27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Makosa ya usajili Yanga, Simba

6Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

TANGU Ligi Kuu Tanzania Bara ianze msimu huu, tayari michezo minne  imechezwa katika viwanja mbalimbali  huku tukishuhudia makosa ya usajili  yaliyofanywa na klabu pendwa za   Simba na Yanga kwa  kushindwa kuboresha eneo la  kiungo ukabaji.

Licha ya Yanga kuwa na mchezaji  kiraka, Mbuyu Twite,  mwenye uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali uwanjani kama vile beki wa kulia, kati, kushoto, na kiungo mkabaji, wameendelea kumtegemea Mzimbabwe Thaban Kamusoko katika nafasi hiyo ya kiungo ukabaji ambayo si namba yake halisi.

Kamusoko humudu zaidi kucheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, kitendo cha kucheza kama kiungo mkabaji kilimfanya kuwa na wakati mgumu katika michezo ya kimataifa ambayo Yanga ilikuwa ikishiriki hivi karibuni.

Udhaifu wa Kamusoko katika namba hiyo ulionekana wazi na kuigharimu timu yake, wakati  ilipocheza michezo yote ya  ya Kundi A katika Kombe la Shirikisho  hususan dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya  Kongo na   Medeama ya Ghana.

Hivyo, kocha mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm, alitakiwa kulitibu tatizo hilo mapema kabla ya kutumia Sh milioni 200 ili kuipata saini ya Obrey Chirwa, ambaye hakuwa na umuhimu wowote kutokana na namba yake kuwa na wachezaji zaidi ya wawili, Donald Ngoma, Amiss Tambwe na Malimi Busungu.

Ilikuwa vigumu kwa Pluijm kutoliona tatizo hilo ambalo kwa sasa linazidi kuathiri uwajibikaji wa wachezaji wa Yanga uwanjani.

Kwa kumtegemea Kamusoko, Yanga inaweza kupata matokeo mazuri baadhi ya michezo ya ligi, lakini itaendelea kupata shida wanapokuwa katika michezo ya kimataifa.

Sababu ya wao kumudu michezo ya ligi inatokana na kuizoea ligi hiyo  ambayo wamefanikiwa kutwaa ubingwa mara mbili mfululizo bila kutamba katika anga za kimataifa.

Jambo hilo pia linaweza kutokea hata kwa mahasimu wao, Simba ambayo muda wowote wanaweza kuwa na wakati mgumu wa kupata mbadala wa  Jonas Mkude, endapo nyota huyo ataumia na kutakiwa kuwa nje kwa muda mrefu.

Mkude kwa muda mrefu amekuwa akicheza nafasi ya kiungo mkabaji wa timu hiyo licha ya ujio wa Justice  Majabvi msimu uliopita, ambapo mara kadhaa alikuwa mbadala wa kiungo huyo.

Ni muda sasa tangu dirisha la usajili lifungwe, huku timu hiyo ikifanikisha  kwa kiasi kikubwa kwa wachezaji wa nafasi ya ushambuliaji na winga baadhi yao akiwamo Laudit Mavugo, Fredrick  Blagnon, Mussa Ndusha, Shiza Kichuya,  Muzamil Yassin na Jamal Mnyate badala  ya kutafuta mbadala wa kiungo  Mzimbabwe Majabvi ambaye kwa sasa hayupo katika timu hiyo.

Kocha wa zamani wa Yanga na Bandari ya Mtwara, Kenny Mwaisabula, alisema  tatizo hilo lipo kwa timu ya Yanga na si   Simba, ambao wana viungo halisi watatu na wanamudu vema kucheza nafasi hiyo.

“Mkude, Yassin, Kazimoto na Said Ndemla hao ni baadhi tu ya wachezaji namba sita imara kwa Simba.

“Upande wa Simba hauna tatizo kabisa katika hilo, wasiwasi wangu upo kwa Yanga ambao huwatumia Kamusoko na Haruna Niyonzima,” alisema Mwasaibula.

Mwasaibula alisema wasiwasi wake   kwa Yanga upo  endapo Kamusoko atapata majeraha na kulazimika kukaa nje kwa muda, Yanga itaathirika zaidi kutokana na kutokuwa na mbadala sahihi wa namba ya mchezaji huyo.

“Niyonzima na Kamusoko wote ni viungo washambuliaji na wanamudu vema nafasi hiyo wakati Said Juma ‘Makapu’ hucheza kama winga.

“Kiufundi, Yanga wana kazi kubwa sana, wanapokutana na timu imara yenye kocha mtaalamu wa mbinu.

“Hivyo, bado nasisitiza Simba wapo vizuri kitimu lakini Yanga kuna tatizo la aina hiyo ya kiungo, ambapo kama ningekuwa Pluijm ningelazimika kuingia sokoni katika dirisha dogo lijalo ili kupata mwafaka wa namba hiyo,” alisema Mwaisabula.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles