29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Makonda anusurika kupigwa mawe Dar

NA WAANDISHI WETU
MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda na maofisa wa Jeshi la Polisi jana walijikuta katika wakati mgumu baada ya kunusurika kupigwa mawe na vijana waliokuwa wamejazana katika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo jijini Dar es Salaam.
Makonda na maofisa hao, walifika eneo hilo kwa nia ya kuwaomba madereva wa mabasi yaendayo mikoani kusitisha mgomo waliouanza juzi.
Maofisa wa polisi walionusurika kupigwa mawe ni Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura.
Tukio hilo lilitokea kituoni hapo saa 4:00 asubuhi, wakati Makonda alipokwenda kuzungumza na viongozi wa Chama cha Madereva kuhusu namna ya kumaliza mgomo uliodumu tangu juzi.
Makonda alipofika kituoni hapo, alikwenda moja kwa moja kufanya mazungumzo na uongozi wa madereva, huku akilindwa na askari polisi na wengine waliovaa kiraia.
Wakati mazungumzo yanaendelea, askari wengine walifika katika eneo hilo wakiwa na mbwa kwa ajili ya kuimarisha ulinzi.
Askari walianza kutumia mbwa kuwatishia madereva pamoja na umati mkubwa wa watu uliotaka kusikiliza kilichokuwa kikizungumzwa na baadaye mbwa alimrukia kijana mmoja na kumjeruhi mkono wa kulia.
Tukio hilo liliamsha hasira kwa baadhi ya madereva ambapo walianza kuzomea na kurusha mawe mfululizo katika eneo ambalo Makonda alisimama pamoja na maofisa wa polisi.
Hali hiyo iliwafanya viongozi wa polisi, wakiwamo Kamanda Mpinga, Wambura na wengine kujikusanya na kumkinga Makonda kwa kutumia mikono.
Kisha walifanikiwa kumweka chini Makonda ili mawe yaliyokuwa yakirushwa ovyo yasimfikie.
Watu wengine wakiwamo waandishi wa habari, walilazimika kukimbilia maeneo mengine ili kujinusuru na adha hiyo.
Vurugu hizo ziliwalazimu askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kufyatua mabomu ya machozi na risasi za moto hewani ili kutawanya kundi kubwa la vijana.
“Hapa tumekuja kutafuta suluhu, wao wanatuletea mbwa na mabomu yao ya nini? Waandishi wa habari mnajionea wenyewe polisi ndio wanaoanzisha vurugu, si madereva,” alilalamika mmoja wa madereva hao.
Baada ya dakika kadhaa, Makonda aliendelea na mazungumzo na viongozi wa madereva hao.
Katika hali ya kushangaza, Makonda alisema anaunga mkono mgomo huo kwa sababu ni haki ya raia kudai haki yao.
“Mimi naunga mkono mgomo huu, kwa sababu ni haki ya kila raia na huu ndiyo msingi wa kupata haki yako kwa mtendaji asiyefanya kazi yake sawa sawa.
“Njia hii inasaidia kuwakumbusha viongozi kufikiri zaidi kwa niaba ya wale wanaowatumikia ili kutatua matatizo yaliyopo,” alisema Makonda huku akishangiliwa.
Baada ya Makonda kuzungumza hayo, Katibu wa madereva hao, Rashid Salehe, alisema lengo lao ni kutaka makubaliano yao na Serikali yawekwe kwenye maandishi.
“Si lengo letu kugoma kila mara, tunataka makubaliano tunayofikia yawekwe kwenye maandishi si kama vile alivyofanya Kabaka (Waziri wa Kazi na Ajira) ili tukiona hayajatekelezwa tudai kwenda mahakamani,” alisema Salehe.
Baada ya kauli hiyo, Makonda alikubaliana na sharti hilo, hivyo alikwenda hadi katika ofisi za madereva hao kituoni hapo ili kuyaweka makubaliano hayo kwenye maandishi.

MBOWE AWASILI
Wakati mchakato huo ukiendelea, ilipofika saa 4:49 msafara wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe uliwasili kituoni hapo.
Mbowe aliwasili akiwa ameongozana na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa, Patrobas Katambi, Diwani wa Ubungo, Boniface Jacob na makada wengine.
Idadi kubwa ya madereva na umati mkubwa wa vijana waliukimbilia msafara huo, na kuanza kushangilia huku wakionyesha alama ya vidole viwili hewani.
“Rais, Rais, Rais… tumeichoka CCM, tumeichoka CCM, tumeichoka CCM,” walisikika wakiimba vijana hao.
Mbowe aliteremka kwenye gari na kwenda moja kwa moja katika ofisi ya chama cha madereva kituoni hapo na kuungana na Makonda na maofisa wa polisi ili kupata suluhu.
Ilipofika saa 6:20 mchana kikao hicho kilimalizika na Makonda alikwenda kuwasomea madereva makubaliano yaliyofikiwa.
Baadaye, Mbowe aliwaambia madereva hao kwamba chama chake kinaunga mkono mgomo huo kwa kuwa hakuna njia nyingine ya kuishinikiza Serikali isiyo sikivu kusikiliza madai yao.
Aliwataka madereva kufuatilia ahadi za Makonda na kama hazitatekelezwa aliwashauri warejee tena kwenye mgomo.
“Nimekuja kwa sababu si tu ya usumbufu na mateso waliyoyapata wananchi waliokuwa wanataka kusafiri, nimeguswa na suala lenu, hata wanasiasa wana haki ya kuhamasisha usalama wa abiria na haki zao,” alisema Mbowe.
Aliwataka madereva kuwasafirisha abiria kwa usalama na utulivu wakati Serikali ikiendelea kushughulikia madai yao ambayo Makonda alisaini kwa ajili ya kuyapatia ufumbuzi.
Mapema wakati Makonda na msafara wake wanaingia kituoni hapo, madereva walikuwa wakiimba kwa pamoja “Mohammed Mpinga akasome, akasome,”.

MAKONDA AIGEUKA SERIKALI
Akiongea na madereva hao, Makonda alisema: “Tumeambiwa kwamba kuna tume imeundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, haiwezekani tume ikaundwa hewani, lazima tujue mambo matatu kuhusu tume hiyo.
“Lazima tuwajue viongozi waliomo ndani ya tume hii, muda ambao watafanya kazi yao na hadidu za rejea ambazo watazitumia.
“Lakini wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Ingawaje mnadai haki yenu nawasihi leo wapelekeni abiria hawa makwao, halafu kesho saa 4 nitaongozana na viongozi wenu kwenda kwa Waziri Mkuu tukajue mambo haya matatu kuhusu tume hiyo.”
Alisema iwapo watayaona majina ya wajumbe wa tume hiyo na kukosa imani nao, ataomba waongeze viongozi wawili wa madereva ambao wanawaamini.
“Iwapo leo hatutapata jibu katika madai yenu, nawaahidi nitakuja hapa na kuendelea na mgomo pamoja nanyi kwa muda wa siku saba hadi tupate mwafaka,” alisema.

DK.MAKONGORO
Hata hivyo, wakati mkuu huyo wa wilaya akizungumza hayo, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga aliwasili kituoni hapo kimyakimya.
Taarifa zilipowafikia maofisa wa polisi, walitoa taarifa kwa Makonda ambapo walishauriana na kubaini endapo Dk. Makongoro angejitokeza katika eneo hilo angechafua hali ya hewa, hivyo akaelezwa asifike eneo hilo.

KATIBU WA MADEREVA
Akizungumza katika mkutano huo, katibu wa madereva hao, Salehe alisema wanataka mikataba bora na si bora mikataba kutoka kwa waajiri wao.
“Dereva apatiwe mkataba ili Serikali nayo ipate kodi kutoka kwao, lakini leo hii sisi tumefikia hatua ya kununuliwa vyakula na abiria tukiwa safarini hii ni aibu,” alisema.
Alisema jambo jingine wanataka waajiri wawaidhinishie matibabu yao (bima ya afya).
“Wanasema tunasababisha ajali, ukweli madereva tunaweza kudhibiti ajali hizi kama askari watashirikiana nasi vizuri.
“Kumekuwapo na faini za makusudi kwa madereva wa daladala na teksi, tunaomba kijengwe kituo kimoja cha ukaguzi angalau ili kuondokana na faini hizi za ajabu ajabu barabarani,” alisema.
Kuhusu madereva kurudi shule kila baada ya miaka mitatu, Salehe alisema sheria za barabarani wanazifahamu na hawaoni mantiki ya kwenda tena darasani kusoma mambo yaleyale.

HALI TETE
Katika hali isiyotarajiwa, bei za vyakula katika kituo cha Ubungo zilipanda mara mbili ya ile ya kawaida.
Kwa mfano, chapati moja iliuzwa Sh 1,000 badala ya Sh 500, kikombe cha chai ambacho awali kiliuzwa Sh 500, jana kiliuzwa Sh 1,000.
Sahani moja ya ugali na nyama ilipanda kutoka Sh 2,000 hadi Sh 3,000 huku sahani ya chips kavu iliuzwa Sh 2,000 badala ya Sh 1,500.
“Mimi nina watoto wanne naelekea Musoma, juzi nimetumia Sh 20,000 kutoka Chanika hadi hapa kituoni… hadi sasa nimekwishatumia zaidi ya Sh 70,000. Vyakula viko juu kiasi kwamba nalazimika kujinyima, nashindia maandazi,” alisema mama aliyejitambulisha kwa jina moja la Pendo.

VYOO
Hali ya afya za abiria na wafanyakazi wengine hadi jana zilikuwa hatarini kutokana na vyoo vilivyopo katika kituo hicho kujaa.
Vyoo karibu vyote, licha ya kuwa ni vya kulipia vilionekana ni vichafu kupindukia, huku vikitiririsha maji machafu sehemu zisizostahili.

MAGARI YAONDOLEWA
Awali baadhi ya mabasi yalioondoka kituoni hapo chini ya ulinzi mkali wa polisi, yakiwamo mabasi ya Kampuni ya Dar Express yanayofanya safari zake kati ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Arusha.
Mengine ni mabasi mawili ya Kampuni ya Mohamed Trans ambayo yalikuwa yanakwenda Musoma na Bukoba.

CHAMA CHA KUTETEA ABIRIA
Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria, Gervas Rutaguzinda, alisema hatua ya polisi si ya haki kwani haikuwa busara kusafirisha abiria wa sehemu moja na kuacha wengine.
Mabasi yote ya mikoani jana mchana yalianza safari zao kama kawaida licha ya usumbufu mkubwa tangu mgomo ulipoanza juzi.
TEMEKE

Katika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salam, polisi walilazimika kufyatua mabomu ya machozi kuwatawanya watu waliokuwa wanataka kufanya vurugu kwa lengo la kuzuia magari yasifanye safari zake.
Mabomu hayo yalifyatuliwa asubuhi katika eneo la Mbagala ambako baadhi ya watu walikuwa wakirusha mawe ovyo.
Hali ya usafiri katika eneo hilo ilikuwa mbaya kutokana na wananchi waliokuwa wakisafiri kutozwa fedha nyingi.
Katika eneo la Tandika hali ya usafiri ilikuwa ngumu, magari machache yalionekana yakishusha abiria na kusisitiza hayafanyi tena safari.
Katika eneo la Mtoni kwa Azizi Ally, baadhi ya watu walikuwa wakirusha mawe kwa magari yaliyokuwa yamepakia abiria na kusababisha baadhi kupita barabara za ndani ili kukwepa adha hiyo.
MTANZANIA lilishuhudia daladala lenye namba za usajili T 693 BYK aina ya Toyota Coaster likiwa limepakia wanafunzi wa Shule ya Sekondari Jitegemee, huku wengi wakiwa ni wale wa kidato cha sita ambao wanafanya mitihani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kihenya Kihenya, alisema waliwakamata watu kadhaa wakihusishwa na vurugu hizo.

KILIMANJARO
Mkoani Kilimanjaro mgomo huo uliingia siku ya pili, huku wananchi wakiendelea kutaabika.
Wengi waliamua kutumia usafiri wa pikipiki na kulazimika kulipa gharama kubwa.
Idadi kubwa ya wafanyakazi pamoja na wanafunzi walilazimika kuamka alfajiri ili kuwahi mabasi ya abiria yaliyoonekana kutoa huduma kabla ya kuanza tena mgomo huo saa 12 asubuhi.
Kituo kikuu cha mabasi mjini Moshi na vituo vingine hakukuwapo na mabasi, badala yake pikipiki, bajaji na magari madogo yalifanya kazi ya kubeba abiria.

ARUSHA
Mkoani Arusha, mabasi ya abiria pamoja na yale yanayotoa huduma ya usafiri katika maeneo ya pembezoni mwa Jiji la Arusha jana yalianza kufanya safari zake kama kawaida baada ya mgomo.
Mabasi ya Kampuni ya Kilimanjaro Express yanayofanya safari zake kati ya Arusha na Dar es Salaam juzi yalishiriki mgomo huo hadi saa nne asubuhi, lakini jana yalisitisha.

MBEYA
Habari kutoka mkoani Mbeya zinasema, mabasi ya abiria yaendayo nje ya mkoa huo yalianza safari zake saa 6 mchana, huku magari madogo ya daladala nayo yakirejea kutoa huduma.
Mgomo huo uliodumu kwa saa 18, kuanzia juzi hadi jana, umeathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi kutokana na shughuli kadhaa kusimama na kutokukamilika kwa wakati kutokana na ukosefu wa usafiri.

Habari hii imeandikwa na Veronica Romwald, Mauli Muyenjwa, Faraja Masinde, Nora Damian (Dar es Salaam), Janeti Mush (Arusha), Upendo Mosha (Kilimanjaro) na Pendo Fundisha (Mbeya)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles