25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MAKAMU WA RAIS AONYA FITINA, WATENDAJI KUSEMEANA KWA MAGUFULI

SAMWEL MWANGA NA DERICK MILTON-SIMIYU

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amewaonya viongozi na watendaji wa Mkoa wa Simiyu kuacha kufanyiana fitina na majungu na zaidi kushtaki mambo madogo madogo kwa Rais Dk. John Magufuli, pindi wanapotofautiana katika utendaji wa kazi zao.

Samia ambaye alikuwa akizungumza katika kikao cha majumuisho kilichofanyika katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki mjini Bariadi mara baada ya kumaliza ziara yake ya siku tano mkoani hapa, alisema mwenendo huo unakwamisha shughuli za maendeleo.

Samia alishangaa baadhi ya watendaji kutuma ujumbe kwa Rais kushtaki mambo madogo madogo ambayo kimsingi alisema yanaweza kumalizwa ndani ya mkoa huo chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka.

Akitolea mfano wa baadhi ya mambo hayo, alisema ni pamoja na maelewano mabaya kati ya Mkuu wa Wilaya ya Busega na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo.

Jingine ni kituo cha mafuta cha mbunge kutokutoa stakabadhi za mashine za kielektroniki (EFD).

Samia alishangaa masuala hayo ambayo yanaweza kutatuliwa na Mkuu wa Mkoa  yanapelekwa kwa viongozi wa juu jambo ambalo alisema linafanya utendaji wa kazi kuwa mgumu.

Makamu huyo wa rais alikiambia kikao hicho kilichohudhuriwa na viongozi na watendaji mbalimbali wa mkoa huo kuwa ushirikiano katika kazi ndani ya taasisi yoyote ni muhimu na si kutunishiana misuli.

Alisema kabla ya kupeleka malalamiko yao kwa Rais au Makamu wa Rais ni vizuri yakashughulikiwa na mkuu wa mkoa.

“Utakuta viongozi ndani ya eneo moja la utawala kama vile Mkuu wa Wilaya ya Busega na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo wanatofautiana, lakini hata suala halijapelekwa kwa mkuu wa mkoa tayari jambo hilo linapelekwa kwa Rais pia malalamiko mengine ni yale ya kuwa kituo cha kuuzia mafuta cha mbunge hakitoi stakabadhi ya EFD jambo hili linapelekwa kwa Rais.

“Rais ana mambo mengi sana ya kitaifa ambayo anapaswa kuyashughulikia, hivyo haya mengine ya tofauti kati ya DC na DED au ya mbunge kutotumia mashine ya EFD katika vituo vyake vya mafuta, yamo ndani ya uwezo wa mkoa na si kumsumbua Rais, ni vizuri mkafuata utaratibu wa ngazi kwa ngazi na si kurukia ngazi ya juu zaidi,” alisema.

Samia alisema hawakatazi mtu kuwapelekea taarifa isipokuwa ni vizuri wakaanzia ngazi za chini.

Katika hatua nyingine, Samia alionya tabia ya kupeana miradi kwa misingi ya urafiki hali ambayo imefanya miradi mingi hasa ya maji kutokamilika huku akitupia lawama vyombo kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kutochua hatua stahiki.

“Mnapeana kazi kirafiki mno na urafiki si mbaya ila urafiki wa kupitiliza si mzuri, mnashindwa kusimamiana, sasa nawaagiza wakuu wa wilaya zote za Mkoa wa Simiyu kuorodhesha miradi yote iliyopo na hatua iliyofikia ili Serikali iweze kuviagiza vyombo vinavyohusika kuchukua hatua stahiki kwa wale walioshindwa kukamilisha miradi hiyo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles