24.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Maswa wakubaliana kukomesha ndoa za utotoni

Na Samwel Mwanga,Maswa

SERIKALI katika wilaya ya Maswa kwa kushirikiana na Wadau na Mashirika mbalimbali ya maendeleo katika wilaya hiyo kwa kauli moja wamekubaliana kukomesha ndoa za utotoni.

Kwa wilaya ya Maswa takwimu za mwaka jana za athari za ndoa za utotoni zinaonyesha ya kuwa msichana mmoja kati ya watatu wanaolewa kabla ya kufikisha miaka 18.

Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake alisema kuwa kampeni yao hiyo inalenga kuungwa mkono na jamii katika wilaya hiyo ili kuongeza umri wa msichana kuolewa na kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu umuhimu wa mtoto wa kike.

Alisema kuwa athari anazokumbana nazo  msichana anapokuwa na hali ya kutarajia kukatisha masomo, utoto na ndoto zao ili kuolewa, inadhuru afya yao ya akili, na wanakabiliwa na mduara wa ukatili, unyanyasaji, changamoto za kiafya na umaskini.

“Kati ya wasichana watatu, mmoja anaolewa chini ya umri wa miaka 18 katika wilaya yetu hii inamfanya msichana apoteze fursa za elimu na ujuzi wa kazi, kupata  maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU), fistula au magonjwa ya zinaa, kunyanyasika kisaikolojia, kimwili, kijinsia na hivyo kudhuriwa kwa haki na utu wao.

“Hili lazima tulikemee kwa kuwa linaathiri kuyumba kiuchumi na kudumu katika umasikini, vifo vya watoto wachanga na watoto wa kike pindi wanapojifungua kwa kuwa viungo vyao vya uzazi bado havijakomaa pia inaongeza  vifo vya wajawazito na kuharibika kwa mimba,” amesema.

Alisema kuzuia ndoa za utotoni ni mwanzo wa kukabiliana na masuala mengine makubwa yanayowahusu watoto na matarajio ya vijana na fursa za maisha, thamani ya wasichana katika jamii, kuvunja mzunguko wa umasikini, na kuhakikisha nafasi za vijana kama wakala wa ndoa za utotoni zinakosa nafasi.

Kaminyoge alisema kuwa kwa  mujibu wa takwimu za UNICEF, inakadiriwa kuwa, wasichana watatu kati ya 10 nchini wanaolewa wakiwa bado watoto, na kuifanya Tanzania kushika nafasi ya 11 kwa ndoa za utotoni duniani.

Naye Afisa ustawi wa Jamii wilaya ya Maswa,Grace Mmasi alisema kuwa sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inaweka miaka 18 kuwa umri mdogo ambao wavulana wanaruhusiwa kuoa, lakini imeweka umri wa miaka 15 kwa wasichana kuolewa kwa ridhaa ya wazazi, sheria hiyo ni vizuri serikali ifanyie marekebisho, kwani inapingana na wakati na haipo wazi, ikishindwa kufafanua mtoto ni nani.

Kwa upande wa Mwandishi wa Redio Sibuka Fm, Nicholaus Machunda alisema kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kutoa elimu ili kusaidia kutokomeza ndoa za utotoni katika wilaya hiyo.

 Alisema  kwa kuwa wanaoathirika zaidi ni wasichana wanaoishi pembezoni, hivyo juhudi kubwa za wamiliki na waandishi wa habari ni kupaza sauti kuwasemea wale ambao hawawezi kujisemea.

“Sauti  inapazwa na vyombo vya habari kwani tunahamasisha kampeni hizi ziende zaidi  maeneo ya vijijini maana huko ndiko athari hizi zinatokea zaidi na wazazi, walezi na wasichana wenyewe hawana taarifa,” alisema.

Naye Mkuu wa dawati la jinsia la Jeshi la Polisi wilayani humo, Koplo Juliana Mjena alisema kuwa  viongozi wa vyombo vya dini waunge mkono kampeni hiyo kwa lengo la kupambana na tatizo la watoto kuolewa katika umri mdogo.

‘Viongozi wetu wa dini ni watu muhimu sana katika jamii hivyo ni vizuri wakaunga mkono kampeni hii kupitia nyumba za ibada na kwenye mikusanyiko ambayo wao wanakuwa wazungumzaji wakuu ili tuweze kupambana na tattizo la watoto kuolewa wakiwa katika umri mdogo,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles