BRUSSELS, UBELGIJI
Kuna uwezekano mkubwa wa Uingereza kujiondowa kwenye Umoja wa Ulaya mwishoni mwa mwezi huu bila makubaliano ya kibiashara, kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, na Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya, Ursula von der Leyen.
Viongozi hao wawili walikuwa wamewaongezea muda wawakilishi wao kwenye mazungumzo ya kusaka makubaliano hayo ya kibiashara, lakini hivi leo Ijumaa Desemba 11, Johnson amewaambia waandishi wa habari kwamba huenda Januari Mosi ikafika bila ya makubaliano yoyote.
Kauli kama hiyo imetolewa na von der Leyen wakati akiwaarifu viongozi wa Umoja wa Ulaya juu ya mwenendo wa mazungumzo hayo.
Masuala tete yanayokwamisha kufikiwa makubaliano hadi sasa ni uvuvi na forodha. Hata hivyo, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema ana matumaini pande hizo zitafikia makubaliano juu ya mahusiano yao ya siku zijazo, ambayo yataheshimu pande mbili pamoja na kulinda maslahi ya Ulaya.