28.8 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

MAKAZI BORA YANAWEZA KUPUNGUZA BAJETI YA AFYA

Na FARAJA MASINDE


TAKWIMU zinaonyesha kuwa kunaongezeko kubwa  kwenye gharama za matibabu duniani kote jambo ambalo linawapelekea wanasayansi kutafuta njia mbadala ya kukabiliana na upatikanaji wa matibu nafuu.

Lengo ni katika kuhakikisha kuwa wanapunguza  matumizi ya tiba kwa mataifa mbalimbali ili rasilimali fedha zinazookolewa ziweze kuelekezwa kutatua masuala mengine muhimu.

Tafiti zinaonyesha kuwa kuna uhusiano mkubwa baina ya upatikanaji wa makazi ya bei nafuu na huduma za afya kwa wananchi, ukiachilia mbali manufaa mengine kama kukuza uchumi na kuokoa gharama za maisha.

Pia uwepo wa makazi bora hupunguza msongo wa mawazo na madhara mengine ya afya yanayoweza kumpata binadamu.

Gharama kubwa za chakula

Ni wazi kuwa nyumba ni moja kati ya rasilimali muhimu ya jamii ambayo huelekeza msimamo wa kiakili, kimwili na maslahi ya familia kwa ujumla.

Hata hivyo bado kuna haja kwa watunga sera kuzingatia njia mbadala zitakazohusisha upatikanaji wa makazi ya bei nafuu ambayo huchangia kwa sehemu kubwa kuboresha afya za wananchi.

Kwa familia ambayo hutumia kiasi kikubwa cha fedha kwenye makazi ambacho kinazidi asilimia 30 ya pato la mwezi husababisha changamoto ya kifedha katika kukidhi mahitaji mengine kama afya na chakula.

Na hii imekuwa ikichangiwa na kubakiwa na kiasi kidogo cha fedha jambo linaloweza kuathiri ustawi wa familia hususan watoto.

Mbali na hilo pia kupanda kwa bei ya chumba au nyumba katikia uchumi wa kawaida kumekuwa na athari ya upatikanaji wa chakula jambo linaloendelea kuzorotesha afya za familia nyingi.

Kuwapo kwa nyumba za bei nafuu kunatafsriwa kuwa sasa wananchi watakuwa na uwezo wa kupata makazi bora bila kutumia kiasi kikubwa cha vipato vyao.

Hatua hii inawasaidia kuokoa fedha ambazo zitaweza kusaidia kwenye maeneo mengine kama ya afya, chakula na hivyo kufanya familia kuwa na afya bora.

Mipango ya serikali imekuwa ni katika kuhakikisha kuwa inapunguza au kutoza viwango nafuu kwa mahitaji haya ili kuondoa gharama za ujumla za nyumba na hivyo kutoa mwanga kwa wananchi wengi kumudu kuishi maisha bora na yakisasa.

Kwa nchi ambazo hutoa ruzuku za makazi kwa kiasi kikubwa husaidia kuokoa uhaba wa chakula na mahitaji mengine muhimu.

Kuepusha maradhi

Familia masikini ambazo huishi kwenye mazingira ambayo miundombinu yake siyo rafiki kwa maana ya maji, umeme ziko kwenye hatari kubwa ya kushambuliwa kiafya.

Hii inakuwa ni tofauti na wale wanaoishi kwenye nyumba bora zilizo kwenye maeneo rasmi yaliyopimwa.

Magonjwa ya milipuko kama homa ya matumbo  na kipindupindu yana nafasi kubwa ya kupenya katika sehemu ambazo zinauhaba wa maji safi na uchakavu wa miundombinu.

Utafiti wa chuo kiku cha Emory uliozinduliwa na Taasisi ya Habitat for Humanity nchini Malawi umebainisha kuwa nyumba bora ni msingi bora wa mafanikio.

Utafiti huo unaendelea kubainisha kuwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanaoishi kwenye nyumba bora mfano zinazojengwa na kampuni ya nyumba za watumishi WHC wameepukana na mlipuko wa magonjwa yanayoenezwa kwa njia ya hewa kwa asilimia 44 ikilinganishwa na wale wanaoishi kwenye makazi yasiyobora.

Hata hivyo inaaminika kuwa watu wanaoishi kwenye mazingira dunia wamekuwa na maisha mafupi zaidi huku viwango vya vifo vya watoto vikiwa juu zaidi kufuatia kukabiliwa na maradhi lukuki ya kuambukiza.

Hakuna asiyetambua kuwa ukosefu wa hewa safi katika makazi huathiri zaidi watoto na wanawake na hivyo kujikuta watoto wengi zaidi wakipoteza maisha.

Tunashuhudia kwa siku za hivi karibuni ambapo nchi nyingi barani Afrika zimekuwa zikitumia kiasi kikubwa cha fedha ili kutibu maradhi ambayo yangeweza kudhibitiwa iwapo kila mtu angeishi kwenye makazi bora.

Kama inavyosisitizwa, kuwa kinga ni bora kuliko tiba  hivyo kuna fursa kubwa katika kupunguza matumizi ya fedha za umma katika kutibu magonjwa ya milipuko na baadhi ya yale yaenezwayo kwa njia ya hewa ambayo chanzo chake ni kuishi katika nyumba zisizo na hewa safi na ya kutosha na ukosekanaji wa utulivu.

Ni wajibu sasa kwa serikali kuhakikisha kuwa inasimamia uboreshaji wa makazi mbalimbali kwa faida ya wananchi wake kupitia kupima maeneo na kuandaa mipango inayolenga kuboresha makazi.

Kwani tafiti zinaonyesha kuwa watoto wasio na makazi wanaathrika zaidi na matatizo ya akili na kuongeza udumavu na msongo tofauti na wale wanaoishi kwenye makazi thabiti.

Athari zitokanazo na uwezo mdogo wa kumudu malipo ya kodi za nyumba, gharama za malipo ya umeme vinaweza kuwa chanzo cha ongezeko la msongo na kukosa matumaini.

Ni dhahiri pia kuwa mikakati inayolenga kuongeza upatikanaji wa nyumba za bei nafuu na uboreshaji wa makazi huleta hali bora za afya kwa wananchi.

Kampuni ya Watumishi Housing ni kati ya himaya chache za serikali ambayo imekuwa na msaada mkubwa katika kuleta makazi bora kwa wananchi  hususan watumishi wa umma kwa bei ya chini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles