24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Makonda aitwa Tabata viwanja vya wazi

PAUL MAKONDA 235

NA HADIA KHAMIS, DAR ES SALAAM

DIWANI wa Kata ya Tabata katika Jimbo la Segerea wilayani Ilala, mkoani Dar es Salaam, Patrick Asenga (Chadema) amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwenda kwenye kata yake ili akamwonyeshe maeneo yote ya wazi yalivyovamiwa ili achukue hatua.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Asenga alisema, viwanja vyote vya wazi viliuzwa na uongozi uliotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kabla ya upinzani kuingia madarakani.

Asenga alitoa wito huo siku chache baada ya Makonda kuwaomba madiwani wa mkoa huo kushirikiana naye katika kuyataja maeneo yote ya wazi katika mkoa huo ili ayarudishe kwenye malengo yake ya kuimarisha michezo kwa watoto na masuala mengine ya kijamii.

Kuhusu kata yake ya Tabata, hahitaji mwezi mzima kutaja maeneo hayo kwa sababu yanajulikana na wananchi wengi wanayafahamu.

Alisema Kata ya Tabata pekee yake ina zaidi ya viwanja 30 ambavyo ni vya meneo ya wazi vimevamiwa na watu ambao wana hati halali, jambo ambalo linazua hofu jinsi watu hao walivyoweza kujipatia hati halali kutoka serikalini.

“Kama kweli Makonda (Mkuu wa Mkoa) anaongea jambo hili kwa dhati kutoka moyoni na si siasa, aje kwenye kata yangu ya Tabata kushuhudia namna viongozi waliopita wanaotoka CCM walivyojimilikisha viwanja katika maeneo ya wazi,” alisema Asenga.

Alisema kuwa tatizo la uvamizi wa maeneo ya wazi ni kubwa kwa sababu watu wamevamia mpaka karibu na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa mwenyewe.

“Ukitoka katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuna Mtaa unaitwa Pangani, pale kuna eneo la wazi lakini limevamiwa na hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa mpaka sasa na nimeshatoa taarifa mbele ya mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, mkurugenzi wa manispaa ya Ilala pamoja na meya, lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa mpaka sasa,” alisema Asenga.

“Hatujui kama ni tamaa za wenyeviti waliopita maana wananchi wengi waliovamia wana hati halali za umiliki wa kiwanja, lakini ukirudi kwenye ramani eneo linaonyesha ni eneo la wazi haliruhusiwi kujengwa kwa ajili ya makazi,” alisema Asenga.

Alisema kuwa kwa maeneo ya wazi ambayo viongozi wa CCM wamejimilikisha watahakikisha wanayachukua na kurejesha serikalini kwa ajili ya kufanyiwa kile kilichokusudiwa.

“Namshauri Makonda kama kweli ameamua kupambana na wanaovamia maeneo ya wazi amshauri Rais ili kuzifuta hati hizo kwa lengo la kukomesha uvamizi wa ardhi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles