29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Wahitimu wa elimu ya juu na kitendawili cha kujiajiri

Swali: Kwanini Wahitimu Wanashindwa Kujiajiri?

Nimejaribu kujielimisha kidogo kama kuna ugumu wowote kwa wahitimu wa elimu ya juu kujiajiri. Nimejifunza kwamba, vikwazo vikubwa kwao kuhusu kujiajiri ni mfumo wa elimu kutokuwajengea tabia ya kujiajiri na changamoto ya kupata mitaji.

Wahitimu wa elimu ya juu wanatumia zaidi ya muongo mmoja na nusu darasani na kwa wakati wote huo, mfumo uliopo hauwaandai kujiajiri.

Kwa mfano, vyuo vingi vikubwa nchini kikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM) vina kozi ambazo wanafunzi wote lazima wazisome, ikiwemo maarifa ya mawasiliano, fikra yakinifu na somo la maendeleo.

Licha ya uhalisia kuwa kujiajiri ni suluhisho la changamoto ya ajira nchini na duniani kote, kozi ya ujasiriamali katika vyuo hivyo na vingine inafundishwa kwa wachache tu ama kwa wale wanaosomea masomo ya biashara au kupitia semina za kujiajiri ambazo mara nyingi haziwafikii wote. Linapokuja suala la kutakiwa kujiajiri, hilo halichagui ulijifunza au haukujifunza.

Kuhusu mazingira yasiyo rafiki ya kupata mitaji kwa ajili ya kujiajiri, mhitimu anaweza kupata mtaji ama kutoka katika taasisi zaki fedha au katika mifuko ya uwezeshaji wa vijana inayoanzishwa na serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (YDF) na zile zinazotolewa kutoka kwenye 4% ya makusanyo ya Halmashauri.

Fursa ya kupata mikopo ya mitaji kutoka benki ina changamoto nyingi ikiwemo masharti magumu ya kuwa na dhamana ya hati ya mali isiyohamishika kama vile nyumba, kiwanja au gari, vitu ambavyo mhitimu huenda asiwe navyo.

Changamoto ya kupata mikopo ya serikali kupitia YDF na fedha za halmashauri inatokana na masharti magumu ambayo hayamruhusu mtu mmoja mmoja kupata mkopo pia, hata akitimiza matakwa ya kuwa kwenye kikundi cha kuanzia watu watano, wanatakiwa kuwa na biashara ambayo tayari imeanza na mpango wa biashara unaoonesha rekodi ya mapato ya awali na namna watakavyotumia fedha hizo.

Fursa ya pili ndio pengine ingekuwa kimbilio jepesi, lakini bado changamoto ipo katika kuifikia hiyo mikopo na huenda wahitimu wengi wa elimu ya juu hawaoni nafasi yao katika fedha hizo.

Swali: Nini Kifanyike ili kuwawezesha wahitimu kujiajiri?

Kwanza kabisa elimu ya kujiajiri/ujasiriamali inatakiwa itolewe kwa wanafunzi wa ngazi zote nchini. Ninaamini kwamba, kujiajiri kunajengwa na tabia ya ujasiriamali ambayo mtu anapaswa kuwa nayo na tabia ni kitu kinachojengwa kwa muda mrefu.

Katika suala la kujenga tabia ya ujasiliamali, tunaweza kuanzia na elimu msingi, kwa kurejelea mitaala na kurudisha au kuweka somo ama vitu fulani ndani ya masomo yaliyopo ambavyo vitajenga tabia ya ujasiliamali au kujiajiri.

Katika somo hili, mwanafunzi aanze kujifunza kutokana na daraja lake la elimu nini maana ya kujiajiri au ujasiriamali. Endapo mtaala utatengenezwa vizuri, somo hili lizidi kupanua wigo wa ufahamu wa suala la ujasiliamali katika kila sekta kutoka darasa moja kwenda darasa la hatua nyingine hadi kufikia elimu ya juu.

Ninaamini kwa kufanya hivi, mwanafunzi atakuwa atajifunza vitu vingi na hata kwa wale ambao hawapati fursa ya kuendelea na elimu ya juu kutokana na ufaulu, basi na wao watakuwa wameambulia kitu cha kwenda kuanzia kujiajiri kulingana na elimu ya kujiajiri waliyoipata kuanzia darasa la kwanza hadi kufikia kiwango cha elimu wanachoishia.

Uanzishwe Mfuko wa Uwezeshaji Wahitimu Kiuchumi (Gradiates Ecomic Empowerment Fund – GEEF)

Pendekezo hili lina lenga kuhakikisha kwamba, wahitimu angalau wa ngazi ya shahada wanapata mikopo ya mitaji mara tu baada ya kumaliza masomo yao, ili kwa kutumia elimu waliyoipata ya kujiajiri/ujasiriamali tangu waanze masomo yao na kwa kutumia kiasi kidogo cha fedha ambacho mfuko huo utawawezesha, basi wakawe na sehemu ya kuanzia katika kujitegemea na kujiajiri huko mtaani.

Kwa maoni yangu, nadhani, kiasi kisichopungua Sh 1,000,000 kinaweza kusaidia kumuwezesha mhitimu kuanza kujiajiri.

Zipo namna nyingi zinaweza kuuwezesha mfuko wa GEEF kupata fedha za kuwakopesha mitaji ya kujiajiri wahitimu wa elimu ya juu.

Hii ni pamoja na; Kupitia fedha za wanufaika wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu – HESLB.
Serikali inaweza kukata Sh 1,500 kutoka kwenye Sh 8,500 anazopewa mwanafunzi kwa ajili ya kula na malazi na fedha hiyo ikawekwa kwenye mfuko wa GEEF.

Au, ikionekana kupunguza kutamuumiza mwanafunzi, serikali inaweza kuongeza Sh 1,500 katika fedha anayopewa hivi sasa mwanafunzi kwa siku (iongezeke kutoka Sh 8,500 hadi Sh 10,000) na kiasi kilichozidi Sh 1,500 kikawekwa kwenye mfuko wa GEEF.

Vyovyote itakavyokuwa, iwe ni kwa kupunguza kiasi cha fedha anachopokea sasa au kwa kuongeza kiasi kilichopendekezwa, namna hii ni rahisi zaidi na yenye uhakika wa kusaidia wanafunzi wengi kwa mara moja.

Kwa mfano, mfumo huu ungeanza kutumika kwa wanufaika wa mwaka wa kwanza 65,000 waliopata mikopo ya HESLB mwaka wa masomo 2021/2022, baada ya miaka mitatu, kungekuwa na kundi kubwa la wahitimu ambao wangekuwa na uhakika wa kupata mtaji wa kuanzia usiopungua Sh 1,080,000.

Muhimu kuzingatia, pendekezo hili linatekelezeka endapo tu litaanza kwa wanufaika wapya tangu wanaanza mwaka wa kwanza.

Jambo hili siyo geni na ni sawa tu na kinachofanyika kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kama NSSF kwa kukata sehemu ya mapato ya mishahara ya watumishi.

Kupitia 1% ya Mapato ya Halmashauri

Kwa lengo la kuwawezesha wahitimu kujikwamua na tatizo la pili la kujiajiri ambalo ni mitaji, basi ikiwezekana, asilimia 1% tu kati ya 4% za mapato ya halmashauri ambazo hutengwa kwaajili ya vijana, zipelekwe kwenye mfuko wa Taifa wa Uwezeshaji wahitimu kiuchumi GEEF.

Hii itasaidia kuongeza uwezo wa mfuko huo kuwawezesha wahitimu wengi zaidi kiuchumi mara tu baada ya kuhitimu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI ya Robo ya kwanza ya mwaka ya makusanyo ya halmashauri nchini kwa mwaka 2021, jumla ya makadirio ya mapato ambayo halmashauri zote nchini zilijiwekea ni Sh bilioni 863.9.

Hii inamaanisha kuwa, kwa pendekezo langu katika eneo hili, asilimia 1% ya mapato yote ya halmashauri iende kwenye mfuko wa kuwezesha wahitimu kiuchumi.

Hii ni sawa na Sh bilioni 8.6 (kwa kutumia akisi ya makusanyo tajwa). Fedha hiyo pekeyake, inaweza kuwawezesha wahitimu 8,600 kwa mgawanyo wa Sh 1,000,000 kwa kila mhitimu na sio kwa kikundi.

Mwisho, tuwawezeshe wahitimu wa elimu ya juu kutatua kitendawili cha kujiajiri kwa kuwapa elimu ya kujiajiri na kuondoa vikwazo vya kupata mitaji.

Mwandishi wa makala haya ni Joseph Malekela ambaye ni mdau wa Maendeleo ya Vijana nchini na Mwanafunzi wa Mwaka wa Tatu Shahada ya Sanaa katika Falsafa na Maadili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles