24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Makalla ataka wanaotupa taka ovyo wazomewe

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, amependekeza watu wanaotupa taka ovyo wazomewe ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira katika mkoa huo.

Amesema mbinu hiyo ilianza kutumiwa na Jiji la Kigali nchini Rwanda na kuliwezesha kuwa la mfano kwa usafi wa mazingira katika Afrika.

Akizungumza Novemba 26,2022 wakati wa usafi wa Jumamosi ya mwisho wa mwezi, amesema mikakati yao ni kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linakuwa kitovu cha usafi.

“Ili kuwa na ustarabu wa kuheshimu mazingira wenzetu Rwanda ilikuwa kila mtu anayetupa takataka anazomewa, huwezi ukala muhindi wako kwenye gari unashuka unatupa gunzi, sasa tunajielekeza katika ‘smart areas’ zote marufuku kutupa takataka…ukiwa na jirani yako anatupa taka ovyo mzomee ilia one aibu azichukue azipeleke sehemu husika,” amesema Makalla.

Amesema pia tayari wamesambaza mapipa 1,000 ya kutunzia taka katika daladala mbalimbali za mkoa huo na kwamba wana mpango wa kwenda kusambaza katika mabasi yaendayo mikoani.

Aidha amewataka watendaji wa mitaa kufanya tathmini za usafi wa mazingira katika mitaa na kata zao na kuhakikisha wamachinga wote wanafanya biashara katika maeneo rasmi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija, amesema watachukua hatua kwa watendaji wasiowajibika na kutahadharisha wale ambao wanaona hawawezi waombe barua wahame wapelekwe kwenye maeneo ambayo hakuna ufanyaji biashara holela.

“Tumepeana majukumu kwamba suala la usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi siyo la mkuu wa mkoa au mkuu wa wilaya, kila mkuu wa idara atatoka tutampangia eneo la kufanya usafi,” amesema Ludigija.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wamachinga Mkoa wa Dar es Salaam, namoto Yusuph, amesema bado kuna nafasi katika masoko ya Mchikichini, Kisutu na Machinga Complex na kuwataka wafanyabiashara kutoka katika maeneo yasiyoruhusiwa.

Amefafanua kuwa wanaofanya biashara kwenye maeneo rasmi wameanza kunufaika na mikopo inayotolewa na taasisi mbalimbali za fedha ambazo sharti mojawapo zinataka mteja awe kwenye eneo rasmi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles