27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MAKINIKIA YAIVURUGA ACACIA

Na Mwandishi wetu – Dar es Salaam


MZOZO wa Kampuni za uchimbaji madini za Acacia na Barrick na serikali, ambayo kiini chake ni udanganyifu unaofanywa na kampuni hizo kwenye mchanga wa dhahabu (makinikia) unaosafirishwa nje ya nchi, umeivuruga kimataifa kampuni ya Acacia, imefahamika.

Taarifa zinaonyesha hisa za kampuni hiyo katika Soko la Hisa la London, Uingereza, zimeporomoka waka asilimia zaidi ya 40, jambo ambalo halijapata kutokea katika   miaka mitano iliyopita.

Hisa hizo zilianza kuporomoka tangu Machi serikali  ya Tanzania ilivyopiga marufuku usafirishaji wa makinikia nje ya nchi.

Juzi, baada ya kampuni hiyo kuweka wazi deni la dola za Marekani bilioni 190 (Sh trilioni 424), ambalo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezitaka kampuni dada zake (Bulyanhulu Gold Mine ya mgodi wa Bulyanhulu  na Pangea Minerals (PML) ya mgodi wa Buzwagi) zililipe, hisa za Acacia na Barrick ziliporomoka zaidi.

Wakati hisa hizo zikiporomoka, vyombo vya habari vya kimataifa vikiwamo CNN ya Marekani  na BBC ya Uingereza, vimekuwa vikitumia muda mwingi kujadili kodi hiyo ambayo baadhi vinadai ni sawa na mapato ya karne mbili ya kampuni hizo.

Wakati Acacia ikilalamikia kodi hizo, Wizara ya Fedha na Mipango, ilisema madai hayo ya kodi yamepelekwa kwa Kampuni za Bulyanhulu Gold Mine (BGML)   na Pangea Minerals (PML)  na siyo Acacia.

Hata hivyo Acacia ndiyo kampuni dada ya kampuni mbili hizo huku Barick ikiwa ni mbia mkubwa mwenye  asilimia 64 ya hisa.

Juzi, baada ya Acacia kuweka hadharani madai hayo ya kodi hizo,  kampuni hiyo yenye makao yake makuu Uingereza,   thamani yake katika Soko la Hisa la London iliripotiwa kushukwa kwa asilimia 42, anguko ambalo halijawahi kuripotiwa tangu mwaka 2013.

Nayo Barrick yenye makao yake makuu Canada, hisa zake katika Soko la Hisa Toronto (TSX), zimeshuka kwa asilimia tano.

Msimamo wa Rais Magufuli

Mara kadhaa tangu kamati mbili za Rais zitoe taarifa zake kuhusu kiwango cha madini  kwenye makontena 277 ya mchanga wa dhahabu yaliyozuiliwa kwenye banadari ya Dar es Salaam, Rais Magufuli amekuwa akitoa kauli zinazoenyesha kutoridhishwa kwake na sekta ya madini nchini.

Julai 21 akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mkoani Kigoma, Rais Magufuli alisema: “Nitasimamia haki siku zote katika maisha yangu.

“Niliwaambia nimeanzisha vita hii ya uchumi, vita ya  uchumi ni mbaya sana, wakubwa wale huwa hawafurahi, kuna viongozi wengi tu mliona yaliyowapata ni kwa sababu nchi zao zilikuwa na mali.

“Lakini wale wakubwa wakataka kuchezea hizo mali kwa manufaa yao na siyo kwa manufaa ya wananchi wa pale. Walitumia mbinu nyingi za kila aina lakini Mungu wangu ni mwema na Watanzania ni wema watasimama kwa ajili ya taifa hili.

“Ninayoongea nayajua ni matrilioni ya fedha ambayo yameibwa, na kwa sasa   tumewaita waje wafanye mazungumzo, wamekubali lakini wakichelewachelewa  nitafunga migodi yote.

“Ni mara 10 migodi hii tukaigawana Watanzania wachimbe wawe wanauza, tuwe tunapata kodi kuliko kuchimbwa na watu wanaojiita wawekezaji halafu hawalipi kodi. Walikuwa wanazungumza mle wanachimba dhahabu, madini machache tu, matatu…tumegundua mle kuna madini mengi.

“Tanzania hii ni nchi tajiri, lakini imekuwa ikiibiwa mno, tumechezewa sana, mimi nipo serikalini na mimi ndiye najua siri za serikalini.

“Tumechezewa sana kwa kuibiwa sana mali zetu, kwenye dhahabu huku tumeibiwa mno, ukiyajua yale yaliyokuwa yanafanyika mle unaweza ukalia.

“Unaweka ukatamani kwamba usiishi… mtu anachimba, anapokea, anapeleka na anashirikiana na baadhi ya watu tuliowaamini kwenda kulisimamia hili.

“Anasema hapa tunasafirisha mchanga na Watanzania wote tunaamini tunasafirisha mchanga, mbona hawajaja Kibondo kuchukua mchanga wa hapa mbona na penyewe tunao?

“Lakini tunaamini, wanaupeleka kwenye makontena wanapeleka Ulaya na wakishaenda kuusafisha kule ule mchanga unaobaki wala hawaurudishi.  Ulikuwa ni utapeli wa ajabu, na ni aibu kubwa kuona utapeli huu unafanywa na watu ambao ni wakubwa”.

Julai 26 akiwa mkoani Singida, Rais Magufuli tena alisema: “Haiingii akili watu wanakuja wanachukua mali zetu na kuondoka nazo, ifike mahali tuamke.

“Tumeibiwa vya kutosha, nendeni mkachimbe madini, hizo fedha tutagawana sisi, hata kama hatufanyi kazi hizo fedha tutagawana.

“Wapo Wachina wanakuja kuchimba barabara hapa nchini, tunashindwaje kuwatumia hawa wakachimbe madini yetu kisha wakatuachia dhahabu yetu halafu wao wakaondoka?

“Mimi ndiye Rais, hakuna anayejua siri za serikali kama mimi na nawaambia mmepata mtu ambaye anazungumza ukweli, ningeweza kunyamaza kwa vingine ninavyoviona, lakini nataka kujenga Tanzania mpya.

“Yale makontena yote ningeweza kuwaambia tugawane mzee, hata kingereza ninajua, ningeweza kuwaambia give me same ten percent.

“Ningejenga mahoteli na kuwa na kampuni nyingi kwa sababu wapo watanzania wamejenga huko nje lakini nyumba za wazazi wao zimechakaa, mimi nimezaliwa hapa, ninaishi hapa na nitakufa hapa”.

Mwiba wa TRA

Wakati kauli hizo hazijapoa, hivi karibibu TRA nayo   ikaidondoshea  kampuni hizo mzigo wa deni   tangu mwaka 2000 hadi 2017 kutokana  na ukokotoaji uliofanywa na mamlaka hiyo kwa hesabu za ripoti mbili zilizoundwa na Rais.

Katika kodi hizo, Mgodi wa Bulyanhulu unadaiwa dola za Marekani bilioni 154 (Sh trilioni 344.8) na Mgodi wa Pangea dola bilioni 36 (Sh trilioni 76.1).

Dola bilioni 40 (Sh trilioni 89.5 trilioni) ni malimbikizo ya kodi na dola bilioni 15 (Sh trilioni 335.9) ni adhabu na riba.

Kampuni maji ya shingo

Licha ya kushuka kwa hisa za kampuni hiyo, taarifa ya hesabu zake kwa nusu mwaka 2017 iliyotolewa na Mtendaji Mkuu wa Acacia, Brad Gordon, imeonyesha mapato yake yameporomoka kutoka Dola za Marekani milioni 318   (Sh bilioni 709.115) hadi Dola za Marekani  milioni 176 (karibu Sh bilioni 392.46), huku hisa zake zikishuka kwa asilimia 31 ikilinganishwa na Desemba, mwaka jana.

Pia athari nyingine ni kulazimika kuweka viwango vidogo vya malengo yake  ya uzalishaji ambayo ni kati ya wakia 850 hadi 900,000 kwa mwaka huu.

Vilevile,  mzunguko wake wa fedha umeshuka kutoka Sh bilioni 709.11 mpaka Sh bilioni 392.46.

Ripoti ya Profesa Osoro

Akisoma ripoti ya kamati yake, Profesa  Nehemiah Osoro, alisema takwimu zilizokusanywa kutoka  TRA mwaka 1998 hadi Machi 2017, zinaonyesha makadirio ya chini ya makontena yaliyosafirishwa  nje ya nchi ni 44,277   kwa makadirio ya juu yakiwa 61,320.

“Jumla ya thamani ya madini katika makontena 44,077 yaliyosafirishwa nje ya nchi katika mwaka 1998 hadi 2017 kwa kutumia kiwango cha wastani, ni Sh trilioni 132.56 trilioni sawa na dola za bilioni 60.25 au Sh trilioni 229.9 sawa na dola za Marekani bilioni 104.5 kwa kiwango cha juu.

“Thamani ya madini yote katika makontena 61,320

yaliyosafirishwa nje ya nchi katika kipindi kati ya 1998 na 2017, kwa kutumia kiwango cha wastani, ni Sh trilioni 183.597 sawa na dola za Marekani bilioni 83.45, kwa kiwango cha juu ni sawa na  Sh trilioni 380.499 ambazo ni dola za Marekani bilioni 144.77,” alisema Profesa Osoro.

Juni 14, Rais Magufuli alikuwa na mazungumzo Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation, Profesa John Thornton.

Baada  ya mazungumzo hayo, Ikulu ilitoa taarifa iliyosema kwamba kampuni hiyo ilisema  ipo tayari kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania  kulipa fedha ambazo nchi imezipoteza kutokana na kampuni hiyo kuendesha shughuli zake nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles