24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Wadau wataka msimamo wa Rais Samia kuhusu uzazi wa mpango

*Wataka uungwe mkono kwa vitendo

Na Damian Masyenene

WADAU wa masuala ya afya ya uzazi, wanawake na watoto nchini wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha mwelekeo chanya katika jitihada za kumlinda mtoto wa kike na kupunguza kasi ya kuzaa huku wakitoa wito kwa watendaji kumuunga mkono na kumsaidia kwa vitendo kutimizwa kwa azma yake.

Akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Geita Oktoba 17, 2022 akiwahutubia mamia ya wananchi wa kata ya Runzewe wilayani Bukombe, Rais Samia aliwataka wananchi kupunguza kasi ya kuzaa ili huduma za kijamii na fursa za maendeleo zilizoko zitosheleze katika kuboresha maisha ya kila Mtanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwapa tuzo baadhi ya waanzilishi wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo barani Afrika (WiLDAF) pamoja na vyeti kwa wadau waliofanikisha maendeleo ya Shirika hilo kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya kuanzishwa kwake kwenye hafla iliyofanyika Oktoba 20, 2022 jijini Dar es Salaam.

Rais Samia alitoa kauli hiyo kufafanua kile kilichozungumzwa mwanzo na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Shaka Hamdu Shaka kuwataka wananchi wa eneo hilo kuendelea kuzaa kwa kuwa huduma za kijamii zinaendelea kuboreshwa.

Katika maadhimisho ya miaka 25 ya Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo barani Afrika (WiLDAF) yaliyofanyika Oktoba 20, 2022, Rais Samia alisisitiza mambo mbalimbali ikiwemo kubadilisha sharia ya ndoa hususan kipengele cha umri wa kuolewa, kutengeneza mikakati ya kuwasaidia wa kike waliokatishwa masomo kutimiza ndoto zao na kuzipitia upya sharia za uzazi wa mpango kwani kasi ya wanawake kuzaa iko juu licha ya jitihada nyingi za kutoa elimu kwa umma.

Akizungumzia hatua hiyo, Mshauri wa afya ya uzazi na malezi nchini, James Mlali amesema kiuchumi jamii ya Kitanzania inakua kwa kasi ndogo kutokana na utegemezi wa kiwango cha juu wa makundi ya umri mdogo ukilinganisha na kundi dogo la watu wanaozalisha na kuchangia kwenye kukuza uchumi na kupunguza umaskini.

“Ndiyo maana Viongozi wetu, Mheshimiwa Rais akiwa mstari wa mbele, wanatoa maelekezo ya kisera ili wananchi na watendaji wachukue hatua za utekelezaji kwa ajili ya kuboresha Afya ya Mama na Mtoto na jamii nzima na kuinua hali ya uchumi. Rais (Samia) ni ni Mama na Mzazi,” amesema Mlali.

Afisa Miradi wa shirika la Thubutu Africa Initiative (TAI), Paskalia Mbugani amesema licha ya Rais kuonyesha nia njema katika kumlinda mtoto wa kike, kuboresha afya ya uzazi kwa kudhibiti vifo vitokanavyo na uzazi lakini baadhi ya watendaji hawaendani na kasi hiyo hivyo kukwamisha juhudi mbalimbali zinazopigwa na wadau wa afya na haki za mama na mtoto.

“Kwa mfano kwenye suala la umri wa kuolewa nikiangalia tamko la wizara ya katiba na sheria napata mashaka kama Serikali na sisi tunaongea lugha moja, wakati wadau tunapiga kelele kuhusu hilo unaona Serikali inapiga hatua kurudi nyuma. Matamko na uhalisia ni vitu tofauti sana hata suala la kurudi shuleni baada ya kujifungua mazingira yaliandaliwa kuwapokea hao watoto? Kila mmoja atomize wajibu wake katika nafasi aliyopo,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa asasi ya Fikra Mpya, Leah Josiah amesema Rais Samia kwa kuwa ni Mwanamke na Mama anaelewa kwa kina muktadha wa masuala ya ukatili yanayotokea kwenye jamii kuanzia ngazi ya familia na ameonesha na kutoa ushirikiano katika kupambana na ukatili hivyo wadau wanapaswa kushirikiana naye ili kuwa na jamii salama isiyo na ukatili.

“Rais wetu anafanya vyema kwa nafasi yake lakini kazi kubwa inabaki kwenye kutilia mkazo matumizi ya sheria zilizopo, endapo sheria zitatafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili wananchi watazifahamu na kila mmoja anapaswa kujua nafasi aliyopo katika kujenga jamii salama isiyo na ukatili. Pia baadhi ya sheria ikiwamo ile ya ndoa irekebishwe, zitiliwe mkazo na zifuatwe,” amesema Leah.

Rais Samia amekuwa msitari wa mbele kuhakikisha tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi linakwisha nchini ambapo Novemba, 2018 akiwa Makamu wa Rais alizindua kampeni ya “Jiongeze Tuwavushe Salama” ya kuongeza kasi ya uwajibikaji kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga huku akiwaagiza wakuu wa mikoa kuifanya afya ya uzazi na mtoto kuwa ajenda ya kudumu katika vikao vya ushauri vya mkoa (RCC).

Afua ya kwanza katika kampeni hiyo Uzazi wa Mpango ambayo inawawezesha wanawake na wasichana kujikinga na mimba zisizotarajiwa (yaani za mapema, za utotoni, na za utu uzima zaidi) ambazo ndizo, kwa kiwango kikubwa husababisha vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na athari zingine za uzazi usio salama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles