Makosa ya Maalim Seif kumrejesha Lipumba CUF?

Lipumba

Na JONAS MUSHI – DAR ES SALAAM

PROFESA Ibrahim Lipumba, ambaye Agosti 6, mwaka jana aliandika barua ya kujiuzulu wadhifa wa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), huenda akarejea kwenye nafasi yake kwa sababu ya makosa ya kutotekelezwa kwa matakwa ya Katiba yaliyofanywa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Hayo yamebainika wakati vikao vya juu vya CUF vikianza kuketi leo katika ofisi za makao yake makuu, yaliyopo Buguruni, Dar es Salaam, chini ya ajenda moja ya kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi za uongozi zilizo wazi, ikiwemo nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti Bara pamoja na Wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa.

Duru za habari kutoka ndani ya CUF zimeeleza kuwa, Katiba ya chama hicho, Ibara ya 117 (1), (2) inaeleza ili kiongozi wa chama ajiuzulu wadhifa wake, analazimika kumwandikia barua Katibu Mkuu wake na yeye kuipeleka barua hiyo katika mamlaka iliyomchagua kiongozi huyo kwa ajili ya kumjadili na kutoa uamuzi.

Kwamba matakwa hayo ya kikatiba ya CUF hayakufuatwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif, ambaye kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu Prof. Lipumba alipomwandikia barua ya kujiuzulu, Agosti 6, 2015, hajapata kuiwasilisha katika mamlaka iliyomchagua kwa ajili ya kuijadili na kuitolea uamuzi.

Baadhi ya viongozi na wanachama wa CUF waliozungumza na MTANZANIA Jumamosi mapema wiki hii, walijielekeza katika hoja hiyo ya kikatiba kuwa kimsingi, Prof. Lipumba bado hajajiuzulu, bali alitangaza kujiuzulu na baadaye kuonyesha nia ya kujiuzulu kwa kumwandikia barua Katibu Mkuu, Maalim Seif, ambaye hadi sasa ameikalia.

“Zipo sababu mbalimbali zinazoweza kumrudisha kuvaa viatu vyake na kimsingi zinatokana na kile kinachoonekana ni uzembe na makosa yaliyofanywa na Katibu Mkuu, Maalim Seif katika kulishughulikia suala hili la Prof. Lipumba.

“Leo Baraza Kuu la Uongozi Taifa la chama linakutana ikiwa ni maandalizi ya Mkutano Mkuu maalumu unaotarajiwa kufanyika kesho na ajenda ni kufanya uchaguzi kwa nafasi zilizo wazi, ikiwemo nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti Bara pamoja na Wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa, lakini uchaguzi wa mwenyekiti wa taifa hauwezi kufanyika bila kwanza kujadili barua yake ya kujiuzulu na kutoa uamuzi,” alisema mmoja wa viongozi waandamizi wa CUF, ambaye jina lake tunalihifadhi.

Wakati CUF kikianza vikao vya juu leo, wanachama na wafuasi watiifu kwa Prof. Lipumba wanadaiwa kujipanga kuchukua hatua za kisheria endapo barua yake ya kujiuzulu haitajadiliwa kabla ya uchaguzi, wakisimamia hoja kwamba utakuwa ni ukiukwaji wa katiba ya chama.

Kujipanga huko kunaelezwa kuwa kunatokana na kuwepo kwa taarifa zinazoonyesha mikakati ya viongozi wanaompinga kutaka kuvitumia vikao hivyo kubariki kuondoka kwake bila kufuata katiba ya chama.

Taarifa nyingine zilizopatikana kutoka ndani ya chama hicho zimeeleza kuwa uamuzi wa kufanya Mkutano Mkuu kesho ukiwa na ajenda mbili ambazo ni kujadili barua ya kujiuzulu kwa Prof. Lipumba na kufanyika kwa uchaguzi wa kujaza nafasi za uongozi zilizo wazi, umelenga kuokoa gharama za kufanya mikutano miwili na pia kukidhi matakwa ya kisheria ya kuhakikisha chama hakikosi viongozi wakuu kwa zaidi ya miezi 12, kwa mujibu wa sheria ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

“Endapo barua ya Prof. Lipumba itajadiliwa kipindi hiki ambacho tayari kuna wajumbe wa mkutano huo wameonyesha wazi kutaka arudi, upo uwezekano wa kutokuwa na uchaguzi kwa nafasi hiyo na badala yake Profesa atakabidhiwa mikoba yake.

“Lakini ili Profesa arudi, inahitajika nguvu kubwa kutoka kwa wajumbe wa mkutano mkuu, kwani tayari imeonekana kuwapo viongozi wakuu wa chama hicho wa Zanzibar na Bara ambao hawamtaki.

“Hii inathibitishwa na ukimya wa Maalim Seif, baada ya Prof. Lipumba kumwandikia barua nyingine ya kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu,” alisema mmoja wa wajumbe wa maandalizi ya vikao hivyo.

Kumbukumbu zilizopo kuhusu sakata la kujiuzulu kwa Prof. Lipumba zinaonyesha kuwa hatua ya kutengwa na viongozi wenzake inathibitishwa na kauli walizokaririwa kuzitoa kuwa Katiba ya CUF hairuhusu kiongozi aliyejiuzulu kurudi kwenye nafasi yake kwa sababu atakiharibu chama.

Miongoni mwa viongozi waliokaririwa wakitoa kauli za aina hiyo ni Twaha Taslima, ambaye anakaimu nafasi ya Prof. Lipumba, kuwa hawezi kurudi katika nafasi aliyojiuzulu kwa sababu atakuwa anakiuka Katiba.

Mbali na Taslima, kiongozi mwingine wa CUF aliyekaririwa kutoa kauli za kutokubali Prof. Lipumba kurudi kwenye wadhifa wake ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, kuwa hawezi kuwa na nia njema ya kukijenga chama hicho endapo atarudishwa kwenye nafasi aliyoikataa.

Mazrui alikaririwa akieleza zaidi kuwa CUF kimefanya mambo mengi bila Prof. Lipumba na kwamba chama hicho kilikwisharidhia kuitisha mkutano wa uchaguzi kujaza nafasi hiyo. Alisisitiza kuwa haoni kinachomrudisha kwa sababu mambo yaliyomwondoa bado yapo.

Hata hivyo, baadhi ya wanachama wanaomuunga mkono Prof. Lipumba wamekuwa wakieleza kuwa pamoja na hoja za viongozi wenzake za kumkataa, walifanya kosa kutoitisha Mkutano Mkuu kujadili barua yake ya kujiuzulu kabla ya wanachama kugawanyika pande mbili za wanaomuunga mkono na wanaompinga.

Inaelezwa kuwa Maalim Seif alipaswa kukitumia vizuri kipindi cha baada ya kumaliza uchaguzi mkuu wa mwaka jana kumwondoa Prof. Lipumba kwa sababu wanachama wengi walikuwa bado wameshikamana na walikuwa wakimuangalia mwenyekiti wao huyo kwa jicho la msaliti ndani ya chama.

Katika mpasuko wa sasa, baadhi ya wanachama wanamwangalia Twaha Taslima kama kiongozi aliyeshindwa kuvaa viatu vya Prof. Lipumba na kwamba ndani ya CUF hakuna mtu anayeonekana kuwa na sifa ya uwezo wa kurithi mikoba yake.

Wajumbe kadhaa wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa linaloketi leo wamedokeza kuwa mpasuko uliopo sasa ndani ya CUF huenda ukaathiri kikao cha kesho kwa wajumbe kutoafikiana kuhusu hatima ya uenyekiti wa Prof. Lipumba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here