31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Makinda awafunda wabunge, madiwani wanawake

Allan Vicent -Tabora

SPIKA mstaafu wa Bunge, Anne Makinda amewataka wabunge na madiwani wanawake nchini kujiamini na kuhakikisha wanasimamia kikamilifu rasilimali za umma ili ziwanufaishe wananchi wote.

Alitoa wito huo juzi katika semina ya kuwajengea uwezo kwa viongozi wanawake wa Serikali za Mitaa (Wasemi), iliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), jijini Mwanza.

Makinda alisema mchango wa wabunge na madiwani wanawake umekuwa hauonekani na kutambuliwa na jamii kutokana na wao wenyewe kuwa na hofu ama kutokujiamini kitu ambacho kimechangia kuwarudisha nyuma.

Alisisitiza kila mmoja wao ana wajibu wa kuonyesha uwezo wake na kuhakikisha unaonekana, hivyo wajitokeze kwa wananchi na wawatumikie kwa uadilifu ili mchango wao utambulike.

“Tatizo letu sisi viongozi wanawake tunajenga hofu na tunaogopa kujitokeza kuwajibika vizuri kwa wananchi eti kwa sababu ni wanawake, hata mimi nilianzia pia viti maalumu, lakini nilipata nafasi ya kwenda jimboni kwa sababu nilijiamini na niliwajibika kikamilifu hadi kufikia hapa,” alisema.

Aliwaasa viongozi hao wa Serikali za Mitaa kuhakikisha wanasimamia ubora wa huduma za jamii katika halmashauri zao na kuhakikisha kila kinachofanyika wanakielewa vizuri na kutoa taarifa kwa wananchi wote.

Aidha aliwashauri kujiendeleza kielimu ili kuweza kuwa na upeo mkubwa zaidi wa kupambanua mambo mbalimbali wanayokutana nayo wakati wakitekeleza majukumu yao na kuwezesha kutoa huduma bora zaidi kwa jamii.

Makinda aliwahimiza viongozi hao kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kupiga kura na kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles