23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

Makamba, Ngeleja wamwangukia JPM

Nora Damian -Dar es salaam

RAIS Dk. John Magufuli amesema amewasamehe Mbunge wa Bumbuli, January Makamba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, baada ya kumwomba msamaha kutokana na kumtukana kupitia simu.

Hivi karibuni kulikuwa na sauti zilizokuwa zikisambaa katika mitandao ya kijamii zikimsema vibaya Rais Magufuli, ambazo zilihusishwa na January, Ngeleja, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye na makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana.

Wengine waliohusishwa na sauti hizo ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bernard Membe na Katibu Kata wa Kijiji cha Rondo mkoani Lindi.

Hadi Rais Magufuli anazungumza jana, Membe peke yake ndiye aliyewahi kujitokeza hadharani akikiri kuwa sauti iliyosikika ilikuwa yake.

Chanzo cha sauti za viongozi hao ulikuwa ni waraka wa makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Makamba na Kinana, kwenda kwa Baraza la Wazee wa chama hicho wakilalamikia hali ya mambo yanayoendelea nchini.

MSAMAHA

Jana Rais Magufuli alitangaza msamaha huo wakati akifungua mkutano wa mwaka wa mashauriano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB).

Alisema walimtukana wengi, lakini January na Ngeleja walijitokeza na kumwomba msamaha na kwa kutambua kuwa hao ni vijana, walimgusa na kuamua kuwasamehe.

“Kusamehe huwa si kitu rahisi, lakini tuna wajibu wa kusamehe na saa nyingine kusamehe huwa kunauma, lakini saa nyingine inabidi usamehe.

“Kuna watu fulani walinitukana wee na ‘nika-prove’ kwamba sauti zile ni zao ‘more than one hundred percent’ (zaidi ya asilimia 100), nikawa nakaa nafikiria, nikasema hawa wakipelekwa kwenye Kamati ya Siasa ya Central Committee adhabu itakuwa kubwa.

“Lakini wakajitokeza wawili wakaniomba msamaha, nikawa najiuliza mimi kila siku naomba msamaha kwa Mungu na ile sala ya kuomba utusamehe makosa yetu kama tunavyowasamehe wengine, nikaona hawa waliokuja kuniomba msamaha kutoka kwenye dhamira yao, nisipowasamehe nitabaki na maumivu makubwa kwenye moyo wangu.

“Niliamua nikawasamehe, ambao ni mheshimiwa January Makamba pamoja na Ngeleja, waliomba msamaha wakanigusa, nikasema hawa ni vijana wamekosea na wamekiri makosa yao na niliwasamehe na kusahau,” alisema Rais Magufuli.

SAUTI ZILIVYOANZA KUSAMBAA

Sauti zilizosambaa zikiwahusisha Nape, Kinana, January na baba yake (Makamba), zilihusu kuandaa taarifa kwa nyombo vya habari kufuatia tuhuma zilizoelekezwa kwa makatibu wastaafu wa CCM.

Siku chache baadaye ikasambaa sauti ya mawasiliano baina ya Nape na Ngeleja kisha kufuatiwa na ile ya Membe na Katibu Kata wa Kijiji cha Rondo mkoani Lindi.

Hata hivyo, Membe alipoulizwa alikiri kuwa sauti hiyo ni yake.

BARUA YA KINANA, MAKAMBA

Kinana na Makamba waliandika barua kwenda Baraza la Ushauri la Viongozi Wastaafu wa CCM wakitaka lichukue hatua dhidi ya tuhuma zilizoelekezwa kwao kwa madai kuwa zimewachafua.

Walisema shutuma zinazotolewa dhidi yao hazina ukweli na kwamba zimeandaliwa kwa lengo la kuwadhalilisha, kuwavunjia heshima, kuwajengea chuki na kuwachafulia majina ndani na nje ya chama.

Viongozi hao walisema waliamini anapojitokeza mtu kuwadhalilisha viongozi waandamizi wastaafu, hatua zitachukuliwa na taarifa kutolewa kwa umma, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kuhusu jambo hilo.

 “Mara kadhaa ametutuhumu sisi wawili, makatibu wakuu wastaafu wa CCM kwa mambo ya uzushi na uongo. Mara ya kwanza alisema tunamkwamisha rais kutekeleza majukumu yake.

“Tuliyapuuza maneno haya kwa imani kwamba viongozi wetu watayaona kwa namna yalivyokuwa, haiwezekani tushiriki kuihujumu Serikali ya chama tulichokitumikia maisha yetu yote. Haiingii akilini wastaafu wawili walio majumbani kwao eti wana uwezo wa kumzuia rais kutekeleza majukumu yake.

 “Tumeamua kutokwenda mahakamani kwa sababu unapochafuliwa unachokwenda kudai mahakamani ni fidia, kwetu sisi heshima yetu haiwezi kuthaminishwa na fidia,” walisema katika barua yao waliyomwandikia Katibu wa Baraza hilo, Pius Msekwa.

Hata hivyo Msekwa aliwajibu akisema Katiba ya CCM imekipangia kila kikao cha chama kazi za kufanya, na kwamba kazi za baraza hilo zimetajwa na kuainishwa katika Ibara ya 127 (3) ya Katiba hiyo, Toleo la 2012, kuwa ni kutoa ushauri kwa chama na kwa Serikali zinazoongozwa na chama hicho.

 “Lakini kazi zile za kuangalia mwenendo wa wanachama na viongozi wake na kuchukua hatua stahiki pale inapobidi, hizo zimepangiwa vikao vingine vya chama ambavyo ni vya utendaji kama ilivyoainishwa katika ibara zinazohusu vikao hivyo.

 “Maana yake ni kwamba kikatiba, baraza halikupewa mamlaka au ‘jurisdiction’ ya kutenda kazi hizo, ambazo ni za ki-uendeshaji. Badala yake, jukumu hilo limetolewa kwa vikao vingine ambavyo ni vya viongozi walioko madarakani,” alisema Msekwa.

Hoja nyingine kwa mujibu wa Msekwa inahusu umuhimu wa kuzingatia miiko ya utoaji ushauri ambayo ndiyo kazi mahsusi ya baraza hilo.

 “Ushauri huombwa kamwe hauwezi kushinikizwa kwa mshauriwa au kutolewa kwake kama amri, ndiyo kusema kwamba ushauri hauwezi kutolewa pale ambapo hauhitajiki. Na mwenye kuamua kuwapo kwa hitaji hilo ni yule anayehitaji kupata ushauri, siyo yule anayetaka kutoa ushauri,” alisema.

Hata hivyo alisema pale ushauri unapotolewa, unaweza amakukubaliwa aukukataliwa na unapokubaliwa thamani yake inakuwa nikubwa kwa maana ya kuondoa tatizo lililokuwapo.

Alisema pale ushauriunapokataliwa thamani yake inakuwa ni sifuri kwa maana ya kutatuatatizo lililopo.

Msekwa alisema pia jukumu la mtu yeyote aliyetuhumiwa la kusafisha jina lake ni la mtuhumiwa mwenyewe na kwamba kiutaratibu si sahihi kujaribu kukwepa jukumu hilo na kujaribu kulihamishia kwa watu wengine.

 “Hii ni kwa sababu watuhumiwa wenyewe ndio wanaojua ukweli kuhusu tuhuma hizo na kama kweli hazina msingi ni wajibu wao kufichua ukweli wanaoujua.

“Umuhimu wa jambo hili unatokana na kuwapo kwa dhana inayosema kwamba ‘silence means consent’ (ukinyamaza kimya bila kukanusha tuhuma zilizoelekezwa kwako, ukimya wako huo unachukuliwa kwamba umekiri ukweli wa tuhuma hizo). Nafurahi na kuwapongeza, kwamba tayari mmetekeleza wajibu huo kupitia vyombo vya habari,” alisema Msekwa.

Hata hivyo Msekwa aliwatahadharisha Kinana na Makamba kutoruhusu machungu ya tuhuma hizo yakawasahaulisha misingi hiyo, wakashawishika kutafuta njia za mkato za kuyashughulikia ambazo zinakiuka katiba ya chama.

 “Naomba ieleweke kwamba madhumuni ya kukumbushana juu ya mambo haya ya msingi ni kuonyesha tu ugumu uliopo wa kikatiba, kwa baraza kushughulikia malalamiko yenu kama mlivyoomba.

 “Ugumu huo unatokana na kuzingatia kuwa katiba ya chama haikutoa jukumu la kufanya kazi za ki-uendeshaji kama hii ya kusikiliza malalamiko yenu. Lakini baraza letu pia halikupewa mamlaka ya kusikiliza rufani zinazotolewa dhidi ya chama kama hii ya kwenu,” alisema.

KUNG’OLEWA JANUARY

Julai 21 mwaka huu, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa January na kumrejesha tena Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).

Wakati akimwapisha Simbachawene, Rais Magufuli alitaja sababu za kumng’oa January kuwa ni pamoja na kutotekelezwa kwa wakati kwa katazo la mifuko ya plastiki na kutotumika vizuri kwa fedha zinazotolewa na wafadhili kwa miradi ya mazingira.

Baada ya mabadiliko hayo January kupitia akaunti yake ya Twitter alisema ameyapokea kwa moyo mweupe na kumshukuru Rais Magufuli kwa kumwamini katika nafasi hiyo.

“Neno la mwisho kwenye hili; Namshukuru Rais kwa kuniamini, Makamu wa Rais kwa kunielekeza, PM (Waziri Mkuu) kwa kunisimamia na timu ya Ofisi ya Makamu wa Rais, NEMC na mawaziri wote kwa ushirikiano,” alisema January.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles