33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MAKONDA AJITOA MHANGA DAWA ZA KULEVYA

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amejitoa muhanga katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kutaja majina ya wasanii wakubwa wanaodaiwa kutumia dawa hizo.

Kutokana na hali hiyo amesema kuwa wasanii hao wamekuwa wakitumia mtandao wa polisi tisa ambao amewataja kwa majina na ameagiza wakamatwe.

Akizungumza na waandishi wa habaji jijini Dar es Saalam jana, Makonda alisema yuko tayari kupoteza nafasi yake ya ukuu wa mkoa na hata kutangulia mbele ya haki (kufa), akisimamia utekelezaji wa vita hiyo.

Makonda ni kiongozi wa kwanza kutangaza majina hadharani ya watu wanaotumia pamoja na wale wanadaoiwa kufanya biashara ya dawa za kulevya wakishirikiana na askari polisi.

Hatua hiyo imekuja miaka kadhaa iliyopita baada ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, kuutangazia umma kwamba ana orodha ya wauza dawa za kulevya wakubwa lakini hadi anaondoka madarakani hakuwahi kuwataja majina yao hadharani.

“Najua siku moja Mungu ataniuliza, nilipokupa Mkoa wa Dar es Salaam kupitia Rais wako (anamtaja kwa jina Rais Magufuli),  watoto waliangamia kwa madawa ya kulevya, sitaki kufika mbinguni nisiwe na jibu. Nataka niwe na jibu kwa Mungu wangu kwamba madawa ya kulevya hayakubaliki ndani ya Jiji la Dar es Salaam,” alisema Makonda.

Alisema tayari watu watano waliokamatwa pamoja na vidhibiti wamefikishwa Kituo cha Polisi Kati na wanaendelea kuhojiwa.

Mkuu huyo wa mkoa aliwataja wasanii wanaodaiwa kutumia dawa za kulevya kuwa ni Khalid Mohamed marufu kama TID, Wema Sepetu, Rashidi Makwiro (Chidy Benz) na wengine akiwataja kwa jina moja moja Rachel, Sniper na Tito.

Makonda aliwataja watu wengine aliowanasa kuwa ni Said Masudi Lina ‘ Alteza’,  Nassor Mohamed Nassor, Bakari Mohamed  Khelif na aliyemtaja kwa jina moja la Omary.

“Hakuna aliyetoa ushahidi kama kweli wanatumia ukimuhoji huyu anasema hivi na mwingine anakwambia huyu tunatumia naye..hivyo hawa nao ni vyema nikakutana nao ‘Central’ kesho (leo). Wote hawa nawahitaji na ni vijana wenzangu nafikiri tutaelewana,” alisema Makonda.

Kuhusu askari hao alisema wamekabidhiwa dhamana kubwa ya kuhakikisha dawa za kulevya na usalama wa raia unazidi kuimarika lakini katika operesheni aliyoifanya amebaini kuwa baadhi yao wanahusika katika biashara hiyo.

Aliwataja askari polisi wanaodaiwa kuwa kwenye mtandao wa dawa za kulevya kwa jina moja moja pamoja na vituo vyao kuwa ni Detective Koplo Noel (Kituo cha Polisi Kati), Dotto (Kituo cha Kijitonyama), 'Makomeo' na Swai (Kituo cha Oyster-bay), WP Glory (Kituo cha Kawe), Inspector Fadhili na Steve (Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kinondoni), James (Kinondoni) na Ditective Koplo Willy.

“Polisi wanashindwaje kufahamu kama huyu anafanya biashara hiyo…nimepata tarifa kwamba wanashirikiana na wafanyabiashara wa dawa za kulevya na hatimaye kuifanya kutokuwa rahisi kutokomezwa.

“Na kwa bahati mbaya hata ukienda kwa mwendesha pikipiki anakwambia fulani anafanya biashara. Wanawafahamu hawa wafanyabiashara lakini hawawezi kuwakamata kwa sababu kila Jumamosi huwa wanakwenda kuchukua fedha. Wanawapigia simu kwanza kwamba tunakuja hela yangu ingiza moja kwa moja kwenye simu na wakifika pale wanamkosa mtuhumiwa

“Hizi ni tuhuma na wao wana nafasi ya kujitetea lakini kwa mamlaka niliyonayo kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na kwa taarifa nilizonazo wanastahili kuwekwa ndani na uchunguzi uanze wakiwa hawapo kwenye majukumu yao ili wasije kuharibu ushahidi.

 “…haya mapambano si rahisi lakini kwa sababu tulikula kiapo na Mungu akatupa nafasi ya kuongoza nataka Dar es Salaam suala la madawa ya kulevya liwe historia,” alisema Makonda.

Mkuu huyo wa mkoa pia alizitaja baadhi ya klabu ambazo alidai kuwa zinajihusisha na biashara hiyo ambazo ni Cuba bar, Element ambapo aliwataka wamiliki wake kujisalimisha wenyewe polisi Kituo cha Kati saa 5 asubuhi ya leo.

“Kuna maeneo ambayo watu wamepata leseni lakini wanafanya biashara tofauti na ile waliyoomba leseni na kuna watu wanasema madawa huwa wanapata sehemu hizo,” alisema.

Pia alisema kama Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro na timu yake wakishindwa kutokomeza dawa za kulevya jijini humo watakuwa wamekosa sifa za kuendelea kuwa askari.

WALIOTAJWA WATOA NENO

Mtanzania lilipomhoji Recho alikuwa tayari kuzungumza masuala mengine ya sanaa yake lakini alipotakiwa kueza mapokeo ya wito wa mkuu wa mkoa alikatisha mazungumzo na kumtaka mwandishi awasiliane baadae kwa kuwa alikuwa kwenye gari.

Mtanzania: Unazungumziaje wito wa mkuu wa mkoa kuhusiana na matumizi ya dawa za kulevya?

Recho: “Nipo kwenye usafi ri, nipo njiani sitaweza kuongelea chochote kwa sasa,” alisema Recho.

Wasanii wengine akiwemo Shilole aliliambia Mtanzania kwamba hajui cha kuzungumza kuhusiana na taarifa hizo kwa kuwa zimemstua.

“Sijui niseme nini kuhusu hilo ila inashangaza kumuona mtu akijihusisha na dawa za kulevya wakati kuna watu wengi wameharibikiwa na madawa hayo,” alieleza.

Kwa upande wa msanii Ditto anayetamba na wimbo wa ‘Moyo Sukuma Damu’ alisema amesikia jina likitajwa lakini mkuu wa mkoa alikosea si Ditto bali ni Titto.

“Sijawahi kujihusisha na dawa za kulevya wala sijui chochote kuhusiana na hilo, kutajwa na mkuu wa mkoa Makonda itakuwa amekosea jina langu,” alisema Ditto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles