24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAKALA: Dhana ya elimu bila malipo, utata kwa jamii

Na Janeth Mushi, Karatu

*Ruzuku haitoshelezi,kutofautiana kiwango

SERIKALI ilianzisha taratibu wa kutoa elimu ya awali,msingi na sekondari bila malipo,ambapo ililenga kuongeza wanafunzi shuleni hasa wanaotoka kwenye kaya maskini.

www.mtanzania.co.tz ambayo ilitembelea shule kadhaa za msingi na sekondari zilizopo wilayani Karatu, Arusha ambapo ilibaini kuna mwitikio mkubwa wa uandikishwaji wa wanafunzi ukilinganisha na kipindi cha nyuma,huku kukiwa na changamoto mbalimbali zinazokwamisha utekelezaji wa dhana hiyo.

Akizungumza na www.mtanzania.co.tz katika uchunguzi kuhusiana na masuala mbalimbali ya sera ya elimu bila malipo uliofanywa kwa msaada wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Arusha (APC) na Internews, Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Diego, Bashiru Mohamed, anasema udahili wa wanafunzi umeongezeka.

Anasema awali shule hiyo ilikuwa ya kwanza katika Kata ya Rhotia hivyo kuwa na wanafunzi wengi kutoka vijiji mbalimbali kabla ya shule nyingine kuanzishwa katika vijiji vya kata hiyo.

Mohamed anasema mwaka 2018 walijiunga wanafunzi 144, shuleni hapo,mwaka 2019 walijiunga wanafunzi 120, na mwaka jana walijiunga wanafunzi 134 na mwaka huu wamejiunga wanafunzi 121,ambapo hadi sasa ina jumla ya wanafunzi 445 na walimu 30, huku kukiwa na vyumba 12 vya madarasa.

“Maabara bado ipo kwenye hatua za ukamilishaji,hadi Julai mwaka huu tutakuwa tumekamilisha ujenzi kwani tumepata fedha serikalini Sh Milioni 30 na kwa sasa tunatumia chumba cha darasa kwa ajili ya wanafunzi kujifunza kwa vitendo.

“Hali ya mahudhurio ni mzuri kwa kiasi kwani kuna sababu nyingi ikiwemo upatikanaji wa chakula shuleni umechangia sana mahudhurio kuwa mazuri,elimu bila malipo limechangia kwani kwa sasa michango imepungua na mtoto harudishwi nyumbani kwa kudaiwa mahitaji mbalimbali,” anasema Mohamed.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Rhotia

Anabainisha kuwa chakula kinachangiwa na wazazi/walezi na kuwa wamejipanga kupitia kamati ya wazazi ambapo inaratibiwa na wazazi huku shule ikikagua utoaji na ubora wa chakula kabla wanafunzi hawajala.

“Kuhusu ruzuku zinazoletwa shuleni hazikidhi mahitaji ya shule kwa maana inakuja ya fidia ya ada na capitation ambazo ukiigawa unakuta fedha inayobaki haitoshi kuendesha shule,nadhani serikali iwe na kiwnago maalum kwa shule zote maana ruzuku huletwa kulingana na idadi ya wanafunzi kwani matumizi kama umeme haijalishi idadi ya wanafunzi,” anasema Mohamed.

Naye Mwalimu wa Fedha katika shule hiyo, Yoel Lukumay, anasema kwa mwezi wanapokea Sh milioni 1.153 kwa ajili ya fidia ya ada,ruzuku ya uendeshaji na posho ya Mkuu wa shule.

“Kwa mwezi fidia ya ada ni Sh 531,600 ambazo hutumika kwa ajili ya ukarabati wa majengo,samanikulipia mitihani ya mock,kulipa posho za walinzi ambapo hapa tunao wawili na tunawalipa kila mmoja Sh 110,000 kwa mwezi,kununua vifaa vya michezo,stationaries,kununua umeme,maji.

“Kati ya fedha hizo ruzuku ya uendeshaji ni Sh 398,555 imeelekezwa kwa ajili ya kununua kemikali za maabara,vifaa vya maabara vya kufudnishia na kujifunzia na posho ya madaraka 250,000 kwa ajili ya Mkuu wa shule ili ruzuku na fidia ya ada huja kwa wakati na ikitokea imechelewa na kuna jambo la dharura linatakiwa kufanywa tunakopa na tunakuja kuwalipa supplies baadae.

“Kiukweli fedha hazitoshelezi tunajikuta tunatembea na madeni,mfano maji bill inaweza kuwa kubwa,hivyo tunapunguza kila mwezi,” anasema Lukumay.

Wanafunzi Shule ya Sekondari Diego

Naye Mwalimu Mwandamizi wa taaluma shuleni hapo, Andrea Yona, anasema suala la taaluma kuna wakati kinapanda na wakati mwingine kinashuka.

“Mwaka 2016 ufaulu kidato cha nne ulikuwa asilimia 61.6,2017 asilimia 72.4,2018 kilishuka hadi asilimia 69.5,2019 asilimia 67.9 na mwaka jana kilipanda hadi kufikia asilimia 87.5.

“Elimu bila malipo inasaidia hasa wanaotoka katika kaya maskini maana kuna wengine walikuwa hawawezii kulipia baadhi ya gharama,inasaidia wanafunzi wanakaa shuleni,hivyo inasaidia kupandisha taaluma yake,” anasema Yona.

Kwa upande wao wanafunzi kutoka shuleni hapo, Theobald Baltazari, anayesoma kidato cha nne tahsusi ya PCB na Leah Mau,wanasema elimu bila malipo inasaidia hasa watoto wanaotoka katika kaya askini,kutokana na kupungua kwa michango.

“Wakati mwingine mzazi kama hajatoa hela ya chakula,wazazi huitwa kwenye vikao ila akiendelea kukaidi unakatazwa kula wakati wenzako wanakula hadi mzazi atakapolipa,”amesema Baltazari

SHULE YA MSINGI RHOTIA

Kwa upande wa Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Rhotia, Rose Lairumbe, anasema Shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 601 kati yao wavulana 298 na wasichana 303.

Anasema shule hiyo yenye walimu 16 pamoja na ina uhitaji wa vyumba vitatu vya madarasa kutokana na ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi ambapo kwa sasa wana vyumba 11 vya madarasa.

Anasema hali ya mahudhurio kwa wanafunzi inaridhisha tofauti na kipindi cha nyuma kabla ya sera ya elimu bila malipo na kuwa wanapata chakula shuleni na wazazi wamepata mwamko kuhusu elimu.

Rose anasema shule hiyo inapokea ruzuku kila mwezi Sh 704,937,ambapo kati ya hizo kitengo cha elimu maalum wanapata Sh 308,000,elimu bure Sh 232,900 na posho ya madaraka Sh 200,000 kwa Mwalimu Mkuu.

“Katika kitengo cha elimu maalum hizo fedha zinatumika kwa ajili ya chakula chao ambapo wako 13,na inayotolewa kwa ajili ya elimu bure hutumika kununua vifaa vya kufundishia,umitashumta imetengwa kwa ajili ya mashindano hayo,” anasema Rose.

Anaongeza kuwa licha ya fedha hizo kutolewa kwa wakati na serikali,bado haitoshelezi mahitaji katika shule ukilinganisha na mahitaji yaliyopo.

“Kuhusu chakula wanafunzi wanachangia mahindi kilo 20 na kilo 8 za maharage na Sh 3,500 kwa nusu muhula.Kiwango kimepanda ukiangalia 2019 ufaulu ulikuwa asilimia 90 na mwaka jana ulikuwa asilimia 87,” anasema Rose.

WAZAZI WAELEZA CHANGAMOTO

“Nashindwa kupambanua mahali elimu bila malipo, kutokana na michango tunayochangishwa,elimu bila malipo ingekuwa ni pale serikali inagharamia hadi chakula na mavazi.

“Michango iliyopungua ni ya madawati,majembe.Ili dhana ya elimu bila malipo iweze kueleweka Serikali ingesimamia kama ni bure kabisa kusiwe na michango yoyote,” hizo ni baadhi ya nukuu kutoka kwa moja ya wazazi ,akizungumzia changamoto za elimu bila malipo.

Wanafunzi Shule ya Sekondari Diego

Mzazi huyo mwenye watoto katika Shule ya Msingi Rhotia na Sekondari Diego anasema licha ya kuwa na michango ya chakula,wazazi wenye watoto wanaosoma madarasa yenye mitihani huchangishwa fedha kwa ajili ya masomo ya ziada.

Anasema kwa shule msingi mwanafunzi akiwa katika madarasa yenye mitihani(darasa la nne na saba)wazazi wanachangia Sh 2,500 kwa mwezi) na kwa shule ya sekondari huchangia Sh 7,000 kwa miezi sita kwa wanafunzi wa kidato cha nne.

“Kwa michango ya chakula kweli tunashirikishwa na kukusanywa na kamati ya wazazi na mimi ni moja ya wajumbe wa Kamati ya wazazi Shule ya Msingi Rhotia,na tuliamua walimu wasiwe wahusika bali kamati ya chakula au ya shule ndiyo inahusika na usimamizi,”anasema

“Michango msimamizi ni kamati iliyoundwa na wazazi lakini katika Shule ya Rhotia ni tofauti na walimu wapo,tulijaribu kuuliza kwa nini tusiwe na akaunti yetu lakini kamati ya shule imekataa hivyo michango yote hutumwa katika akaunti ya shule ambapo tunaona haijakaa sawa,”anaongeza.

“Shule ya Sekondari tulitaka kuwahoji kwani kuna bweni la wasichana wa kidato cha nne,kwa miezi sita tumechangishwa Sh 145,000 kwa kila mzazi mwenye mwanafunzi wa kike kwa chakula cha bweni,mahindi kilo 80 na maharage kilo 26,hatujapewa mchanganuo wa fedha zaidi,kwani licha ya fedha hizo kutumika kununua mavazi hatujajua matumizi mengine,”

Anasema kuhusu wanafunzi wa bweni shuleni hapo kamati ya chakula haihusiki na ukusanyaji wa fedha wala chakula na kuwa shule ndiyo inaratibu masuala yote. Anasema kwa wanafunzi wa madarasa mengine wazai na walezi huchangia kilo 36 za mahindi,kilo 13 za maharage na Sh 25,000 kwa nusu muhula.\

Naye mzazi mwingine kutoka Kata hiyo ya Rhiria,anasema licha ya kushirikishwa katika vikao vya maamuzi kuhusu chakula cha watoto, wazazi ambao huchelewa kulipa fedha hizo kwa wakati huhamasishwa na wasipotoa kabisa huitwa kwa Mtendaji kwa hatua za kisheria.

MWONGOZO ULIOTOLEWA

Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia pamoja na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),walitoa mwongozo ambao ulikua unaainisha utoaji wa elimumsingi bila malipo.

Serikali kupitia Waraka wa Elimu No 5 wa mwaka 2014,iliamua kutoa elimumsingi(kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne), bila malipo lengo la serikali ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014,ambayo ililenga kuhakikisha watoto wote wa kitanzania wanapata elimu bila kikwazo chochote ikiwemo ada au michango.

Ili kutekeleza elimumsingi bila malipo nyaraka na miongozi mbalimbali ilitolewa ikiwemo mwongozo wa matumizi ya fedha za ruzuku ya uendeshaji (Capitation Grant) kwa shule za serikali.

Kupitia waraka wa elimu namba 3 wa mwaka 2016 kuhusu utekelezaji wa elimu msingi bila malipo uliotolewa Mei 25,2016 ukiwa na Kumb.Na. ED/OKE/NE/Vol.1/01/71, uliainisha masuala kadhaa kuhusu dhana ya elimu bila malipo.

Kupitia waraka huo unafafanua kuwa utoaji wa elimumsingi bila malipo una maana kwamba mwanafunzi atasoma bila mzazi/mlezi kulipa ada wala michango ya fedha iliyokuwa ikitozwa shuleni kabla ya kutolewa kwa Waraka wa Elimu namba 5 wa mwaka 2015.

Pamoja na masuala mengine katika mwongozo huo kulibainishwa majukumu yanayotakiwa kufanywa na wizara hiyo, TAMISEMI,Ofisi ya Mkuu wa mkoa,wilaya,Wakurugenzi wa Wilaya,Miji,Manispaa na Majiji,wakuu wa shule za serikali,kamati/bodi za shule za serikali,walimu,wanafunzi na wazazi/walezi.

Tamisemi ilikuwa na majukumu ya kutoa mwongozo wa wa matumizi ya fedha za umma kwa wakuu wa shule,kuratibu uandaaji wa mipango na bajeti ili kupata mipango na bajeti ya taifa kila mwaka inayozingatia mahitaji halisi ya elimumsingi bila malipo.

Majukumu ya wazazi na walezi ni pamoja na kununua sare za shule,michezo,vifaa vya kujifunzia vikiwemo madaftari na kalamu,kushirikiana na uongozi wa shule kuweka utaratibu wa kutoa chakula cha mchana kwa shule za kutwa na zenye hosteli kulingana na mazingira yao.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Rhotia

Kupita waraka huo ambao ulianza rasmi kutumika Juni mosi 2016, Wizara inazitaka kamati au bodi za shule kusimamia matumizi ya fedha zinazotolewa na serikali ili ziweze kutoa tija,kuhakikisha sera,nyaraka na miongozo ya serikali inazingatiwa.

Kwa upande wa wakurugenzi wa halamshauri wanatakiwa kuandaa mipango na bajeti kila mwaka inayozingatia mahitaji ya elimumsingi bila malipo.

Wanafunzi ambazo ndiyo walengwa wakuu wa utoaji elimu wametakiwa kuhakikisha wanakuwepo shule katika kipindi chote cha masomo huku walimu kazi yao kubwa ikiwa ni kusimamia sera na miongozo ya utoaji elimu bila malipo.

TAMISEMI

Hivi karibuni mjini Dodom,Naibu Waziri wa Tamisemi, David Silinde,amenukuliwa akisema serikali kupitia Waraka wa elimu no 5 ya mwaka 2015,iliamua kutoa Elimumsingi bila malipo kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne.

Sìlinde amesema Serikali ilitia waraka wa Elimu namba 3 wa mwaka 2016 kuhusu utekelezaji wa elimumsingi bila malipo.

“Hii sio elimu bure ni elimu bila ada,na wakara umezungumza na kuainisha wajibu wa serikali na wananchi ambapo wananchi wajibu wao ni pamoja na kushiriku katika miradi ya maendeleo ya kiserikali kama kujenga miundombinu ikiwemo madarasa,”

Naibu huyo alikua akijibu swlai la Mbunge wa Nkasi Kaskazini,Aida Khenani (Chadema), aliyekua akihoji kwanini wazazi wanachangishwa wakati serikali inasema elimu ni bure.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles