanuzi. Nikafafanua. Hatimaye akasema anachotaka. Nikaona ni lengo dogo. Nilitaka awe na lengo kubwa la kufanyia kazi. Katika umri wake, fahari ya kufikia malengo ni motisha tosha.

Nikamsaidia kuona zaidi: ‘Hivi unajua unaweza kabisa kujilipia ada ya shule ukiamua?’ Ikaonekana naongea ‘mazingaombwe.’ Baada ya maswali yake kadhaa tukafikia muafaka kuwa inawezekana.

Nikaamua kupanua lengo lake; ‘Ungependa kwenda wapi mwezi wa 12 wakati wa Krismas ijayo?’ Macho yake yakachangamka kwa furaha. Nilikuwa nimegusa jambo muhimu kwake.

‘Sasa nataka nikupe mtihani utakaokuwezesha kufanya yote hayo kwa fedha zako mwenyewe.’ Akasisimka. Nikamweleza mpango ulivyo; ‘Tunataka kuwa na kiasi kitakachokutosha kulipa ada yako, kwenda kufurahia Krismas kule ulikochagua na kununua mahitaji yako uliyonitajia.’ 

‘Nitakuwa nakupa kazi za kufanya na ukizikamilisha mwisho wa wiki nitakulipa.’ Naelewa hatari ya kutumia fedha kama motisha kwa mtoto. Hata hivyo, lengo langu lilikuwa kumfanya ajione anawajibika na kipato chake na wakati huo huo afikie malengo aliyojiwekea.

‘Fedha utakazopata, utaziweka kwenye kibubu. Kila wiki utaweka kiasi cha fedha kinachoonekana kwenye karatasi hii ya mtihani.’ Nikamwonyesha katarasi iliyokuwa na utaratibu wa kuweka kiasi fulani cha akiba kwa wiki. Kiasi hicho kinaongezeka mara mbili kila wiki inayofuata. 

‘Ukishaweka fedha yako kwenye kibubu, unatiki hapa.’ Nikamwonyesha kisanduku cha kutiki mbele ya tarakimu zinazoainisha kiasi cha fedha atakachoweka kila wiki. 

‘Una swali lolote?’ Maswali mengi. Nikamwelewesha. Hatimaye akauliza swali la mwisho, ‘Tunaanza lini?’ Nikamwambia, ‘Utakapokuwa tayari aniambie tukatengeneze kibubu.’ Hapo nilikuwa napima uwezo wake wa kufuatilia mambo ya msingi.

Kesho yake sikusikia akiongea suala la kibubu. Wiki moja ikapita sisikii habari za kibubu. Nikapatwa na wasiwasi. Ikabidi nimuulize kulikoni. 

‘Baba nilikuwa bado nafikiria utakuwa unanipa kazi gani hizo mpaka unilipe?’ Nikaelewa hoja yake. Tukaliweka hilo vizuri.

Kesho yake akanikumbusha kibubu. Nikajua somo limeeleweka. Tukamwomba mama yake atutengenezee. Nikamkabidhi karatasi inayomwongoza kiasi cha kutumbukiza kwenye kibubu. Nikamwomba aeleze shughuli nzima itakavyokwenda. Nikagundua anaelewa. Kazi ikaanza.

Nilichokiona kimenifunza. Wiki ya 10 sasa mtoto haombi tena fedha ya kwenda kununua ‘chocolate’ wala ‘ice cream.’ Kila anachokipata, anakitumia kupunguza deni kwenye mtihani wake wa ‘kibubu.’ Inavyoonekana lengo lililokidhi mahitaji yake limebadili tabia yake. 

Kilichonifurahisha zaidi, sasa hivi anaomba ‘kazi’ za kufanya ili apate fedha za kupunguza ‘deni’ lake la ‘kibubu.’ Kuombaomba fedha za kwenda kutumia, kumepungua kwa kiasi kikubwa. Binti yangu anaonekana kuelekeza nguvu zake katika kuhakikisha lengo lake limetimia. Kama kuna jambo umejifunza, bado hujachelewa. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles