MAKAMBA ASISITIZA UMUHIMU WA KUTUNZA MAZINGIRA

0
1104
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba

 

 

Na SHOMARI BINDA -BUTIAMA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, amesisitiza umuhimu wa utunzaji na uhifadhi wa mazingira katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na kulinda uoto wa asili.

Akizungumza wakati wa kongamano la utunzaji wa mazingira kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayofanyika kitaifa wilayani Butiama mkoani Mara, Makamba alisema kila mmoja analo jukumu kubwa la utunzaji mazingira kuanzia maeneo tunayoishi.

Alisema kumekuwa na uharibifu mkubwa wa mazingira na kudai kongamano hilo ambalo limewakusanya wadau mbalimbali wa mazingira, litasaidia kufungua mijadala inayohusu kulinda na kuhifadhi mazingira.

Makamba alisema kufanyika kwa  madhimisho hayo Butiama ni kuenzi juhudi kubwa za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alikuwa mstari wa mbele katika suala zima la uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti na kulinda hifadhi za mazingira.

Alisema katika misitu iliyopo Kijiji cha Butiama, Mwalimu Nyerere alifanya kazi nzuri ambayo inapaswa kuenziwa kwa kushiriki kikamilifu katika kuyatunza mazingira na kulinda misitu iliyopo.

“Nashukuru kwa wadau mbalimbali kwa uamuzi wenu wa kuja kushiriki kwenye kongamano au mjadala huu, ambao utatusaidia kuibua changamoto mbalimbali za uhifadhi na utunzaji wa mazingira ili kwa pamoja tuweze kufanya kazi hii.

“Nashukuru familia ya Baba wa Taifa ambayo inaendelea kusimamia suala zima la utunzaji wa mazingira na wizara yetu itaendelea kutoa ushirikiano kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kufikia malengo yanayokusudiwa,” alisema.

Akizungumzia suala la mazingira na umuhimu wake, mmoja wa wanafamilia hiyo, Madaraka Nyerere, alisema kazi kubwa inatakiwa ifanyike kwa kuwa bado kuna uharibifu wa mazingira ikiwamo watu wanaojihusisha na uchomaji wa mkaa.

Alisema elimu inapaswa kuendelea kutolewa katika uhamasishaji wa utunzaji wa mazingira na kudai kwa sasa wapo watu ambao wanaingia kwenye misitu na kukata miti na kufanya uharibifu mkubwa.

Maadhimisho hayo yatafungwa leo na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, baada ya kushiriki na wananchi kupanda miti na kutembelea mabanda ya maonyesho mbalimbali ya utunzaji wa mazingira katika Uwanja wa Mwenge.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here