27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MAKAMU WA RAIS AZIPA NENO NCHI ZA AFRIKA

Na ELIYA MBONEA-ARUSHA


NCHI wanachama wa Umoja wa Nchi za Afrika zimetakiwa kukamilisha kwa wakati michango yao ya uendeshaji wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR).

Mahakama hiyo ilianzishwa kwa mujibu wa kifungu cha kwanza cha Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu ya kuanzishwa kwa mahakama hiyo.

Itifaki hiyo ilikubaliwa Juni 9, 1998 nchini Burkina Faso na kuanza kutumika Januari 25, 2004 na shughuli zake zilianza rasmi Novemba mwaka juzi.

Akizungumza jana kwenye hafla ya kiapo cha majaji watatu wapya wa mahakama hiyo yenye makao makuu jijini hapa, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alisema uendeshaji wa mahakama hiyo unategemea fedha kutoka Umoja wa Afrika.

Alisema ipo haja kwa nchi wanachama kujitahidi kukamilisha michango yao kwa wakati hatua itakayoiwezesha mahakama hiyo kupata fungu la fedha za kutosha na kufanya shughuli zake kwa wakati.

“Mahakama hii inapangiwa fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli zake na katika hili kwanza ni fedha za michango tunayotoa sisi wanachama.

“Tujitahidi kujitegemea kwa kutoa michango yetu kwanza kabla ya kupokea michango kutoka nje ya Afrika,” alisema Samia.

Kuhusu Serikali ya Tanzania kutekeleza yaliyomo kwenye mkataba wa kuipokea mahakama hiyo hapa nchini, alisema ahadi ya kujenga majengo ya kisasa eneo la Laki Laki jijini hapa bado ipo pale pale.

“Awali Tanzania tulikubali kutoa jengo na vitenda kazi ambapo kwa kiasi fulani tumejitahidi kutoa jengo hili. Kama mnavyofahamu kwa sasa shughuli za mahakama zimetanuka, hivyo nafasi imekuwa finyu.

“Ahadi yetu ipo, kama tulivyosaini mkataba wa kuipokea na kuahidi kutoa jengo lenye nafasi na vitendea kazi. Tunalifanyia kazi, vipaumbele ni vingi kupitia marafiki na watakaopenda kutusaidia ujenzi tunawakaribisha,” alisema Samia.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa mahakama hiyo, Ben Kioko, alisema hawawezi kufikia malengo yao bila kuwapo ushirikiano wa nchi wanachama wa Afrika, Serikali ya Tanzania na wadau mbalimbali.

Majaji wapya walioapishwa ni Blaise Tchikaya kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Stella Isibhakhonem Anukam kutoka Nigeria na Imani Aboud kutoka Tanzania.

Akizungumza hatua hiyo, Jaji Aboud ambaye anakuwa jaji wa pili kutoka Tanzania baada ya Jaji Augustine Ramadhani aliyewahi kushika nafasi ya Rais wa Mahakama, aliahidi kushirikiana na majaji wengine kusikiliza na kumaliza kesi kwa wakati.

“Nimepata fursa hii si kwa uwezo wangu bali ni kwa sababu Serikali yangu imekubali na imekuwa tayari kunisaidia mpaka nimefikia hapa, naamini nchi nyingine za Afrika sasa zinaelewa masuala ya jinsia,” alisema Jaji Aboud.

Jaji Aboud alitoa kauli hiyo huku mahakama hiyo ikiwa na majaji wanawake sita na wanaume watano na kukamilisha idadi ya majaji 11 wa mahakama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles