Na Abducado Emmanuel, Dar es Salaam
SIKU moja baada ya kumalizika kwa fainali za michuano ya Kombe la Dunia nchini Brazil kwa Ujerumani kuchukua ubingwa huo kwa kuifunga Argentina bao 1-0, makocha wa hapa nchini wamefunguka na kueleza kuwa Ujerumani imestahili ubingwa huo.
Bao la Ujerumani kwenye fainali hiyo, limefungwa na Mario Gotze dakika 30 za nyongeza (dakika ya 113) baada ya dakika 90 za muda wa kawaida kwisha kwa sare ya bila kufungana, bao hilo limekata ukata wa miaka 24 wa Ujerumani kutotwaa ubingwa huo tokea mwaka 1990.
Kocha wa timu ya JKT Ruvu, Fred Minziro, alisema michuano ya mwaka huu ilikuwa haina msisimko tuliouzoea miaka ya nyuma, kutokana na timu nyingi kubwa zilizoshiriki kutokuwa na viwango vizuri.
“Ujerumani ilistahili ubingwa lakini michuano haikuwa na msisimko kabisa kama miaka ya nyuma, timu kama Ufaransa, Italia, Brazil na Uholanzi zilikuwa zinaleta changamoto kubwa miaka ya nyuma, lakini sasa hivi hazina timu nzuri na kupelekea kushindwa hata kufika fainali,” alisema Minziro.
Naye kocha wa zamani wa Simba na Mwadui FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, alisema michuano ilikuwa bora, lakini timu nyingi zilizoshiriki zilikuwa na tatizo kwenye nafasi ya ushambuliaji, huku akidai zilikuwa fainali za makipa, kwani walionesha umahiri mkubwa.
“Washambuliaji walikuwa na tatizo na hata kwenye mechi ya fainali Argentina ilitengeneza nafasi nyingi, lakini umaliziaji ulikuwa tatizo, fainali hizo zimebebwa na makipa ambao wameng’ara kwa kiasi kikubwa. Wajerumani walikuwa hawaipi timu yao nafasi kubwa ya kuchukua kombe, lakini walianza kuipa nafasi mara baada ya kuwafunga wenyeji Brazil mabao 7-1 kwenye nusu fainali,” alisema Julio.
Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’, Hemed Morocco, aliitaka Tanzania kuiga mfano wa Ujerumani kwenye kuunda timu, kwani walitumia miaka minne kuitengeneza timu hiyo hadi kutwaa ubingwa huo juzi.
“Ujerumani walistahili ubingwa na sisi tunatakiwa kuiga mfano wao, kwani kikosi chao kimesheheni wachezaji wengi waliokuwa pamoja miaka minne iliyopita, hapa nchini tumekuwa na kasumba ya kutaka mafanikio ya haraka, hii si njia bora, cha msingi ni kutengeneza kikosi cha muda mrefu,” alisema Morocco.