23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAKONDA AKAMIWA: MBUNGE CCM ATAKA ACHUNGUZWE MALI ZAKE, WEMA AKWAMA

Na MAREGESI PAUL-DODOMA

VITA iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ya kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya, sasa inaonekana kuanza kumgeukia kwa kukamiwa na baadhi ya wabunge.

Wabunge kadhaa kwa siku ya jana na juzi wameonekana kuanza mapambano na Makonda kuhusu vita yake ya kutokomeza biashara ya dawa za kulevya, huku wengine wakihoji uadilifu wa kiongozi huyo juu ya mali anazomiliki.

Jana, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM), alidai kuwa Makonda anamiliki mali nyingi zisizoendana na muda aliokaa kwenye utumishi wa umma.

Kutokana na hali hiyo, alisema yuko tayari kushirikiana na vyombo vya dola kumchunguza ili uhalali wa mali zake uweze kujulikana.

Msukuma aliyasema hayo bungeni wakati alipokuwa akiomba mwongozo kwa Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson.

“Mheshimiwa Naibu Spika, RC wa Dar es Salaam mwaka 2015 alikuwa akiishi kwa Membe, lakini tangu awe RC kwa mwaka mmoja sasa, anatumia Lexus ya petroli yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 400.

“Lakini kama hiyo haitoshi, amekarabati ofisi yake ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 400 bila kufuata utaratibu wa manunuzi ya Serikali.

“RC wa Dar es Salaam anamiliki ma-V8 na Mwanza amejenga maghorofa ndani ya mwaka mmoja. Je, ni akina nani hao wanaomfadhili kupata mali hizo?

“Hawa mawaziri tulionao humu kwanini mmepigwa ganzi? Waziri wa Utawala Bora, Waziri wa Sheria, mbona mmepigwa ganzi na mnalifanya suala hili liwe ni la rais peke yake?

“Hata kama mali hizo anachangiwa na wafadhili, atutajie wafadhili hao kwa sababu sheria ya maadili inataka anayekufadhili umtaje, sasa ni lini amewataja wafadhili hao?

“Kwa hiyo, naomba mwongozo wako mheshimiwa Naibu Spika kwa sababu kama wengine wanafanya mambo ya ovyo halafu wakawa na kinga na mawaziri wakapigwa ganzi humu ndani na hawawezi kufuatilia, utuelekeze na tunataka RC wa Dar es Salaam achunguzwe mali zake alizonazo na mimi niko tayari kuwasaidia mawaziri na vyombo vya usalama ili tuwaonyeshe ukweli.

“Kama tunataka kumaliza wauza dawa za kulevya, lazima tuanze na mizizi, tusishike matawi, naomba mwongozo wako mheshimiwa Naibu Spika,” alisema Msukuma huku akipigiwa makofi.  

Akitoa mwongozo wake, Naibu Spika alimtaka Msukuma atumie kanuni nyingine ya Bunge kwa kuwa kanuni ya 68 (7) aliyokuwa ametumia, inahusu jambo lililotokea bungeni muda mfupi uliopita.

Msukuma ametoa kauli hizo ukiwa ni mwendelezo wa kumtuhumu Makonda baada ya kufanya hivyo bungeni juzi aliposema anashangaa kuona Taifa linaifanyia kazi taarifa ya mkuu huyo wa mkoa juu ya wauza dawa za kulevya, wakati mawaziri wa zamani wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe na Charles Kitwanga, wamewahi kusema wana orodha ya watu wanaouza dawa za kulevya na hakuna hatua zilizochukuliwa.

“Wauza dawa za kulevya wanajulikana na hata walio mstari wa mbele kukamata wenzao wanashinda nao na kuwasafirisha nchi mbalimbali kama Marekani.

“Kwanini vyombo vya ulinzi na usalama visimchunguze Makonda maana anasafiri sana Ulaya, Ufaransa na Dubai, hivi anasafiri kwa mshahara upi alionao?

“Tunaambiwa juu ya vita ya kupambana na dawa za kulevya halafu tunawakamata akina Ray C na Chidi Benz wakati hao ni wagonjwa.

“Kama Rais Magufuli amesema kama mkewe Mama Janet anahusika na dawa za kulevya akamatwe, kwanini Makonda naye asihojiwe kwa sababu amewapangisha watu nyumba wakati wanajihusisha na dawa za kulevya?” alisema Msukuma.

Juzi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alisema busara inatakiwa kutumika wakati wa kuwachukulia hatua wasanii waliotajwa na Makonda, kwamba wanajihusisha na matumizi ya dawa za kulevya.

Alisema pamoja na kwamba ni rahisi kuwatambua wasanii maarufu wanaojihusisha na dawa hizo, wasanii hao wasichukuliwe hatua kwa kutumia hisia.

Naye Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, akizungumza bungeni juzi alisema kuwa inawezekana Makonda katumwa kwa sababu William Lukuvi na Rais mstaafu jakaya Kikwete waliwahi kusema wana orodha ya wauza dawa, kwa hiyo ifanyiwe kazi.

“Nchini sasa tuna njaa, kwa hiyo, mnachotaka kufanya ni kubadili akili za Watanzania kwa hizi mbwembwe zenu,” alisema Mdee.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), akizungumzia kampeni inayoendeshwa na Makonda, alisema: “Ukiona kifaranga kipo juu ya chungu ujue chini kuna mama yake, leo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametamka kuwa vita ile sio ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam bali ni vita ya wote.

“Vita ya wote kuendeshwa na Mkuu wa Mkoa mmoja ni jambo la kushangaza kidogo, lakini halina ubaya kwani lazima awepo wa kubutua kombolera.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles