25.4 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Makomando sita walivyobadili historia ya Gambia

JOSEPH HIZA NA MTANDAO

JUMAMOSI ya Agosti 13, 2016, walinzi sita kutoka kikosi cha Rais wa Gambia, Yahya Jammeh, walishonana kwenye gari la kukodi wakachoma mafuta kuelekea mji wa pwani wa Serekunda.

Wakaenda kuweka kambi ya muda Senegambia, mji mkuu wa mtaa maarufu kwa matanuzi, ambako muziki husikika daima kutoka baa na watalii wa kizungu huonekana beneti na wapenzi wao vijana wadogo.

Wanaume hao walitulia tuli wakinywa juisi na kutafuna chochote wakati wakisubiri usiku mkubwa uingie ili waingie kazini kuifanya kazi waliyoikusudia.

Hakukuwa na aliyewashtukia pale. Saa saba usiku, wakati walipoona ni wakati mwafaka na salama kusonga mbele kutimiza lengo walilojia, ambalo litabadili historia ya taifa lao. Walipanda gari na kuelekea makao makuu ya chama tawala cha Jammeh, the Alliance for Patriotic Reorientation and Construction (APRC).

Walisimama kwa umbali mdogo kutoka jengo hilo na kuambaa gizani. Jengo lilionekana tupu. Baada ya kulizunguka mara mbili walipaki gari umbali wa mita 300 kutoka lilipo hilo jengo. Kulikuwa na mlinzi mmoja tu katika kibanda kidogo kilicho karibu na lango la kuingilia humo.

Mlinzi akiwa hana hili wala lile alijikuta akikabiliana na mdomo wa bunduki na kisha kuwekwa chini ya ulinzi na kufungwa pingu kabla ya kuwekewa matambara mdomoni asipige kelele na makomando wanne wakawa na jukumu la kuangalia huko na huko kuhakikisha usalama wakati wale wawili wakiingia mjengoni kufanya yao.

Walijua nini walichokuwa wakitafuta humo, lakini walipindua meza na shelfu na kutupa tupa vitu chumbani ili kufanya ziara yao jengoni humo ionekane kana kwamba ni kitendo cha kama kitendo cha uharibifu.

Katika chumba kingine. Walivikusanya pamoja viti na kompyuta katikati ya sakafu huku mafaili, makaratasi na vifaa vingine vya ofisi juu yake. Juu ya lundo hilo, waliweka kile walichokijia: maboksi matatu yaliyohifadhi vitambulisho vya raia waliosajiliwa kupiga kura.

Walinzi hao walikuwa na taarifa za Kiintelijensia kuwa vitambulisho bandia watapatiwa wageni waliolipwa kukipigia kura chama tawala.

Wao badala ya kutumia nguvu kumng’oa rais, walinzi hao waliona kuwa njia nzuri ya kuanzia ni kumzuia asiibe kura. Mmoja wapo alimimina petroli katika lundo hilo na mwingine akachukua kiberiti chake na kuliteketeza moto.

Hiyo, ilikuwa moja ya hatua ndogo kadhaa ambazo ziliwezesha kumpindua kwa mshangao wa dunia mmoja wa madikteta wa ajabu, mwingi wa vioja na vitimbi na aliyedumu muda mrefu zaidi duniani.

Ndivyo ambavyo miaka 22 ya utawala wa Yahya Jammeh ulioonekana hautokoma leo wala kesho ulivyohitimishwa kirahisi namna hiyo. Utawala wake wa kikatili na kinyama ulihitimishwa na upinzani mdogo lakini shupavu chenye mchanganyiko wa waasi.

Wakati wa utawala wake huo wa miongo zaidi ya miwili, Jammeh alilichukulia taifa lake hilo maskini na lililorefuka Magharibi mwa Afrika kama kadola kake binafsi ka kifalme.

Alipenda kuendesha magari kwa kasi katika mitaa na barabara za nchini humo akiwa katika msafara wake, akirusha biskuti na fedha kwa umati uliokuwa kandoni mwa barabara kushangaa msafara wake akiwa juu ya limousine lenye uwazi kwa juu aina ya Hummer – mbwembwe ambazo ziliua na kujeruhi makumi ya raia wake.

Alikuwa ameapa kutawala kwa ‘miaka bilioni’ na kufanya chaguzi kila baada ya miaka michache ili kuupa utawala wake wa kidikteta uhalali, baada ya kuukandamiza upinzani wowote uliojitokeza njiani.

Vikosi vyake vya usalama na siri vilipenya katika kila ngazi ya jamii na wanamgambo wake binafsi, The Jungulars, waliwafanya wakosoji wake, wanahabari na wapinzani wa kisiasa kutoweka kitatanishi.

Utawala huu uliweka wazi utayari wake wa kuzima maandamano ya umma kwa nguvu kubwa. Mwaka 2000, wakati makumi ya wanafunzi kutoka chuo kikuu cha taifa walipoandamana katika mitaa yote ya Banjul kupinga ubakaji wa msichana mwenye umri wa miaka 13 uliofanywa na polisi, majeshi ya Jammeh yaliachia risasi za moto kwa wanafunzi hao wasio na silaha.

Wanafunzi 14 na mwandishi mmoja wa habari waliuawa na operesheni hiyo katili ikatoa ujumbe wa wazi kwa watu wa Gambia: Yeyote atakayeupinga utawala wake ataadhibiwa kikatili.

Wakiwa wameporwa uhuru na fursa zao, vijana wengi wa Gambia walichagua kukabili hatari ya kuvuka Bahari iliyo kaburi la wahamiaji wengi- Mediterranea kuliko kukaa katika taifa la kipolisi, Gambia chini ya Jammeh.

Mwaka 2016, Wagambia 12,000 walijazana katika pwani ya Italia na Ugiriki– kiwango kikubwa kuliko taifa lolote lingine la Afrika kuwahi onekana. Lakini baadhi walibaki nchini humo kupambana humo humo. Hawa ndio walioleta mabadiliko!

Katikati ya mkabilio wa ukandamizaji wa kikatili, mseto usiotarajiwa wa vikundi vidogo vidogo vya waasi ndani na nje ya Gambia uliendesha upinzani na kuelekea uchaguzi ule walikuwa wamegawana majukumu na mojawapo ni kikundi kile cha walinzi wa rais kilichohakikisha kinasambaratisha mpango wowote wa wizi wa kura.

Kundi moja liliandaa waraka wenye kurasa 25 wa namna nzuri ya kumng’oa dikteta, ukiwa pamoja na mambo mengine namna ya kujenga kampeni, ujumbe mfupi wa maneno ulioandaliwa vyema kuwahamasisha waandamanaji na mwongozo wa jinsi ya kuunganisha upinzani.

Waraka huu ndio uliokuwa mwongozo, ambao kupitia vikundi hivyo vidogo vidogo vyenye majukumu tofauti tofauti, vilipenya hadi serikalini na kufanikisha mabadiliko ya utawala.

Baada ya mabadiliko ya sheria za uchaguzi Julai 2015 uliofanya iwe ghali mno kusimama kama mgombea, uchaguzi feki ulipangwa kufanyika Desemba 2016 ukawa msingi wa maandamano ya mitaani.

Dhamira ya kuuvunjilia mbali uking’ang’anizi wa Jammeh katika Gambia ulikuwa bado mbali mno kuufanikisha, lakini hatua ya mwisho ya kumtokomeza ilichukua miezi mitano tu.

Wachache walipoteza maisha yao katika mchakato huo, lakini baadhi walibaki hai kusimulia yaliyojiri katika mkakati huo wa siri uliomtafuna Jammeh ikiwamo kutimiza ile methali ya wahenga ya ‘kikulacho kinguoni mwako.

Wakati Jammeh alipoingia madarakani zaidi ya miongo miwili iliyopita, hakuwa akiwakilisha chama chochote na au itikadi. Akiwa na umri wa miaka 29 tu, alikuwa akisimamia kikosi cha kumlinda rais wa kwanza na wa pekee tangu taifa hilo lipate uhuru wake kutoka Uingereza, Dawda Jawara.

Samba Faal, ambaye alikuwa naibu meya wa mji mkuu wa Banjul, bado anakumbuka wakati wa joto la kiangazi Julai moja ya 1994 wakati alipoona kundi la walinzi wakiongozwa na Jammeh wakichanja mbuga kuelekea Ikulu.

Walichukua fursa ya kutokuwapo kwa rais, aliyekuwa ziarani nje, Jammeh na makomredi wake walitwaa madaraka katika Mapinduzi yasiyo na damu.

Mpango wa Jammeh ulikuja wakati mwafaka. Jawara alishikilia urais tangu mwaka 1970 na Wagambia waliuchoka utawala wake. Rushwa ilikuwa sehemu ya kawaida ya maisha na marafiki wa rais walitajirika mno.

Akimkosoa Jawara na mataifa ya magharibi yaliyomuunga mkono, ikikumbukwa pia alisomea Uingereza, Jammeh alijitangaza kama mtu maskini kutoka vijijini Gambia, mtu wa watu.

Leo hii Wagambia wengi wanamwita punguani, ambaye alikuwa akiharibiwa na kiburi. Lakini miongoni mwa watu waliofanya naye kazi kwa karibu, kuna kundi linaloheshimu uwezo wake.

“Alikuwa mwelewa mwenye mbinu nyingi nzuri, naam hakuwa na uwezo wa kiitikadi au mipango ya namna ya kutawala ikiwamo diplomasia, lakini alichukua madaraka kwa muda mwafaka na alijua namna ya kuyang’ang’ania yasimponyoke.

Muda mfupi baada ya kuidhibiti nchi, Jammeh aliamuru kunyongwa kwa makumi ya maofisa wa ngazi ya juu jeshini, ambao aliwahesabu kuwa wanaweza kuwa tishio kwake. Tambua kipindi cha kwanza cha utawala wa dikteta yeyote ndicho kigumu kisichotabirika.

Kwa mujibu wa Kitabu cha Udikteta, kilichoandikwa na wanasayansi wa siasa, Alastair Smith na Bruce Bueno de Mesquita wa Chuo Kikuu cha New York, nchini Marekani dikteta ana nafasi 50-50 ya kuhimili miezi sita ya kwanza madarakani.

Kwa Jammeh, hakupata tabu yoyote. Kama mwanamieleka wa kulipwa na mchuuzi wa mitaani, ni watu wachache wangekuwa tayari kuweka pesa zao katika mchezo wa kamali kutabiri uwezekano wa kukwea kuelekea uraisini.

Akifahamika kwa wingi wa vioja na vitimbi, aliutangazia ulimwengu kuwa na uwezo wa kutibu maradhi hatari ya VVU/Ukimwi.

Fatou Jatta, ambaye alikumbana na Jammeh kwa mara ya kwanza mwaka 2007, alikuwa mmoja wa Wagambia wa kwanza waliojianika hadharani kuwa na VVU, walioagizwa kwenda katika makazi ya rais mjini Banjul.

Yeye na watu wengine wanane wenye VVU walianza matibabu hayo yaliyofanywa na Rais. Akiwa amevalia kanzu ndefu nyeupe na kwa upole, alimtaka kuvua nguo zake na kulala chali. “Haikuwa masaji nzuri,” Jatta alikumbuka.

“Hakuwa mtaalamu wa masaji. Lakini alikuwa rais.” Kila aliyepelekwa kwa ajili ya masaji na Jammeh alipewa dawa: glasi yenye kimiminika kijani, ambacho alikitengeneza mwenyewe. Kamwe Jatta hakuweza kubaini ni mseto wa aina gani huo. Mara ya kwanza watu walipokunywa, kila mmoja alitapika, lakini wakajifunza kuweza kuudhibiti, chini ya macho makali ya askari waliovalia silaha waliokuwa wakifuatilia kila kinachoendelea kwa chati.

Wagonjwa walirudi katika matibabu yao kila siku asubuhi kwa miezi minane. Matibabu yalikuwa ubunifu wa rais mwenyewe na alitangaza sana mafanikio ya tiba yake katika vyombo vya habari vya kimataifa huku akisisitiza kwamba maelezo ya namna dawa ilivyopatikana na kutengenezwa yanabakia siri kama ilivyo kwa kinywaji cha Coca-Cola.

Wagambia wenye VVU 9,000 walilazimishwa kuacha kwenda vituo vya tiba kwa ajili ya kionjo kilichotengenezwa kienyeji cha Jammeh, kwa mujibu wa taasisi yenye makao makuu Marekani NGO Aids-Free World.

Si tu Jammeh alisisitiza uwezo wa kutibu VVU bali pia alionekana kuamini kuwa na nguvu ya kimungu. Hata hivyo, wengi wa waathirika hawa wa VVU wanataka afunguliwe mashtaka kwa udanganyifu wake na kuhatarisha maisha yao na wengine waliokwishatangulia.

Alifuga simba kama wanyama kipenzi na alizika miili ya maadui wake nyumba ya makazi yake. Pia alikausha uchumi wa nchi.

Haikuwa ngumu kusema mpango wa uchumi wa Jammeh ulishindikana: kamwe hakuonekana kuwa na mpango wowote halisi. Uchumi ulidumaa chini ya utawala wake; baadhi ya wachumi walikadiria kuwa mfumuko wa bei ulikuwa kati ya asilimia 20 na 25 kipindi cha miaka mitano. Gambia haina utajiri wa madini lakini kulikuwa na shughuli muhimu zinazoweza kutumika kutengeneza faida: miundombinu, maji, umeme.

Kuziteka huduma hizi kukawa njia ya utajiri ya Rais Jammeh. Kwa maana hiyo, Jammeh alijilimbikizia utajiri mkubwa na kuuficha nje.

Wizara ya Sheria ya Gambia bado inahaha kurudishwa kwa miliki zaidi ya 130 kote duniani, akaunti za benki 88 na kampuni 14 zilizokuwa zikishirikiana naye. Jammeh alikuwa na magari ya kifahari aina ya Rolls Royces mawili  na limousines kadhaa ikiwamo kipenzi chake Hummer.

Muda mfupi kabla ya kuangushwa, ndege ya mizigo ilisafirisha magari sita ya kifahari ya Jammeh kutoka nchini humo, kwa mujibu wa New York Times.

Kulinganisha na utajiri mkubwa wa rais, karibu nusu ya watu wa Gambia wanaishi chini ya dola 1.25 kwa siku kwa mujibu wa Benki ya Dunia.

Badala ya kufuta chaguzi, aliziendesha kila baada ya miaka mitano, akijiamini kutokana na mbinu zake na alikuwa akishinda si chini ya asilimia 70 ya kura katika kile wapinzani na waangalizi wa kimataifa walichoshuku wizi wa hali ya juu wa kura.

Kutokana na kuwa na wapiga kura wasiozidi 800,000, ilikuwa rahisi kutengeneza ushindi kwa kuchomeka kura bandia kwa kutumia raia wa kigeni waliolipwa kutoka Senegal na Guinea-Bissau.

Iwapo kadi bandia ambazo chama tawala ilipanga kuzisambaza kwa wapiga kura wa kigeni zingeharibiwa, kikundi kile cha watu sita kiliona chama tawala hakingepata muda wa kutengeneza nyingine.

Ndivyo ilivyotokea, ambapo walinzi hao wakatoroka, wakiwa tayari wamezihamisha familia zao nje kabla ya kukamatwa.

Moto uliwashwa, ukashika kasi haraka, wanaume hao wakatumia njia tofauti kutokea jengo hilo wakakimbilia garini mwao na kulikimbia jiji.

Naam, mpango ulienda vyema, moto uliharibu ofisi mbili lakini si jingo zima. Hakuna aliyejeruhiwa na waharibifu hao hawakupatikana.

Vitambulisho vikageuka majivu na ikawa ngumu mno kutengeneza vingine.

Baada ya shambulio hilo, walinzi hao sita walikimbilia kusini mwa mpaka na kukimbia msituni wakiwa pamoja hadi walipovuka kuingia Senegal. Waliweza kufika mjini Dakar, ambako walisubiri kinachotokea.

Hapo walikutana na Wagambia wengine waliokuwa wakifanya kazi kumuangusha Jammeh.

Ukaja uchaguzi wa Desemba Mosi 2016, wakajitokeza zaidi ya nusu milioni sawa na  asilimia 60 ya wapiga kura waliojiandikisha.

Kura zilipohesabiwa ikaonekana majigambo ya Jammeh ya kutawala miaka bilioni ni bure. Waandishi wa habari wa Gambia waliona hilo mapema hawakujua nini cha kuripoti.

Ni nadra kuripoti habari zilizo kinyume na utawala wakiogopa kitakachowapata. Ili kupata majibu wanahabari walikusanyika mbele ya ofisi ya Tume Huru ya Uchaguzi.

Katika ofisi yake, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi,  Alieu Njai (82) alikaa kitini akiwa ameingiwa na gofu, akiwa ameona mambo si mazuri kwa rais, huku karatasi za kurasa tano au sita zikiwa mkononi, mwisho akaenda kutangaza matokeo kama yalivyo.

Licha ya shinikizo kutoka kwa ofisi ya rais asitishe kutangaza matokeo yaliyokuwa yakitoka, mwisho aliuvaa ushupavu akatangaza yalivyo mshindi akiwa Adama Barrow.

“Jammeh alidhani anaweza kuniamini kwa asilimia 100. Lakini nilikuwa na imani sifuri kwake,” Njai alisema. Wakati alipotangaza, waandishi wa habari kutoka televisheni ya taifa walimtaka aache, lakini Njai alipuuza.

Mwishowe Jammeh akalazimika kukata mawasiliano ya intaneti na simu ili kuwafanya Wagambie wasijue matokeo, lakini yalikuwa yamesambaa tayari. Maji yakawa shingoni mwake.

Jammeh akakubali kushinda na kumpongeza mpinzani wake Adama Barrow, lakini wiki mbili baadaye akabadili msimamo akitaka kubaki madarakani kwa madai uchaguzi haukuwa huru na haki. Lakini Mataifa ya Magharibi yakamtisha kumng’oa kijeshi. Salama yake ikawa kukimbilia Guinea ya Ikweta kwa dikteta mwenzake Teodoro Obiang Nguema Mbasogo.

Rais Teodoro ameapa kumlinda Jammeh, akitia pamba masikioni kupuuza miito ya kumtaka amrudishe nchini humo au nchini Ghana akakabili tuhuma zinazomkabili.

Mwisho…..

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles