24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAKALA| Mwelekeo na uwiano wa matumizi ya Uzazi wa Mpango Geita

Na Yohana Shida, Geita

MKOA wa Geita uliopo Kanda ya ziwa nchini Tanzania ni miongoni mwa wanufaika wakubwa wa huduma pamoja na elimu ya afya ya uzazi ambayo imeendelea kutolewa na mashirika, taasisi za umma na binafsi chini ya usimamizi wa Wizara ya Afya.

Manufaa hayo yamechagizwa na ongezeko la vituo vya afya ambapo hadi Februari mwaka 2021 mkoa wa Geita ulikuwa na vituo vya kutolea huduma ya afya 183 kati yake vituo vya serikali vikiwa ni 136 sawa na asilimia 75 huku vituo vya binafsi vikiwa ni 47 sawa na asilimia 25.

Katika mahojiano maalumu na Mwandishi wa makala hii, Mratibu wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto mkoa wa Geita, Daniel Sinda anabainisha, kwa ujumla ubora wa miundombinu umeimarisha huduma za afya ya uzazi huku elimu ikiongeza mwamko wa matumizi ya uzazi wa mpango mkoa hapa.

Upatikanaji wa Huduma za Uzazi wa Mpango Geita

Akizungumuzia juu ya hali ya upatikanaji wa Huduma ya Uzazi wa Mpango mkoani hapa, Mratibu huyo anasema hadi sasa huduma inapatikana katika vituo vyote vya kutolea huduma na hadi Juni mwaka 2022 jumla ya vituo 165 mkoani Geita vimethibitika kutoa huduma ya uzazi wa mpango.

Mratibu wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto mkoa wa Geita, Daniel Sinda.

Sinda anasema, takribani katika vituo vyote kuna uhakika wa huduma za uzazi wa mpango ambapo ukiachilia mabli vituo 165 vya umma vinavyotoa huduma ya afya ya uzazi, lakini kuna vituo vya binafsi ambavyo pia vinatoa huduma hiyo.

“Kwa maana nyingine vituo vinavyotoa hii huduma vipo karibia kila kata, bado hatujawa na ile ya kufikisha huduma kwenye kila kijiji, kwa hiyo wale wahitaji wa hizi huduma sasa wanapata huduma kutoka kwenye vituo ambavyo vinawazunguka,” anasema Sinda.

Anaeleza, kwa maeneo ambayo bado hayajafikiwa na vituo vya afya vyenye kutoa huduma ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango vinanufaika moja kwa moja na kampeni ya Mkoba ambapo watoa huduma hutoka vituoni na kuwafuata wananchi kwenye maeneo yao.

“Lakini ukiacha mbali na vituo vyenyewe kufanya huduma za Mkoba kuna wadau ambao tunafanya nao kazi katika eneo la huduma za afya ya uzazi ikiwemo Marie Stopes, In-Gender Health, USAID Afya Yangu ambao hawa wote wanatusaidia katika eneo hili.

“Kwa upande wa wataalamu watoa huduma hatuna changamoto kwa sababu watoa huduma kila vituo wamepata mafunzo na ukienda katika kila kituo kuna si chini ya watoa huduma wawili ambao wamepata mafunzo ya huduma ya afya ya uzazi na mtoto.

“Kwa hiyo hatutegemei kwamba mteja aende kwenye kituo cha huduma harafu akute kwamba hakuna mtaalamu ambaye atamusaidia kupata hiyo huduma. Wataalamu tunao wa kutosha na wote wamepata mafunzo na huduma inatolewa vizuri kabisa,” anasema Sinda.

Uwiano wa Matumizi ya Njia za Uzazi wa Mpango Geita

Akitoa takwimu juu ya mwitikio na uwiano wa matumizi ya njia tofauti za uzazi wa mpango toka mwaka 2017, Sinda anasema mwamko umeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka kulingana aina kwa maana ya njia za muda mfupi, muda mrefu na njia za kudumu.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

Anaeleza, takwimu zinaonyesha kwa mwaka 2017 mkoa wa Geita kulikuwa na watumiaji 3,467 waliojiandikisha kupatiwa huduma ya njia ya uzazi wa mpango kwa njia vidonge lakini ilipofika mwaka 2021 watumiaji 8,439 walisajiliwa kutumia njia hiyo ya uzazi wa mpango  

Sinda anasema kwa upande wa njia ya uzazi wa mpango ya sindano, mwaka 2017 kulikuwa na jumla ya wateja 14,334 lakini kufikia mwaka 2020 iliongezeka na wateja 28,067 walisajiliwa kuchoma sindano za kupanga uzazi.

“Kwa mwaka 2021 takwimu ilishuka kidogo ukilinganisha mwaka 2020, lakini ukilinganisha 2017 na hiyo 2021 bado pia kuna ongezeko kwa sababu kwa 2021 tulikuwa na jumla ya wateja 27,296 ambao walipanga uzazi kwa njia ya sindano.

“Lakini idadi hiyo ilishuka kwa mwaka 2021 ikilinganishwa na mwaka 2020 ni kwa sababu tu kipindi hiki kulikuwa na changamoto kidogo ya upatikanaji wa hii njia ya uzazi wa mpango lakini si kwamba labda kulikuwa hakuna wateja ambao walihitaji kutumia hii njia.” Anafafanua.

Sinda anabainisha, njia nyingine ya uzazi wa mpango ambayo kina mama wengi wamevutiwa zaidi kuitumia ni njia ya vipandikizi maarufu kama njiti ambapo kwa mwaka 2017 kina mama 33,481 walisajiliwa kutumia njia hiyo kupanga uzazi

“Ilipofika mwaka 2020 idadi hiyo ilipanda kutoka 33,481 mpaka kufikia watumiaji 85,769, Lakini kidogo imeshuka kwa mwaka 2021 kwa sababu pia kuna kipindi ambacho hii njia upatikanaji wake ulikuwa tatizo na ilishuka mpaka watumiaji 42,488.

Sinda anaongeza “Tuna njia nyingine ya uzazi wa mpango, ambayo tunaita ni njia ya kitanzi, hii kwa mwaka 2017 tulikuwa na wateja 11,085 ambao walitumia hiyo njia na idadi hiyo ilipanda kwa mwaka 2019 na kwenda mpaka watumiaji 18,150.

“Lakini kwa mwaka 2020 ilishuka kidogo mpaka 17,729 huku kwa mwaka 2021 matumizi yalishuka mpaka 12,151. Lakini kushuka huku si kwamba wateja hawakuwepo bali kama ilivyo kwa njia zingine upatikanaji wake unakuwa ni wa shida na wanaokuja kuhitaji hizi njia wanakosa.

Akizungumuzia njia ya kudumu ya uzazi wa mpango (kufunga kizazi) Sinda anaweka wazi, kwa mwaka 2017 akina mama 6,210 walifungiwa vizazi ambapo kwa njia hii takwimu zimekuwa zikishuka na kwa mwaka 2021 ni kina mama 1,929 pekee walifungiwa uzazi kama njia waliyochagua ya uzazi wa mpango.

“Tukiangalia hizi njia zote uzoefu unatuonyesha njia ya vipandikizi au njia ya njiti, hii inaonekana akina mama wengi wanapendelea kuitumia kwa kuwa mama akitumia kipandikizi ana nafasi ya kuchagua kipandikizi cha miaka mitatu au mpaka mitano na anaweza kukitoa akitaka kupata mtoto,” anasema.

Mikakati ya Kuimarisha Uzazi wa Mpango Geita

Akizungumuzia mikakati ya kutanua uwigo wa huduma ya uzazi wa mpango mkoani hapa, Sinde ambaye ni Mratibu wa kitengo hicho anasema kwa mwaka huu njia zote za uzazi wa mpango zinapatikana kwa uhakika na wateja wanaendelea kupatiwa kwa utimirifu kadri ya matakwa yao.

“Mkakati uliopo kwetu sisi kama idara ya afya mkoa wa Geita ni kuweza kuwafikia wateja wengi zaidi, kwa sababu kama tunavyojua Geita ni moja ya mikoa ambayo ina wakazi wengi, na kile kiwango cha kuzaliana kwa Geita kiko juu.

“Kwa hiyo ili tuweze kufikia malengo, moja tuna wadau wetu ambao tunafanya nao kazi, ambao sasa hao tunategemea kwa kipindi hiki ambacho kinakuja kuanzia oktoba mwaka huu tutaingia zaidi ngazi ya jamii.

Sinda anaeleza, Idara ya Afya kitengo cha afya ya uzazi  na mtoto mkoani Geita imejipanga kuwekeza zaidi katika elimu ya uzazi wa mpango, kutoa mafunzo kwa watoa huduma na kuimarisha huduma ya Mkoba.

“Tunategema elimu zaidi itaendelea kutolewa ngazi ya jamii kupitia vyombo vya habari ikiwemo redio za kijamii. Kwa hilo litafanyika kuhakikisha kwamba wateja wetu wanapata taarifa ambazo ni sahihi na ambazo zitawafanya washawishike kwenda kupata huduma.”

Uwiano wa Utumiaji Uzazi wa Mpango Kitaifa 

Akiwasilisha mapendekezo ya bajeti ya wizara ya afya kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Waziri Mwenye dhamana, Ummy Mwalimu anabainisha kuwa serikali imeendelea kuboresha huduma ya uzazi wa mpango nchi nzima.

Waziri Ummy anasema, katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022, Wizara kupitia Bohari ya Dawa (MSD) ilinunua na kusambaza vidonge vya uzazi wa mpango dozi 1,755,349 sawa na asilimia 82 ya lengo.

Anaeleza, jumla ya sindano za uzazi wa mpango (aina ya depo-provera) dozi 2,125,625 sawa na asilimia 93 ya lengo huku vipandikizi 206,000 sawa na asilimia 78 ya lengo zilinunuliwa na kusambazwa katika halmshauri zote nchini.

“Katika kipindi hicho, (mwaka 2021) jumla ya wateja waliotumia njia za uzazi wa mpango walikuwa 4,189,787 ukilinganisha na wateja 4,357,151 waliokuwa tayari kupokea na kutumia huduma ya uzazi wa mpango kwa mwaka 2020. 

“Njia hizo za uzazi wa mpango zimetolewa katika vituo mbalimbali vya huduma za afya nchini ni pamoja na vipandikizi asilimia 57.1, sindano asilimia 18.5, vidonge asilimia 10.1, kondomu asilimia 5.3, kufunga kizazi mama asilimia 0.4, Kitanzi asilimia 7.2 na njia zingine asilimia 1.4,” anasema.

Matazamio ya Wananchi Juu ya Huduma ya Uzazi wa Mpango

Aisha Mohamed (35) mkazi wa mtaa Nyankumbu mjini Geita anakiri huduma za uzazi wa mpango zimeimarika kwenye vituo vya afya mkoani Geita lakini anaiomba serikali kuongeza watalaamu watakowafuata na kuwasaidia watumiaji wanaokutana na changamoto baada ya kutumia.

Martha Jospeh (30) mkazi wa mtaa wa Miti Mirefu mjini Geita anakiri kuwa njia ya vipandikizi ama njiti imewavutia kina mama wengi ambapo mbali na yeye kutotumia lakini ameshuhudia kina mama wengi wametumia huku akiwaomba watalaamu kutoa elimu zaidi ya njia hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles