24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Wakalimani lugha ya alama kikwazo ajira kwa viziwi

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Changamoto ya wakalimani wa lugha ya alama imesababisha baadhi ya viziwi kushindwa kufanya vizuri kwenye usaili wa nafasi mbalimbali za kazi wanazoomba.

Akizungumza na Mtanzania Digital nyumbani kwao Keko, Joyce Jumbe (31) ambaye ni kiziwi na mhitimu wa Shahada ya Sayansi ya Jamii na Uongozi kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU), amesema aliwahi kuomba kazi sehemu tano tofauti na kote huko hakukuwa na mkalimani wa lugha ya alama wakati wa usaili.

Amesema alikuwa akifanya usaili kwa kuandika au kujibu maswali baada ya kumuangalia usoni yule anayemuuliza.

“Niliomba kazi ya Social Worker Muhimbili nikaitwa kwenye ‘interview’ iliyofanyika DUCE. Hakukuwa na mkalimani lakini nilijieleza kuwa nina matatizo ya kusikia, walinipa karatasi nikaandika majibu ya maswali waliyoniuliza… nilianguka kwenye hatua ya kwanza ya ‘interview’ sikuingia hatua ya pili.

“Kwingine nilikwenda unakaa unamuangalia usoni HR (Human Resource) anakuuliza unajibu, ‘interview’ inataka ‘attention’ kuna mengine unajibu sivyo ulivyoulizwa kumbe tayari nimekosa sifa…nafeli si kwa kupenda ni kwa sababu ya kutokuwa na mkalimani,” amesema Joyce.

Joyce ambaye awali alikuwa akifanya kazi ya upishi katika Hoteli ya Serena Dar es Salaam amesema wakalimani wa lugha ya alama ni kiungo muhimu cha mawasiliano kwa viziwi na kwamba wanapokosekana jamii inayowazunguka inakuwa haiwaelewi.

“Hata vikao ofisini hawaweki mkalimani unakuta watu wanacheka unatamani kucheka lakini utachekaje wakati husikii,” amesema.

Joyce ameshauri suala la wakalimani wa lugha ya alama lipewe kipaumbele hata katika mazingira ya kazi huku akitaka pia Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Namba 9 ya mwaka 2010 itekelezwe ipasavyo hasa katika suala la haki ya ajira kwa wenye ulemavu.

“Viziwi wengi tumesoma lakini hatuna kazi waajiri hawatuamini kwamba nasisi tunaweza, wasitukatie tamaa tupewe nafasi watuamini wasituone kama ni watu ambao hatuwezi,” amesema Joyce.

Naye Ofisa Uhusiano wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), Msafiri Mhando, amesema wakalimani wengi walikuwa hawatambuliki kwa sababu hawakupitia chuo cha kitaaluma kinachotambulika na serikali hivyo wengi wamefundishwa kipitia mafunzo na kozi fupi za CHAVITA.

Amesema ukalimani una maana pana kwamba mtu anatakiwa awe amefuzu mafunzo maalumu ya ukalimani si kujua lugha ya alama. Kwa Tanzania wakalimani wengi walikuwa hawatambuliki kwa sababu hawakupitia chuo cha kitaaluma kinachotambulika na serikali, bali wamefundishwa kipitia mafunzo na kozi fupi za CHAVITA.

“Changamoto itaisha mara tu kanuni ya huduma ya ukalimani itakapokamilika na kusimamiwa na serikali,” amesema Mhando.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Dk. Aggrey Mlimuka, amesema wamekuwa wakiwahamasisha wanachama wao kuajiri watu wenye ulemavu na kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha wenye ulemavu kufanya kazi bila vikwazo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles