26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

MAKOSA YANAYOFANYWA NA MADAKTARI KWA WAGONJWA

 

 

Na JOACHIM MABULA,

UNAPOKUWA mgonjwa na kupelekwa hospitali, unakuwa na amani kwa kuwa uko katika mikono salama. Hudhani kwamba daktari au muuguzi mwenye ujuzi anaweza kufanya makosa ya kitiba kwako na kwa watu unaowapenda.

Makosa ya kitiba yanaweza kusababisha madhara katika mwili na wakati mwingine hugharimu maisha kabisa.

Taaluma ya tiba na upasuaji hubadilika kila uchwao, hivyo madaktari na wahudumu wengine wa sekta ya afya wanaweza kufanya makosa katika kutoa bainisho (diagnosis) la mgonjwa pamoja na matibabu ambayo yanahusisha upasuaji pale wanapotumia utalaamu uliozoeleka na si ule mpya ulioboreshwa.

Makosa ya kitiba hutokea pale mgonjwa anapodhurika kutokana na huduma za ushauri, tiba na upasuaji alizopata kwa daktari au wahudumu wengine wa sekta ya afya. Mashtaka juu ya wahudumu wa afya katika nchi nyingi zinazoendelea ni machache kwa maana watu wengi hawana uelewa mkubwa wa mambo mbalimbali kuhusu matibabu, ikitokea mhudumu yoyote wa afya kashtakiwa mara nyingi hushtakiwa na watu wenye elimu na kipato kikubwa kiujumla.

Ni vyema kutambua mteja/mgonjwa anaposhindwa kuridhika na huduma za afya zinazotolewa katika kituo cha kutolea huduma za afya iwe ni zahanati au hospitali haina maana kuna makosa ya kitiba yalitokea.

Kukosea na kuchelewa kutoa bainisho (diagnosis) la hali ya afya ya mgonjwa ni moja ya tatizo kubwa katika makosa ya kitiba. Daktari anapokosea bainisho la ugonjwa hatari kama kupanda kwa shinikizo la damu (high blood pressure) au upungufu mkubwa wa damu (severe anaemia), mgonjwa anaweza kukosa matibabu ambayo yangeweza kuzuia madhara zaidi na hata kusababisha kifo.

Kuangalia alichokifanya daktari kwa mgonjwa au ambacho hakukifanya kwa mgonjwa na alipaswa kufanya ndio ufunguo wa kutambua makosa ya kitiba. Mara nyingi hulinganishwa kile ambacho angekifanya au asingekifanya daktari mwenye sifa za kitaaluma na ujuzi kama yule daktari aliyefanya makosa.

Matatizo ya mfumo wa fahamu kama utahira na degedege na majeraha ya viungo kama vile mkono au mguu kupinda kwa mtoto mchanga yanaweza kutokea pale daktari au mkunga anapomzalisha mjamzito bila kuwa au kutotumia ujuzi stahiki. Madaktari na wakunga wanaweza kuchelewa kumzalisha mjamzito na kusababisha mtoto kuchoka na kukosa hewa kabla hajazaliwa au wanaweza kutumia mbinu ambazo hazina ufanisi wakati wa kumzalisha mjamzito.

Nini wajibu wa madaktari kwa wagonjwa?
Kulingana na shida iliyomleta mtu hospitali, daktari hutoa bainisho la ugonjwa (diagnosis), hupendekeza aina ya vipimo vya kufanya, aina za dawa kwa ugonjwa mahususi na kufuatilia maendeleo ya mgonjwa. Madaktari wanawajibika kwa matendo yao na maagizo wanayotoa kwa wasaidizi wao kama wauguzi na wanafunzi walio katika mazoezi kwa vitendo.

Majukumu makubwa ya madaktari ni pamoja na kutoa bainisho la ugonjwa na kutibu, hii ina maana wanapaswa kufuata njia zinazopaswa ili kuweza kutambua tatizo la mgonjwa kwa kutumia taaluma ya kisasa zaidi kulingana na hali na ngazi ya kituo cha kutolea huduma za afya. Pia madaktari wanapaswa kuwaeleza wagonjwa wanachoumwa, matibabu yake, hasara na faida za matibabu hayo na kitakachotokea wasipopata matibabu haraka.

Kabla ya kumhudumia mgonjwa daktari anapaswa kumweleza mgonjwa anachotaka kumfanyia ili aweze kutoa ridhaa yake mwenyewe kabla ya kuhudumiwa. Ikiwa mgonjwa yupo mahututi basi ndugu anaweza kumsaidia kutoa ridhaa kwa maandishi. Wakati wote wa kutoa huduma wahudumu wa sekta ya afya wanapswa kuzingatia faragha ya mteja wao pamoja na kutunza siri za wateja wote wanaowahudumia.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles