33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Worldvision na mpango wa kuboresha ustawi wa mtoto kupitia miradi ya kijamii

Na Derick Milton, Maswa

Ustawi wa mtoto unaweza kukosekana endapo haki zote za msingi za mtoto hazitazingatiwa na mzazi au mlezi kama ambavyo sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009 inaelekeza.

Katika sheria hiyo kifungu cha 8 (1) imeelekeza kuwa ni wajibu wa mzazi, mlezi au mtu yeyote mwenye kumlea mtoto kutoa matunzo kwa mtoto kwa kumpatia haki zake za msingi kama Chakula, Malazi.

Moja ya mashamba ya mahindi wakulima ambao wanalima kilimo cha Umwagiliaji katika kijiji cha Malekano ambao wanawezeshwa na Shirika la World Vision.

Haki nyingine ni Mavazi, Dawa pamoja na chanjo, Elimu na maelekezo au mafunzo, Uhuru, na haki ya kucheza na kupumzika.

Aidha Sheria hiyo inataja ulinzi na usalama wa mtoto ni wajibu wa mzazi, mlezi au mtu yeyote mwenye kumlea mtoto kumlinda mtoto dhidi ya kutelekezwa.

Lakini pia kutengwa, kufanyiwa vurugu, kunyanyaswa, kutumiwa vibaya, na kuwa katika mazingira mabaya kimwili na kimaadili.

Hata hivyo, ustawi wa mtoto unaweza kukosekana, endapo jamii haitakuwa na uwezo wa kupata huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo huduma za Afya, Elimu, Maji pamoja na Chakula bora kwenye maeneo yao.

Upatikanaji wa Chakula bora, huduma bora za Afya na Elimu, huduma za maji safi na salama vinatajwa kuchochea kwa kiwango kikubwa cha ustawi wa mtoto kwenye familia.

Mwaka 2013 Shirika la lisilokuwa la kiserikali la World vision Tanzania katika kuhakikisha ustawi wa mtoto unapatikana, lilianzisha mpango wa maendeleo wa miaka 15 katika Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu.

Mpango huo ambao unafadhiliwa na watu wa Canada ukitekelezwa katika kata za Shishiyu, Jija na Kadoto Wilayani humo, ukilenga kuchangia katika kuboresha ustawi wa watoto wa kiume na wa kike.

Mradi huo ambao unajulikana kwa jina la Shishiyu AP (Programu ya Maendeleo Shishiyu) umejikita katika kuboresha huduma mbalimbali za kijamii, ikiwemo Afya, Elimu, Maji safi na salama lakini pia ulinzi na usalama wa mtoto.

Betty Isack ni mratibu wa Mradi huo kutoka World Vision anasema kuwa kaya 5,586 zenye watu zaidi ya 41,452 zinanufaika na shughuli zinazotekelezwa na mpango huo ambapo asilimia 90 ya wanufaika ni wale wanaojihusisha na Kilimo cha kujikimu na ufugaji mdogo.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Aswege Kaminyoge akiwa kwenye shamba la mmoja wa wakulima wanaowezeshwa na Shirika la World Vision kulima kilimo cha Umwagiliaji katika kijiji cha Malekano alipotembelea Shamba hilo.

Mratibu huo anasema kuwa kupitia mpango huo wanatarajia kuwepo kwa ongezeko la idadi ya wavulana na wasichana wa darasa la kwanza mpaka la tatu wanaosoma kwa ufahamu, ikiwa pamoja na upatikanaji wa elimu bora ya mapema ya ukuaji wa mtoto na awali ulioboreshwa.

“Pia tunatarajia ongezeko la watoto waliondikishwa shule, kubakia na kumaliza elimu ya msingi, upatikanaji endelevu wa maji safi na salama pamoja na vitendo sahihi vinavyozingatia usafi na Afya.

“Kaya zenye kuzingatia milo ya kutosha kutoka katika makundi tofauti ya vyakula, wanawake, vijana rika wa kike pamoja na watoto wanapata uangalizi wa kutosha, ongezeko la wazazi wenye kutoa malezi bora yanayosaidia kutengeneza mazingira salama,” anasema Betty.

Malengo mengine ni kuweka mifumo imara kwa ajili ya ulinzi wa mtoto, uhusishaji wa jamii katika kuweka mipango, ufuatiliaji na uendelevu wa shughuli za programu iliyoboreshwa.

Huduma ya Maji safi na Usafi wa mazingira.

World Vision inaamini kuwa uwepo wa huduma bora za maji safi na salama kwenye jamii, ni kichocheo kikubwa cha ustawi wa mtoto, kwani familia zitakuwa na uwezo wa kupata huduma hiyo kwa ufasaha.

Kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, World Vision kupitia programu hiyo imewezesha kupatikana huduma bora za maji kwa ajili ya kunywa, matumizi ya nyumbani na shughuli za umwagiliaji na ufugaji wa samaki.

Mratibu wa Mradi huo anasema kuwa kisima kimoja cha maji kimechimbwa katika kijiji cha Mwatumbe, lakini wamejenga choo cha walimu shule ya msingi Shishiyu, ujenzi wa vyoo vya kisasa kwenye zahanati na shule zilizopo ndani ya eneo la mradi.

Aidha, kupitia mradi mkubwa wa Maji wa Shishiyu, World Vision imewezesha kusambaza maji kwenye shule zote za msingi za Shishiyu, Mwaliga, Kakola pamoja na Mwatumbe ikiwemo kupeleka maji katika Zahanati zote za Shishiyu na Mwatumbe.

“Kupitia mradi huo tumewezesha kusambaza maji katika Mji wa Shishiyu, lakini pia mradi kwa kushirikiana na viongozi pamoja na wahudumu wa Afya tunatoa hamasa ya elimu juu ya afya na usafi wa mazingira ambapo zaidi ya kaya 835 zimetembelewa,” anasema Betty Mratibu wa Mradi.

Miradi yote ya maji katika vijiji vya Shishiyu na Mwaliga  ambayo imetekelezwa kupitia mradi huo imewanufaisha watu 4,454, ambapo kati ya hao watoto, 2,300 na watu wazima 2,154

Afya na Lishe

Moja ya changamoto kubwa ambayo ilikuwa ikiwakabili kwa muda mrefu wakazi wa kijiji cha Mwatimbe ni huduma za Afya ambapo walilazimika kutembea umbali wa kilometa 14 kila siku kufuata huduma katika zahanati ya Shishiyu.

Rahel Maduka mmoja wa akina mama katika kijiji hicho anasema kuwa kabla ya kujengewa zahanati na World vision katika kijiji chao, walitumia mmoja wa mti uliopo kijijini hapo kwa ajili ya kupatiwa huduma za Afya ikiwemo chanjo kwa watoto.

“Ukihitaji huduma zaidi za Afya kipindi cha nyuma, tulilazimika kwenda kilometa 14 kila siku kijiji jirani cha Shishiyu, lakini huduma za kawaida kama chanjo tulizipata kwenye mti hapa kijijini,” anasema Rahel.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu Aswege Kaminyoge akiwa kwenye shamba la mmoja wa wakulima wanaowezeshwa na Shirika la World Vision kulima kilimo cha Umwagiliaji katika kijiji cha Malekano alipotembelea Shamba hilo.

Kutokana na adha hiyo World Visioni kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji hicho, wamejenga Zahanati, kumalizia nyumba ya mganga, choo, kichoma taka na shimo la kutupia kondo la nyuma.

Zahanati hiyo ya Mwatimbe imekamila kwa asilimia 100, ambapo huduma mbalimbali za awali za Afya zimeanza kutolewa huku serikali ikileta watoa huduma wawili kwa ajili ya kutoa huduma za Afya.

Katika upande wa Lishe World Vision imewezesha uanzishaji wa vitalu vya kilimo cha mbongamboga na kutoa mbegu, viuatilifu na kuwezesha huduma za ugani na mafunzo ya lishe kwa vijana rika wapatao 853 .

“Mradi pia umewezesha upatikanaji wa vipando vya viazi lishe kwa jamii kwa lengo la kuongeza uhakika wa chakula, kuboresha afya ya watoto na jamii lakini pia kutumia ziada ya mavuno kuongeza kipato cha kaya,” anasema Betty.

Mratibu huyo anasema kuwa mradi umegawa vipando 694,900 kwa wanajamii wanaoishi katika mazingira hatarishi wapatao 893 kama njia ya maandalizi kukabiliana na janga la njaa kutokana na hali ya kukosa mvua muda mrefu.

Elimu

Katika sekta ya Elimu programu imewezesha mafunzo juu ya mbinu za ufundishaji kwa walimu wapatao 25, huku vitabu 3,600 vimetolewa katika kambi za usomaji zilizopo katika vijiji vinne vya kata ya Shishiyu.

Aidha Mradi umewezesha ujenzi wa vyoo vya walimu na wanafunzi kwa kushirikiana na jamii, ikiwemo kutoa madawati kwa ajili ya wanafunzi kuwa na mazingira bora ya usomaji darasani.

Jumla ya makambi manne ya usomaji yameanzishwa katika vijiji vitatu kata ya Shishiyu ambapo watoto wanapata nafasi ya kujifunza kusoma na kuandika baada ya muda wa masomo shuleni jumla ya watoto 350 wanashiriki mafunzo hayo.

Kilimo na ufugaji

Licha ya Programu hiyo kuwezesha kilimo cha mbongamboga kwa ajili ya lishe, jamii imewezeshwa pia kuzalisha mazao mbalimbali kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji lakini pia ufugaji wa Samaki.

Kupitia shughuli hizo mradi umechangia kuinua kipato cha kaya na kuhamasisha uzalishaji wa aina tofauti za vyakula, kwa ajili ya biashara na kula, ikiwemo uwezeshaji wa ufugaji nyuki, kuku wa kisasa.

Zahanati ya Kijiji cha Mwatumbe kata ya Shishiyu Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, ambayo imejengwa na World Vision kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji hicho, kupitia Programu ya maendeleo ya jamii Shishiyu.

Mradi umewezesha kuunda na kutoa mafunzo juu ya mbinu bora za uzalishaji wenye tija na kuwezesha kufikiwa na huduma za ugani kwa wakulima katika makundi yao.

Mayala Nengelo Mkazi wa kijiji cha Malekano ni mmoja wa wanufaika wa kilimo cha umwagiliaji akiwezeshwa na World Vision, ambapo anasema amekuwa akizalisha nyanya, vitunguu na mahindi.

Anasema kuwa kabla ya kuwezeshwa na World Vision alikuwa analima mara moja tu kwa mwaka kwa kutengemea mvua, lakini kwa sasa anazalisha kwa kutumia teknologia ya umwagiliaji.

“World Vision waliniwezesha mashine ya kumwagilia mazao yangu, mpaka nikafikia hatua ya kununua mashine yangu mwenyewe, kwa sasa familia yangu haiwezi kukosa chakula lakini pia nazalisha zaidi hadi kuuza.

“Kwa mwaka huu nimelima hekari moja ya mahindi, mbegu bora na huduma za ugani nimewezeshwa na World Vision, kupitia mazao haya nategemea kupata kiasi cha Sh. Milioni tano kama nitauza lakini na familia yangu tutakula,” anasema Nengelo.

Mratibu wa mradi anasema kuwa siyo Nengelo peke yake anayenufaika na kilimo hicho cha umwagiliaji, bali wapo wengi ambapo wamekuwa wakiwapatia mbegu bora na vifaa mbalimbali vya uzalishaji.

“Vikundi vya uzalishaji vimepatiwa mizinga ya kisasa ya nyuki, mbegu bora za kuku, vifaranga vya samaki, kuwawezesha wakulima mabwawa ya samaki, incubator, mbegu bora za malando ya viazi lishe, karanga na Alzeti.

Ulinzi na usalama wa mtoto

Moja ya matatizo makubwa kwa sasa nchini ambayo yanawakumba watoto ni vitendo vya unyayasaji ikiwemo ukatili wa kijinsia kutoka wa wazazi, walezi na wanajamii kwa ujumla.

Katika kuboresha ustawi wa mtoto, suala la ulinzi na usalama wake ni suala la msingi zaidi, kwani ni moja ya haki yake ya msingi ambayo imetajwa katika sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na mzazi au mlezi anatakiwa kuhakikisha hilo linafanyika kwa mtoto wake.

Kupitia mradi wake ambao umelenga kuboresha ustawi wa mtoto, World Vision waliona suala la ulinzi na usalama ni jambo muhimu zaidi, kutokana na matukio mbalimbali ya ukatili ambayo watoto wamekuwa wakitendewa.

Mratibu wa Mradi Betty, anasema kuwa kupitia mradi wa Shishiyu AP wameanzisha madawati ya jinsia katika shule za msingi na sekondari ambapo jumla ya wanafunzi 110 wameshiriki.

Kamati za ulinzi wa mtoto katika kila kijiji kwenye kata za mradi, zimeanzishwa ambapo zimekuwa zikishiriki katika mapambano dhidi ya ndoa na mimba za utotoni.

Busolo Limbu ni mmoja wa wajumbe wakati ya ulinzi na mtoto kijiji cha Mwatumbe anaeleza kuwa uwepo wa kamati hiyo umewezesha mmoja wa watoto ambaye alikatazwa na baba yake kwenda shule ili akamuozeshe.

“Kuna mkazi mmoja hapa kijiji maarufu kwa jina la Shetani, yeye alimzuia mtoto wake asiende shule lengo ni kumuozesha, yule mtoto kwa kuwa alipata mafunzo shuleni, alitoa taarifa na sisi tukaweza kuzima hilo jaribio la mzazi na mtoto sasa anaendelea na shule,” anasema Limbu.

Kupitia mradi huo mbali na kamati za ulinzi wa mtoto ngazi za vijiji kuundwa, walimu na viongozi wa dini wapatao 40 wamepewa mafunzo namna ya kuwafundisha na kuwapatia elimu ya dini inayolenga kuwapatia malezi bora ya kiroho wanajamii.

Serikali

Serikali inapongeza miradi yote ambayo imetekelezwa na World Vision kwa kipindi cha miaka 9 kati ya miaka 15 ya programu, ambapo inasema kuwa kazi inayofanywa ni kubwa na imewezesha kuinua kipato na maisha ya wananchi.

Aswege Kaminyoge Mkuu wa Wilaya ya Maswa, anasema kuwa katika sekta ya kilimo World Vision wamewezesha wananchi kulima kilimo cha umwagiliaji, jambo ambalo limesababisha kutokuwepo suala la njaa wakati wa kiangazi.

“Mimi sikujua kama kuna wananchi wanaweza kulima mahindi mengi kiasi hiki wakati huu wa kiangazi, niwapongeze Wolrd Vision kwa kazi kubwa ambayo mmefanya ya kuongeza kipato kwa wananchi wetu,” anasema Kaminyoge.

Mkuu huyo wa Wilaya anasema kuwa ni wajibu wa Halmashauri kutenga bajeti ya kuchimba mabwawa kwenye mito kwa ajili ya kuhimiza kilimo cha umwagiliaji kama ambavyo Rais Samia anaekeleza.

Katika miradi ya Afya, Mkuu huyo wa Wilaya anashukuru Shirika hilo kwa ujenzi wa zahanati ya Mwatumbe, nyumba ya mganga na choo, ambapo anatumia nafasi hiyo kutoa muda wa wiki mbili halmashauri kuhakikisha zahanati hiyo inaanza kufanya kazi.

“Zahanati hii ina muda mrefu imekamilika na haijaanza kutoa huduma, ndani ya wiki mbili nataka kuona huduma hapa zinaanza kutolewa, wadau wametusaidia alafu sisi serikali tunarudisha nyuma juhudi zao, hapana hiyo haikubaliki, nataka kuona wananchi wanaanza kupata huduma hapa,” anasema Mkuu wa Wilaya.

Kuhusiana na ulinzi na usalama wa mtoto Mkuu huyo wa Wilaya anaziagiza kamati za ulinzi wa mtoto ngazi ya vijiji, kuwachukulia hatua kali wale wote wanaotenda vitendo vya unyanyasaji kwa watoto.

Lakini pia juu ya mradi wa maji Shishiyu, Mkuu wa Wilaya anagiza wakala wa maji (RUWASA) Wilayani humo kuchukua mradi huo na kuuendeleza kwa kusambaza zaidi huduma ya maji kwa wananchi wengi.

World Vision

Kaimu meneja wa World Vision Kanda ya Nzega Irene Abusheikh anasema kuwa Shirika hilo, linataka watoto watambue kuwa wapo watu ambao wanataka waishi katika ustawi ulio bora kama ambavyo itanakiwa.

Anasema kuwa kupitia miradi iliyopo kwenye Programu hadi kukamilika kwake mwaka 2028, ustawi wa mtoto kwenye vijiji vyote viliyopo kwenye mpango utakuwa umeboreshwa kwa kiwango kikubwa.

Anasema kuwa World Vision inaamini kuwa ikiwa familia zitakuwa na uwezo wa kujipatia kipato kupitia shughuli wanazozifanya za kilimo na ufugaji, ulinzi na usalama wa mtoto ukawepo, huduma bora za kijamii zikawepo Ustawi wa mtoto utakuwa imara zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles