30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Makufuli yafungwa darajani, funguo yatupwa baharini kutunza ndoa

Na FARAJA MASINDE

MAPENZI yanachukua sehemu kubwa katika maisha ya binadamu na katika kuyaenzi kumekuwa na mambo mengi yanayofanywa na wapenzi ili kudumisha penzi.

Kwa nchi zetu za Afrika, mara nyingi suala la kufunga ndoa huishia kula kiapo kanisani na kisha kutunukiwa vyeti na wakati mwingine kuambatana na tafrija kulingana na uwezo wa wanandoa wenyewe au familia zao.

Japo pia wapo wale ambao huwa wanakaa kimya baada ya kutoka kanisani kama alivyofanya Rais Dk. John Magufuli.

Lakini kama hufahamu ngoja nikufahamishe leo kuwa huko duniani kwenye mataifa yaliyoendelea kuna utaratibu ambao wanandoa wanautumia pale wanapofunga ndoa mbali na kile kiapo cha kanisani.

Iko hivi, wanandoa hao pindi tu wanapotoka kanisani au hata ndoa za namna nyingine basi hulazimika kupita kwenye kibanda kilichokaribu na kununua kufuli jipya, namaanisha kufuli unalolifahamu wewe kisha huenda kulifunga kwenye madaraja maalum kwa ajili yao na funguo hutupwa baharini.

Fahamu kuwa kwenye makufuli hayo wenzi hao huandika majina yao mfano (Kelvin & Camille) kisha hufunga na kutupa ufunguo kama ishara ya kiapo.

Sababu kubwa ya kufungwa kwa kufuli hizo na funguo kutupwa ndani ya maji ni kuwa iwapo mtataka kuachana basi mtalazimika kuzama ndani ya maji kwa ajili ya kuisaka funguo yenu hadi muipate na msipofanikiwa basi mtalazimika kurudisha mapenzi yenu na kufuta kabisa mpango wenu wa awali wa kutaka kutengana.

Utaratibu huu umekuwa ukitumika hasa kwenye nchi za barani Ulaya na kwingineko.

Lakini mjini Paris nchini Ufaransa ndiko kunaonekana kuwa kinara zaidi katika daraja la Pont Des Arts ambalo ni daraja la watembea kwa miguu.

Hili ndilo daraja lenye makufuli mengi zaidi duniani na unaambiwa kuwa kiwango cha makufuli yaliyoko hapo ukisema uyabebe kwenye gari basi utahitaji semitrailer mbili ili kuweza kuyamaliza.

Hapo kuna maelfu ya makufuli yaliyowekwa huku mengine yakiendelea kuwekwa ikiwa ni ishara ya kiapo.

Lakini pia, mbali na wakazi wa eneo husika pia hata watalii wamekuwa wakifika kwenye mji huo na kununu makufuli na kisha kuyafunga darajani hapo.

Hatua hiyo pia imechangia kuchochea uchumi wa wauza makufuli ambapo moja huuzwa kati ya Euro tano hadi 10 sawa na Sh 12,000 hadi 20,000.

Mbali na Ufaransa, kuna nchi kama Marekani ambapo utaratibu huo unafanyika kwenye daraja la Brooklyn, pia kuna miji kama Brussels Ubelgiji, Berlin Ujeruman na Moscow Urusi katika madaraja ya Luzhkov na Vodootvodny Canal.

Italia nako hawajabaki nyuma kwani huduma hiyo utaipata kwenye madaraja ya mjini Rome na Venice lakini kuna nchi nyingi kama Serbia, China, Korea Kusini na Jamhuri ya Czech.

PARIS, FRANCE – FEBRUARY 14: The Pont Des Arts is covered in roses to celebrate Valentine’s Day on February 14, 2014 in Paris, France. (Photo by Kristy Sparow/Getty Images)

Hata hivyo, wenzi katika mji wa Brooklyn  Marekani watalazimika kusaka daraja jingine baada ya mamlaka nchini humo kuondoa makufuli 6,000 kwa kile ilichosema kuwa ni utunzaji wa mazingira.

Hivyo, huo ni utaratibu unaolezwa kama sehemu ya kutunza ndoa kwenye mataifa hayo.

Unafikiri wewe unaweza kulifanya hili iwapo itatokea kwa hapa Tanzania? Jibu baki nalo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles