31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Makonda aja na muswada wa mabadiliko sheria ya mirathi

FAUSTINE MADILISHA (TUDARCo) Na AVELINE KITOMARY

DAR ES SALAAM

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema ofisi yake inatarajia kuwasilisha muswada wa mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya mirathi na sheria ya ndoa kwa Waziri wa Katiba na Sheria.

Makonda alisema hatua hiyo imekuja mara baada ya kufanya kongamano la wanawake wajane 5,181 wa Mkoa wa Dar es Salaam lililokuwa na lengo la kubaini na kutatua changamoto zinazowakabili pindi wanapofiwa na waume zao.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Makonda alisema sheria za mirathi, mila na ile ya watoto haziendani na mahitaji ya sasa, kwani ni za muda mrefu hivyo zinahitaji kufanyiwa marekebisho.

“Mwezi wa nne nilikutana na kina mama wanaotaabika na mirathi na tulitengeneza fomu za kuainisha shida zao, tulipata kero nyingi sana za kisheria na ukosefu wa elimu za kisheria.

“Sheria za kiserikali za mirathi ya mwaka 1865 na sheria ya mirathi ya kimila ni za muda mrefu na haziendani na mabadiliko ya maisha ya sasa na zimekuwa changamoto kwa wajane na wagane wengi,” alisema Makonda.

Alisema mapungufu yalioyoonekana katika vifungu vya sheria ni mwanamke kuhesabika kama sehemu ya mali ya mwanaume, sheria haijabainisha msimamizi na mrithi wa mali pindi mwanaume anapofariki.

“Kifungu cha 114 cha sheria ya ndoa namba 5 ya mwaka 1971 kinamlinda mwanamke pale atakapoachana na mumewe kugawana mali na sio pale mwenzi wake anapofariki bila kuacha wosia.

“Ukiangalia sheria ya sasa ya probate and administration of estate sura 352 kama ilivyopitiwa mwaka 2002, kifungu cha 33 kinaonyesha wazi ni pale tu mwanaume anapofariki ndio mke anapoenda kuomba usimamizi wa mirathi,” alieleza Makonda.

Alisema mapungufu mengine ni yale ya sheria za mirathi za kimila ya mwaka 1963 na sheria ya kiserikali ya mirathi ya mwaka 1865.

“Sheria ya mirathi ya mila inayotamka kuwa mwanamke haruhusiwi kurithi ardhi ya ukoo, inapingana na katiba ya nchi katika ibara ya 13(1)(2) ambayo inatafsiri binadamu wote ni sawa.

“Sheria ya mirathi ya mwaka 1865 iliyorithiwa kutoka India imetamka kuwa mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa haruhusiwi kurithi, sheria hii inapingana na ile ya mtoto ya 2009 katika kifungu cha 10 ambacho kimeweka haki ya mtoto kutokubaguliwa kurithi mali za baba yake,” alieleza Makonda.

MAPENDEKEZO

Makonda alisema pendekezo mojawapo ni mke au mume wawe miongoni mwa wasimamizi wa mali, sheria itoe muda maalumu wa kesi za mirathi kusikilizwa.

“Kutokana na mapungufu yaliyopo, tunapendekeza mabadiliko ya sheria za usimamizi wa mirathi, muda maalumu wa kesi za mirathi, mgawanyo sawa kwa watoto wote wa kike na wa kiume, kuwachukulia hatua wasimamizi wa mirathi wanaotumia vibaya mali za marehemu.

 “Pia tumependekeza kuwa msimamizi wa mirathi awe mume, mke na watoto, tunapendekeza mgane asitolewe ndani ya nyumba kabla mahakama haijaamua,” alibainisha Makonda.

 Hata hivyo alisema kwa sasa kesi za mirathi zimeongezeka kutoka asilimia 17 ya mwaka 1978 hadi 1999 na kufikia asilimia 80.46 mwaka 2000 hadi mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles