23.9 C
Dar es Salaam
Monday, September 20, 2021

Makonda awaita waliokimbia corona Dar

 MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewaitaka watu waliokimbia mkoa huo kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa corona kurudi ili kuendelea na shughuli zao kama kama kawaida.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Makoanda alisema watu wote waliofunga hoteli, migahawa na sehemu za biashara kutokana na hofu ya corona wanapaswa kuzifungua na kuanza kazi kama kawaida.

“Pamoja na kufungua maeneo yote, wahakikishe wanachukua tahadhari kwa kufuata maelekezo ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

“Nawaomba warudi na kuendelea na majukumu yao kama kawaida,tumshukuru mungu kwa tunu hii,”alisema.

Kutokana na hali hiyo, Makonda ametangaza Jumapili ya wiki hii,itakuwa siku ya sherehe na shukrani kwa Mungu kwa kuwakinga Watanzania na janga la corona.

“Nitafuraji kuona kila mmoja anasherekea siku hiyo. Rais Dk. John Magufuli ametupa siku tatu za kumshukuru Mungu wetu, naamini kila mmoja atafanya ibada ya shukrani, mimi nimeomba Jumapili kila mtu apige shangwe na vigelegele ikiwa ni ishara ya shukrani kwa Mungu wetu kwa makuu aliyotutendea.

“Mtakumbuka historia ya wana wa Israel walichofanya kwenye ukuta wa Yerico…kama wewe una muziki wako nyumbani piga kelele uwezavyo na tarehe 25, tunaendelea kuchapa kazi kama kawaida,”alisema.

Uamuzi wa Makonda, umekuja siku tatu baada ya Rais Magufuli kusema endapo hali ya ugonjwa wa corona itaendelea kama ilivyo sasa, Serikali itafikiria kufungua vyuo ili wanafunzi warudi kuendelea na masomo na pia michezo itaruhusiwa kuendelea kufanyika nchini.

Kauli hiyo aliitoa Jumapili wilayani Chato mkoani Geita wakati wa ibada iliyofanyika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Chato iliyoongozwa na Mchungaji Thomas Kangeizi.

Rais Magufuli alisema hakutoa amri ya kuwafungia ndani wananchi (lockdown) wala kufunga mipaka kwa sababu ingeleta madhara makubwa katika shughuli za uzalishaji mali, utekelezaji wa miradi, ajira za watu na pia upatikanaji wa mahitaji muhimu ikiwemo chakula hali ambayo ingesababisha madhara makubwa zaidi.

Alitoa takwimu za mpaka kufikia siku hiyo, Hospitali ya Amana, Dar es Salaam iliyokuwa na wagonjwa 198 imebakiwa na wagonjwa 12, Hospitali ya Mloganzila iliyokuwa na wagonjwa 30 imebakiwa na wagonjwa 6, kituo cha Lulanzi (Kibaha) kulikuwa na wagonjwa zaidi ya 50 wamebaki 22, Agha Khan wamebaki wagonjwa 31.

“Hindu Mandal 16, Regency wamebaki 17, TMJ 7, Rabinisia 14, Moshono (Arusha) 11, Longido 0, Karatu 0, Buswelu 2, Misungwi 2, Ukerewe 0, Magu 0, Mkuyuni 0, Nyahunge 0, Sengerema 0, Kwimba 0, Bugando na Sekou Toure 2, Dodoma 2 (kutoka zaidi ya 40), Kongwa 0, Kondoa 0 nakadhalika. Na kwamba wagonjwa wengi wana hali nzuri.

“Mimi namwamini Mungu na Mungu amejibu maombi yetu, tumshukuru mwenyezi Mungu kwa kutusikiliza na tuendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu wa corona,” alisisitiza Rais Magufuli.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
156,961FollowersFollow
518,000SubscribersSubscribe

Latest Articles