Makonda: Nakosa usingizi kwa kuhujumiwa

0
635
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

AVELINE KITOMARY na ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema amekuwa hapati usingizi kutokana na watu kutokuwa waaminifu na kutotekeleza majukumu yao, hatua inayomfanya aende mwenyewe maeneo ya kazi kutafuta taarifa.

Makonda alisema hayo Dar es Salaam jana, alipokuwa akizungumza na viongozi wa kidini wakati wa kongamano maalumu kuelekea uchaguzi, uchumi wa viwanda, amani, mahusiano, uzalendo na ustawi wa taifa.

Katika kongamano hilo, Makonda alielezea mafanikio ya Mkoa wa Dar es Salaam.

“Ninakosa usingizi, mambo mengi yamebadilika kwa sababu watu wengi si waaminifu, hawana hofu ya Mungu, hawatimizi majukumu yao na hupata kila sababu ya kueleza wamekwama, wengine wanakwama hata kabla hawajaanza.

 “Wengine wamekuwa wakitengeneza mabomu ili wenzao walipuke halafu wanakaa pembeni wakishangilia. Na hii ndiyo sababu iliyotufanya mimi na RAS (Ofisa Tawala Mkoa) tumeamua kubadilisha mfumo wa utendaji. Badala ya kuwa watu wa kupokea taarifa ofisini, sisi tunaenda ‘site’ (sehemu za kazi) kutafuta taarifa,” alisema.

Alimweleza mgeni rasmi katika kongamano hilo, Naibu Waziri Tamisemi ambaye pia ni Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (CCM) ambaye alimwakilisha Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kuwa jimbo lake barabara imeanza kujengwa, baada ya kuwaweka ndani wakandarasi.

Makonda alisema ni wazi kungekuwa na utamaduni wa watu kuwa waadilifu, kazi zingekuwa zinakwenda vizuri ila kwa kuwa watu wamekosa hofu ya Mungu mambo si kama alivyokuwa akitarajia kwakuwa wengi hawatimizi wajibu wao.

“Kupitia kamati hii, nimeona mafanikio makubwa sana na ninaona kama tungekuwa na utamaduni wa watu kuwa waadilifu, kazi zingekuwa rahisi sana, lakini watu si waaminifu hata kidogo.

 “Tatizo watu hawatimizi wajibu wao, halafu mzigo ameamua kuubeba Makonda, haiwezekani, kwa hiyo mzigo nimeamua kuupeleka msalabani, hapigwi mtu hapa, watapigwa wao,” alisema.

Alisema wameamua kuingia mitaani kwa kuwa nia ya Serikali katika Mkoa wa Dar es Salaam ni kuhakikisha ifikapo 2020 miradi yote isiyopungua Sh trilioni 3 iwe imekamilika.

Makonda alisema baada ya kupata fedha kwa Hospitali ya Wilaya ya Ubungo, anaendelea kusimamia kuhakikisha eneo linakuwa tayari na ujenzi unaanza wiki hii.

“Nikitoka hapa ninakimbia kwenda Ubungo kuangalia eneo la kujenga hospitali ya wilaya, nimepata pesa juzi na ikiwezekana ikichelewa, Jumatano ujenzi uanze.

“Nimeshapata wajenzi kutoka kwa Brigedia Mbuge (Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa-JKT) na amemwaga kikosi chake cha JKT na ninataka ikiwezekana ndani ya miezi minne wana-Ubungo wawe wanatibiwa,” alisema.

Alisema miradi hiyo inayoendelea, inazalisha ajira nyingi kutoka kwa mtu mmoja hadi hatua ya viwanda na tayari ameshaagiza katika Mkoa wa Dar es Salaam hakuna bidhaa za ujenzi wa miradi zitakazonunuliwa kutoka nje, ikiwamo saruji, nondo, mabomba na vitu vyote vitakavyotumika.

UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA

Aliwaomba viongozi wa dini kuhamasisha watu kwenda kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 24 kwa kuchagua viongozi waadilifu.

“Huko kwenye mitaa ndiyo kuna viwanja feki na migogoro ya ardhi isiyokwisha, ndiko kuna mitaro na mifereji ya maji kwenye makazi, hawa viongozi ndio chimbuko la maendeleo kuanzia ngazi ya mitaa,” alisema.

WANAOTELEKEZA WATOTO

Katika hatua nyingine, Makonda alisema Serikali iko mbioni kutunga sheria itakayowabana watu wanaotelekeza watoto, ikiwemo watumishi wa Serikali wenye tabia hiyo.

Alisema miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakibezwa lakini yameonyesha mafanikio makubwa, ni hatua yake ya kuwakusanya wanawake wote waliotelekezewa watoto.

Makonda alisema tayari wako kwenye mchakato wa kutunga sheria ya kuwabana wazazi wanaotelekeza watoto na kusababisha kuongezeka kwa idadi ya watoto wa mitaani.

 “Tunatengeneza sheria kuhakikisha kwamba mzazi amemtelekeza mtoto, tunahakikisha kama una posho inakatwa huko huko na kupelekwa kulea mtoto.

 “Sheria hii itakuwa ni kali kiasi itahakikisha kusaidia mtu anaogopa kumpa mtu mimba kama mtu anavyoogopa Ukimwi. Sheria hii inatakiwa kuhakikisha kwamba mama akipata mimba tu na kwamba wewe ndiye muhusika wa mimba unaanza kutoa huduma,” alisema.

KAULI YA WAITARA

Kwa upande wake, Waitara alisema Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa dini, hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi ili kudumisha amani na mshikamano katika jamii.

Aliwapongeza viongozi wa dini wa kamati ya amani kwa kuhamasisha amani na kwamba mchango wa taasisi za kidini umechangia kujenga ustawi mzuri katika Taifa.

“Tunawapongeza viongozi wa dini hasa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam, kamati hii sasa imeimarika katika mikoa mingi nchini. Nawashukuru pia kwa kuunga mkono juhudi za taifa kwa ajili ya uchumi wa viwanda.

“Taasisi za kidini zimekuwa zikihamasisha amani na kusababisha kuwepo kwa uwekezaji, ukuaji wa uchumi, viwanda. Haya ni mafanikio makubwa kwa maendeleo ya nchi,” alisema Waitara.

Pia aliwataka viongozi wa dini kuendelea kusimamia sekta ya elimu katika shule za kidini ili kutengeneza wataalamu watakaoweza kujiajiri wenyewe.

“Taasisi za kidini zote zimewekeza katika sekta ya elimu na kupelekea kuwepo kwa wataalamu wa kutosha, mfano vyuo vikuu 27 vilivyopo nchini vinamilikiwa na taasisi za kidini, huku vyuo vya kati vikiwa 15, hapo bado shule za msingi na sekondari.

“Hivyo Serikali inaomba muendelee kusimamia sekta ya elimu katika shule zenu kwa kujenga uadilifu kwa jamii ya ki-Tanzania ili wawe na hofu ya Mungu,” alibainisha.

Aliwataka viongozi kuhimiza uadilifu na uaminifu kwa waumini wao ili kuepuka vitendo vya kihalifu kama rushwa, uvivu na ufisadi.

MUFTI WA TANZANIA

Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir alisema makusudio makubwa ya kongamano hilo ni kuzungumzia kuhusu amani, uzalendo na uchumi wa viwanda.

“Kongamano hili lililoshirikisha wadau mbalimbali hata wa mikoani, makusudio makubwa ni kutaka kuzungumza kuhusu uchumi wa viwanda, ni juu ya kumpa nguvu rais na Watanzania kuwa ni jinsi gani tunaweza kufikia uchumi wa kati.

“Pia uzalendo tunazungumziwa, kwani pasipokuwa na uzalendo nchi itadidimia. Kwa sababu nchi ni ya kwetu sisi, ni wajibu wa kila Mtanzania kusimamia na kuimarisha uzalendo,” alisema.

Mufti alisema sehemu kubwa ya uzalendo ni kupiga kura ili kuchagua viongozi wanaofaa, kwa hivyo akawataka Watanzania kutengeneza Tanzania wanayoitaka kwa kupiga kura.

ASKOFU MKUU ANGLIKANA

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Jimbo la Dar es Salaam, Jacsona Sosthenes, aliwataka viongozi wa Serikali na kidini wawe mstari wa mbele kuonyesha njia kwa jamii kwani wao ni nguzo.

“Watanzania tupende kufanya kazi kwa bidii kwani umasikini uliopo sio wa rasilimali bali ni wa utendaji, kwahiyo kazi ikifanyika vizuri tutafikia uchumi wa viwanda kama alivyotaka Rais wetu.

“Pia nawaasa viongozi wasionyeshe tu njia bali na wao wafuate hizo njia ili kuishi kwa vitendo, viongozi wawe mstari wa mbele kuwashawishi watu wafuate matendo yao mema na yenye kufundisha na pia viongozi wa dini wawaelimishe waumini wao kuhusu uchumi wa viwanda,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here