29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Makomando JWTZ, US. Amry wahitimu mafunzo maalumu

NA WINFRIDA MTOI, Mtanzania Digital


MAFUNZO ya Makomando wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Marekani (U.S.Amry), yamefikia tamati leo Septemba 10, 2021, ambapo Mkuu wa Mafunzo na Utendani Kivita wa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, Brigedia Jenerali Iddi Nkambi amesema lengo ni kukabiliana na vitendo vya uhalifu ikiwamo ugaidi.


Hafla ya kufunga mafunzo hayo imefanyika katika kituo cha mafunzo ya ulinzi na amani, Kunduchi,jijini Dar es Salaam ambapo makomando hao walionesha burudani mbalimbali.


Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, yaliyoanza Julai 28, mwaka huu,Brigedia Jenerali Nkambi, amesema anatarajia mabadiliko ya kiutendaji kwa makomando hao kutokana na kile walichojifunza.


“Haya mafunzo yawe chachu kwenye utendaji wao wa kazi, yawabadilishe na yawapeleke kwenye ufanisi zaidi na yawe ni daraja la kuunganisha Jeshi la Marekani na la kwetu upande wa ‘Special Force,” ameeleza Brigedia Jenerali Nkambi.


Amesema si mara ya kwanza kufanyika mafunzo ya aina hiyo nchini, ni programu yenye zaidi ya miaka saba na dhima kubwa ni kubadilishana uzoefu na ujuzi wa jinsi ya kukabiliana na matishio mbalimbali.


“Matishio sasa hivi yamegeuka, hayana sura ya mwanzo, ule ugomvi wa nchi kwa nchi umepungua na yamekuwa mtambuka zaidi,ndio maana tunabadilishana uzoefu na ujuzi wa kukabiliana na matishio kwa sababu ya sasa hivi huwezi kuyakabili peke yako.


“Sisi tumejifunza na wenyewe wamejifunza, lakini tukiunganisha kwa pamoja tunaweza tukafanikiwa zaidi katika matatizo ya sasa hivi,” amesema.


Kwa upande wake Kamanda wa kikosi cha Makomando, Luteni Kanali Cliff Kulya, amesema washiriki wa mafunzo hayo ni askari na maofisa wa Jeshi la Wananchi ambao wana taaluma maalumu ya komando wanatumiwa na nchi kukabiliana na matishio ambayo hayahitaji nguvu kubwa ya majeshi ya kawaida.


“Huwezi kukabiliana na ugaidi kwa kutumia majeshi makubwa makubwa, unatumia vikundi vidogo kama hivi ambayo vimepewa mafunzo maalum na vinaweza kufanikisha jukumu hilo kwa ufanisi bila kuleta athari kwa wale ambao hawahusiki,” amefafanua Luteni Kanali Kulya.


Sherehe hizo ziliambatana na utoaji zawadi mbalimbali kwa askari wa Jeshi la Marekani kutoka kwa wenyeji wao JWTZ.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles