25.6 C
Dar es Salaam
Friday, December 2, 2022

Contact us: [email protected]

Makala| Maswa na mkakati wa kupambana na ndoa za utotoni

Na Samwel Mwanga, Maswa

Mkoa wa Simiyu ulio kusini mwa Ziwa Victoria mwa Tanzania ni miongoni mwa mikoa inayotajwa kushamiri kwa ndoa za utotoni.

Takwimu kutoka mashirika mbalimbali ikiwemo UNICEF zinaonyesha kuwa kwa siku watoto 2 hapa nchini wanahusika katika ndoa  za utotoni.

Kwa mujibu wa wataalamu, hali hii imekuwa ikiendelea kwa muda mrefu na kwa asilimia kubwa imezorotesha maendeleo ya mtoto wa kike katika eneo hilo.

Ili kumwokoa mtoto wa kike kutokana na janga hili, kumekuwa na jitihada mbalimbali kutoka serikalini na mashirika yasiyo ya kiserikali za kuwaokoa hasa wale ambao tayari wameshatumbukia katika dimbwi hilo.

Ukubwa wa tatizo Mkoa wa Simiyu ni moja ya mkoa hapa nchini ulioathirika  kwa ndoa za
umri mdogo hapa nchini ni mkoa wa pili huku mkoa wa Shinyanga ukitajwa kuwa kinara wa ndoa za utotoni.

Kwa wastani,wasichana wawili kati ya watano huolewa kabla hawajatimiza miaka 18. Mwaka 2018 jumla ya wasichana 239 wenye umri chini ya miaka 14 walioolewa kabla ya kufikia miaka 18.

Takwimu za mkoa huo zinaonyesha  kati yao wasichana 138 ni kutoka wilaya ya Maswa ambao ni sawa na asilimia 57.7 ya wasichana walioolewa wakiwa na umri mdogo.

Serikali ya wilaya ya Maswa kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la World Vission Tanzania limeweza kuwaokoa wanafunzi wa kike wapatao 102 wakiwa wamepitia ndoa za utotoni.

Katika kupambana na  ndoa hizo  Shirika la World Vision Tanzania imebidi kuzindua  kampeni ya miaka mitano katika wilaya ya Maswa ijulikanayo ”Mahari kwa  mzazi kwa ndoa za utotoni si utajiri”.

Watoto wengine wa kike tayari wamezalishwa wakiwa na umri chini ya miaka 13 hivi sasa wanaanza maisha mapya ya kusoma.

Waathirika wanaeleza

Watoto wathirika Wanaeleza yaliyowasibu. Mmoja wa watoto waliokolewa akiwa amejitambulisha kwa jina la Esther Jidamabi mkazi wa kijiji cha Shishiyu ana miaka 13 na ni mama wa mtoto mmoja na amekubali kueleza kilichomsibu.

“Niliolewa kwa sababu wazazi wangu waliniambia sitaendelea kuwa mzigo kwao yaani kuwategemea wao katika maisha yangu hivyo niolewe ili nianzishe mji wangu niweze kujitegemea,” anasema Esther.

Wazazi na walezi wa watoto hawa wanalaumiwa kwa kuwalazimisha watoto wao kuingia katika ndoa za utotoni licha ya kukithiri kwa ndoa hizo pia imebainika kwamba asilimia 95 ya ndoa hizo hazidumu.

Hollo Khija mwenye umri wa miaka 14 ambaye aliolewa mwaka 2020 ni mama mwenye watoto wawili ambao ni mapacha ambaye ni mkazi wa kijiji cha Jihu ni mmoja wa waathirika wa ndoa hizi ambaye ndoa yake imevunjika.

“Nilidhani kuolewa ndio kutatatua matatizo yangu, kumbe nilijiongezea matatizo kwani mwanamume  aliyenioa kwanza alikuwa mkubwa kwangu kiumri na pili alikuwa mlevi wa kupindukia akinywa pombe za kienyeji kijijini hapa tunapoishi,” alisema Hollo.

Mmoja wa wasichana walioathirika na ndoa za utotoni akiwemo, Sara Dwese mwenye miaka 14 ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kadoto ambaye kwa sasa ni mfanyabiashara ya kuku amesema kuwa  tayari yuko katika janga la ndoa za Utotoni alisema kuwa wazazi wake walimtoa shuleni ili waolewe na waliona vigumu kurudi shule baada ya kuolewa.

Naye, Kwandu Jilala mkazi wa kijiji cha Ipililo mwenye umri wa miaka 14 alisema kuwa wasichana waliopata mimba au walioolewa mara nyingi walifukuzwa shule sera ya serikali ya Tanzania inaruhusu shule kuwafukuza au kukatisha masomo ya wanafunzi walioolewa au waliofanya kosa lililo kinyume cha maadili mema ambalo mara nyingi hujulikana kumaanisha kufanya ngono au kupata mimba kabla ya ndoa licha ya sasa wanafunzi waliopata ujauzito kuruhusiwa kuendelea na masomo baada ya kujifungua.

 Taus Said mkazi wa Maswa Mjini mwenye umri wa miaka 16 alisema kuwa wasichana ambao walijaribu au kukataa kuolewa walishambuliwa, walidhalilishwa kwa maneno au walifukuzwa nyumbani na familia zao ilawengine w alioshindwa kukwepa ndoa, wameeleza jinsi waume zao walivyowapiga na kuwabaka na hawakuwaruhusu kufanya uamuzi wowote
nyumbani.

Idadi kubwa ya wasichana hao  ambao niliongea nao walieleza kuwa waume zao waliwatelekeza na kuwaacha kuwatunza watoto bila msaada wowote wa kifedha sambamba na kupitia ukatili na unyanyasaji mikononi mwa wakwe zao.

“Mie nilikuwa nikijihisi mpweke kwa kutengwa na nilikuwa nalazimika kubaki nyumbani na majukumu ya mama wa nyumbani  na kulea watoto kwa sababu mwanamme hataki ujue mienendo yake.

“Kitu ambacho mara nyingi kinahusika na ndoa za utotoni pamoja na unyanyasaji wa kimwili wa maneno na kingono ambao wasichana walioolewa wanapitia ni  kukosa msaada pale wasichana wanapotafuta msaada kutoka kwa vyombo vya dola na familia”, alisema Shoma Jilala mkazi wa kijiji cha Badi.

Aliongeza kueleza kuwa  pamoja na shinikizo la kiuchumi na kitamaduni ambalo linazuia baadhi ya wasichana kuondoka kutoka kwenye ndoa zenye unyanyasaji  zina athari kubwa kwa afya ya kisaikolojia ya msichana.

Monica James(15) mkazi wa kijiji cha Shanwa ambaye ni mama wa watoto watatu ambaye kwa sasa anaishi na wazazi wake akijishughulisha na shughuli za kilimo  aliyezungumza bila masharti yoyote alisema kuwa hakuwa na furaha kwenye ndoa yake na anajuta kuolewa mapema na aliongeza kueleza awali alifikiria kujiua.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima.

Pia alisema kuwa hapa nchini hakuna nyumba za salama za kutosha ambapo wahanga wa ndoa za utotoni na wahanga wa unyanyasaji mwingine unaohusu ndoa za utotoni wanaweza kupata hifadhi na usalama.

Waliitupia lawama serikali kuwa hadi sasa haijafanya jitihada za kutosha kuwalinda watoto walio hatarini kuingia kwenye ndoa za utotoni na za kulazimishwa na kuwasaidia wahanga na msaada wa kisaikolojia, kijamii au kiuchumi ambao wanauhitaji sana.

Je wadau wanasemaje?

Hata hivyo, baadhi ya wadau mbalimbali wa maendeleo katika wilaya ya Maswa likiwemo Shirika la World Vision Tanzania ambao wanapigania haki za mtoto wa kike wanaulalamikia mfumo mzima wa kusimamia sheria kushughulikia masuala ya ndoa za utotoni kwa kutowachukulia hatua kali za kisheria watu wanaobainika kuwapa mimba watoto, wakidai kuwa ni kutokana na vitendo vya rushwa vilivyogubika vyombo vya sheria.

Meneja wa World Vision Kanda ya Nzega,Jaquline Kaihura ambaye anafanya kazi katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Tabora anasema kwa kutowachukulia hatua kali za kisheria watu wanaobainika kuwapa mimba watoto, wakidai kuwa ni kutokana na vitendo vya rushwa vilivyogubika vyombo vya sheria.

Amesema kuwa anaamini ili jamii ifanikiwe haina budi kusimamia usalama wa mtoto kwa manufaa ya kizazi kijacho.

Kaihura amesema kuwa  kwa kulitambua hilo wameamua kuungana na sekta nyingine ikiwamo Serikali kupambana na masuala yanayokatisha ndoto za watoto katika mkoa wa Simiyu hasa katika wilaya ya Maswa.

Kwa namna yoyote ile mtoto anastahili kusoma, kuwa na afya bora badala ya kukatishwa ndoto zake kwa kuolewa au kupata mtoto na yeye akiwa mtoto.

“Hii si haki inabidi ipigwe vita kila kona ya nchi na sisi kwa miaka hii mitano tutakuwa na kazi ya ziada kuhakikisha jamii inaelimika na kuona thamani ya mtoto hasa mtoto wa kike,” amesema.

Athari za Uzazi  na Afya kwa watoto chini ya Umri mdogo zikoje?

Zawadi Pima ni Muuguzi katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa kitengo cha Uzazi  amesema kuwa  matokeo mabaya ya uzazi kwa wasichana wenye umri mdogo na watoto wao ni  pale wasichana wanapojifungua, pamoja na vifo vya wajawazito, fistula, kujifungua kabla ya muda, utapiamlo na kupungukiwa damu na huduma za afya za kabla na baada ya kujifungua hususan kwenye maeneo ya hapa nchini hasa vijijini ni haba hivyo
kuongeza hatari.

Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Maswa, Grace Mmasi anaeleza athari mbalimbali zinazotokana na ndoa za utotoni ambazo ni pamoja na tofauti ya umri kwa ndoa za utotoni inaongeza athari ya maambukizo ya UKIMWI,hakuna msaada kwa wasichana walioathiriwa na ndoa za umri mdogo kwa sababu wengi wao hutengwa na ukosefu wa elimu.

Alisema kuwa mara nyingi ndoa za umri mdogo huwakumba wasichana wenye elimu ndogo au wasio na elimu kabisa na kuongeza kueleza kuwa ndoa za aina hii zimekithiri zaidi vijijini.

Ndoa za Utotoni kugeuzwa kitega Uchumi

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Simon Berege alisema Aina ya ndoa hizi zimeenea zaidi vijijini miongoni mwa familia maskini.

Alisema kuwa wakati mwingine wazazi huamini kwamba ndoa hizo zinawalinda wasichana, wengine huamini kuwa zinasaidia kulinda familia ya mhusika kwa kuipatia kipato kitokanacho na mahari; hata hivyo, wakati mwingine wasichana hawa hutumiwa kama bidhaa.

“Kwa wilaya hizi ndoa za utotoni zimekithiri sana katika maeneo ya vijiji na wazazi wengine huwageuza hawa watoto wao wa kike kama bidhaa wakiamini kuwa wakiwaozesha bado wakiwa na umri mdogo watapata mahari ambayo inaweza kubadili maisha yao na kuwa na kipato yaani matajiri maana watapewa ng’ombe na huku ukiwa na mifugo wewe inahesabika ni tajiri hivyo tunaendelea kuwaelisha ili kuondoa dhana hiyo,” alisema.

Kinachokwanisha haki kupatikana katika vyombo vya Sheria

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Maswa, Christian Rugumila alisema kesi zilizo nyingi ambazo zimekuwa zikifunguliwa katika mahakama hiyo zilizo nyingi zinaishia kufutwa kutokana na kutokuwepo kwa ushahidi wa kutosha wa kumtia mshitakiwa hatia na hii inatokana na upande wa wazazi wa msichana aliyeolewa kutotoa ushirikiano mahakamani na mtuhumiwa huachiwa huru.

Nini Kauli ya serikali ya wilaya juu ya tatizo hilo

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge alisema kuwa serikali imefanya maboresho muhimu ya kisheria na sera kwenye eneo la haki za binadamu za wasichana na wanawake kwa sasa sheria ya Makosa ya kujamiiana iliyopitishwa mwaka 1998 inaweka kubaka, utumikishwaji kingono wa watoto na ukeketaji wa wanawake kuwa makosa ya jinai na imeweka umri wa kuridhia tendo la ngono kuwa miaka 18.

Pia alisema kuwa Waraka wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia No 2 wa Mwaka 2021 unaeleza watoto wa kike walioacha shule kwa sababu za kupata Ujauzito watarudi shuleni kuendelea na masomo yao kupitia mfumo rasmi wa elimu.

 Kaminyoge alisema ipo haja ya  kuipitia upya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inaweka miaka 18 kuwa umri mdogo ambao wavulana wanaruhusiwa kuoa, lakini imeweka umri wa miaka 15 kwa wasichana kuolewa kwa ridhaa ya wazazi.

Alisema kuwa sheria zilizopo zinapingana na wakati mwigine haziko wazi zikishindwa kufafanua mtoto ni nani hivyo ni muhimu kupitia mapitio ya sheria ya ndoa ili kutoa ulinzi dhidi ya ndoa za utotoni.

“Wahanga wengine hawatoi taarifa  ya ndoa ya kulazimishwa na kunyanyaswa kwenye ndoa kwa sababu hawana imani na mfumo wa sheria na wanaogopa kulipiziwa kisasi kama wakiripoti familia zao au waume wao hili nalo ni changamoto kubwa katika kushughulikia suala la ndoa za utotoni,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,504FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles