30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, August 9, 2022

Makonda ataka wanaishio mabondeni kuhama wenyewe

WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amewataka wananchi wanaoishi maeneo ya mabondeni kuhama kwa hiyari yao kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kujitokeza.

Akizungumza wakati wa ziara aliyoifanya kutembelea maeneo yaliyokubwa na mafuriko jana, Makonda alisema kwa mujibu wa taarifa ya utabiri wa hali ya hewa, mvua zitaendelea kunyesha hivyo ni vyema kuchukua tahadhari mapema katika maeneo yao.

 “Nitoe tahadhari kwa wanaoishi katika maeneo hatarishi kuondoka wenyewe katika maeneo hatarishi kwa kuwa mvua ndio kwanza zimeanza kwa mujibu wa utabiri wa hali ya hewa,” alisema Makonda.

Alisema Serikali ya si ya kidikteta hivyo haitawaondoa kwa kutumia ubabe bali itaendelea kuwasihi kufanya hivyo ili wabaki salama na mali zao.

“Mwaka 2012 watu walipatiwa viwanja Mabwepande ili wahame mabondeni na wengine wakajitolea kuwajengea nyumba lakini waliuza na kurudi mabondeni.

“Jana(juzi) tumefanya kazi kubwa ya kuwasiliana na Mungu aachie nafasi jua liwake hivyo tutumie nafasi hiyo kwa kutafuta makazi salama na kuondoka mabondeni,” alisema Makonda.

Makonda aliwataka pia kufuata taratibu za ujenzi wa makazi kama sheria ya mipango miji inavyoelekeza.

“Tunaadhibiwa kwa kutokufuata taratibu za usafi wa mazingira na ujenzi hasa kujenga bondeni, kujaza vifusi bila kufuata taratibu husika na kusababisha wananchi wengine kukumbwa na mafuriko,” alisema Makonda.

Aliwashauri wakazi wa jiji hilo kuacha tabia ya kuchota maji ya mito kwa matumizi ya nyumbani jambo ambalo linaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko.

Meya wa Ilala, Omary Kumbilamoto, akisaidia kutoa maji kwenye nyumba zilizopo mtaa wa Miembeni Vingunguti yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha juzi.

“Kuna watu wanatumia mvua hizo kuachilia maji ya chooni kwenda mitoni na baadhi ya wakazi kuchota maji ya mtoni kwa matumizi ya nyumbani, hatuna shida ya maji hivyo kwa Jiji la Dar es Salaam tuna zaidi ya lita milioni 504 ambayo ni salama hivyo tusijitafutie magonjwa ya mlipuko,” alisema Makonda.

Alisema Serikali inaendelea na ukarabati wa kurejesha miundombinu yote ya umma iliyoharibiwa na mafuriko hasa katika maeneo ya Jangwani na Sinza.

“Kuanzia leo(jana) saa tisa mchana tunatajia kufungua njia zilizokuwa zimefungwa kwa kushirikiana na Tanroads (Wakala wa Barabara) mkoa ambao wapo kazini kuhakikisha njia hizo zinapitika,” alisema Makonda.

Hata hivyo Makonda alisema mpaka sasa wanakusanya taarifa kamili juu ya athari zilizojitokeza.

Kwa upande wao wakazi wa Sinza wamemlalamikia mkandarasi anayejenga Daraja la mto Ng’ombe linalounganisha Sinza na Manzese maarufu kama daraja la Salma Kikwete kwa kushindwa kuwasikiliza walipomtahadharisha kuhusiana na kujenga daraja dogo la muda ambalo halikuwa na uwezo wa kupitisha maji mvua zinaponyesha.

Mmoja wa wakazi hao ambaye ni mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Sinza E, John Buleta, alisema baada ya mkandarasi huyo kuweka makaravati na kuuchepusha mto walimfuata na kumwonya juu ya mafuriko ambayo yangeweza kutokea.

“Alikuwa jeuri na kukaidi akisema wamefanya upembuzi yakinifu katika mto huo, tulimwomba afunge njia hiyo na watumie njia nyingine mbadala ili waendelee na ujenzi lakini hakukubali,” alisema Buleta.

Alisema hata mvua ilipoanza kunyesha walimwomba afungulie njia ya kupita kwa kuwa yasingeweza kupita katika makaravati hayo akakaidi.

“Matokeo yake maji yalikosa njia ya kupita na kuingia katika makazi ya watu na kuharibu mali na kuwaacha wakiwa hawana pa kulala,” alisema Buleta.    

Wakati huohuo, zaidi ya nyumba 30 zimekumbwa  na mafuriko katika eneo la Vingunguti na kupewa hifadhi katika nyumba za majirani.

Akizungumza na MTANZANIA Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala, Omary Kumbilamoto, alisema mvua hizo zineleta madhara ya uharibifu wa mali na kuhatatisha usalama wa wananchi wake.

Alisema chanzo cha mafuriko hayo ni kiwanda kimoja cha tambi kilichojengwa maeneo hayo ambacho kimezuia maji kupita kwa urahisi.

“Awali hakukuwa na shida ya mafuriko katika eneo hili lakini baada ya kujengwa kiwanda miundombinu imezuiwa na kusababisha mafuriko,”alisema Kumbilamoto.

Alisema tayari ametoa taarifa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kutafuta suluhu ya jambo hilo.

” Hawa ndugu zetu wamehifadhiwa kwa majirani lakini wengi Simu, magodoro, makochi na vyakula vimeharibika kabisa kwakuwa maji yalikuwa yanafika hadi magotini,”alisema Kumbilamoto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,291FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles