Na Nora Damian, Mtanzania Digital
“Wakati mwingine tunapata shida tukihitaji wakalimani utakuta mwingine anakutajia bei kubwa, mwingine anakuambia nitakufanyia kirafiki utanipa hela ya soda, mwingine anaweza kukuambia umpe shilingi elfu arobaini au elfu hamsini inategemea,” anasema Joyce Jumbe mwenye ulemavu wa uziwi.
Kutokana na hali yake ya uziwi ili aweze kuwasiliana na watu wakati wote anahitaji mkalimani wa lugha ya alama, hii ni pamoja na huduma ya hospitali, mafunzo, usaili na pengine hata atakapotaka kununua kitu dukani. Hata hivyo kumlipa mkalimani wakati wote ni gharama kubwa kwake.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Joyce (31) ambaye anaishi na hali ya uziwi kwa miaka 17 sasa, aliamua kumfundisha mdogo wake Veronica Jumbe lugha ya alama ili amsadie kutafsiri anapofanya shughuli zake mbalimbali.
“Usimuone hivyo ana kichwa chepesi (yaani mdogo wake), nilimfundisha kwa muda mfupi lakini ameweza kuelewa na anapenda ukalimani wa lugha ya alama,” anasema Joyce kwa lugha ya alama huku Veronica akitasiri wakati wa mahojiano na mwandishi wa makala haya.
Anasema hivi sasa mdogo wake anafahamu namna ya kutumia lugha ya alama na kwa kiasi kikubwa amekuwa akimsaidia na kuokoa gharama ambazo angeweza kuzitumia endapo angemlipa mkalimani.
“Mimi napenda wanavyoongea na dada Joy amenifundisha siku hizi najua namsaidia,” anasema Veronika anayesoma kidato cha pili Shule ya Sokondari Mzinga.
Veronica anasema anajivunia dada yake ambaye ni mpambanaji kwani anafanya shughuli mbalimbali za kumuingizia kipato.
Joyce mkazi wa Keko alyezaliwa bila uziwi, alipata tatizo hilo alipofika kidato cha pili. Anasema lilianza tatizo la macho kisha likaja la kutosikia hali iliyomlazimu kusimama masomo kwa mwaka mmoja ili kupata matibabu.
“Nilikuwa nasikia vizuri lakini nilivyofika ‘form two’ nilipata hitilafu ya macho ilikuwa ni ghafla, nikapelekwa Hospitali ya Mkoa Rukwa ambako nako nilipewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa Mbeya.
“Nilisimama shule mwaka mzima ikabidi mwaka 2005 nirudie ‘form two’…tatizo la masikio nalo likaanza wakaniambia niendelee kusoma nikimaliza ndiyo nikatibiwe,” anasema Joyce.
Anasema baada ya kuhitimu kidato cha nne alijiunga na Shule ya Sekondari ya Loleza iliyoko Mbeya kwa masomo ya kidato cha tano na sita katika Tahasusi ya HGL (Historia, Jografia na Lugha).
Aidha baada ya kuhitimu kidato cha sita alijiunga na Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU) Tawi la Dar es Salaam kwa masomo ya Shahada ya Sayansi ya Jamii na Uongozi ambapo alijikuta akiwa mwanafunzi pekee mwenye uziwi.
“Nilipokuwa nasoma KIU nilijikuta niko peke yangu ambaye sisikii baadhi ya wanafunzi wenzangu wakawa wananitenga hawanielewi. Jamii inayokuzunguka wakati mwingine hawakuelewi wanakuona mtu wa ajabu unadharauliwa, pengine anakusalimia hujasikia,” anasema Joyce.
Joyce anasema darasani alikuwa hamsikii mwalimu anapofundisha hivyo alimtafuta mwalimu na kumlipa gharama za ziada huku akijifunza pia kwa kupitia ‘notsi’ na kuingia maktaba.
DAKTARI ANASEMAJE?
Daktari Bingwa wa macho kutoka Hospitali ya Kairuki, Mustapha Yusufali, anasema kuna uhusiano baina ya magonjwa ya macho na tatizo la kutosikia ambalo husababishwa na mshipa wa jicho kuchoka kutokana na upungufu wa vitamin kwenye mwili.
“Tatizo linaweza likaanza kwenye jicho au masikio kwasababu mara nyingi huwa ni upungufu wa vitamin mbalimbali. Mtu akiwahi tatizo hili linatibika na huwa tunawapatia Multi-vitamin (vitamin mchanganyiko) na folic acid (asidi ya folic) kuepuka chochote kitakachotokea.
“Kwa upande wa macho mtu huwa anapona lakini sikio siwezi kujua kwa sababu sisi tukishatibu macho tukimaliza tunawaachia wenzetu wa masikio,” anasema Dk. Yusufali.
Anasema pia presha ya macho kwa kiasi kikubwa ni ugonjwa wa kurithi na ikizidi sana mtu huweza kuumwa kichwa mara kwa mara, kutokwa na machozi mengi na kuathiri mshipa wa kuonea.
“Presha ya macho maana yake ni maji ndani ya jicho hayapati mlango wa kutosha wa kutoka nje na kuongeza presha ndani ya jicho. Huu ni ugonjwa wa kurithi na Waafrika ndiyo wenye shida kubwa, tiba yake ni kufanyiwa upasuaji, kuvaa miwani au kutumia dawa kwa maisha yote,” anasema Dk. Yusufali.
Anasema presha ya jicho ikiwa kubwa mtu husika huanza kupoteza kuona pembeni na mwisho inakuwa katikati hivyo ni vigumu kugundua kwamba haoni.
Joyce anasema anapenda kusaidia wahitaji, wasiojiweza na wenye ulemavu ndiyo maana akasomea ustawi wa jamii, hata hivyo anaona lengo lake linatimia kwa sababu anafanya kazi za kujitolea. Kwa sasa binti huyu anafanya kazi ya kujitolea katika Taasisi ya Kusaidia Vijana Wenye Ulemavu (YOWIDO).
“Ukipata matatizo ukubwani unakuwa kama umeathirika kisaikolojia, nimekata tamaa mara nyingi lakini wazazi wangu wameendelea kunipigania, wanajinyima wananijali nisome, sijapata kazi lakini nikikwama wananisaidia,” anasema Joyce
WAZAZI
Mama mzazi wa Joyce, Mabile Mpanduzi, anasema mwanawe alikuwa mzima akisikia vizuri na kila kiungo kilikuwa kizuri lakini alipofika kidato cha pili ndipo alipoanza kupata matatizo.
“Tatizo lilitokea ghafla walimu wakatuambia tumchukue tumpeleke hospitali, tulipompeleka Mbeya wakasema amepata presha ya macho. Akaambiwa awe anakula vyakula vya Vitamin ‘A’ halafu akapewa vidonge na miwani.
“Lakini Joy ni mtoto ambaye alikuwa na imani na Mungu alikataa ile miwani akasema Mungu aliyempa macho hatomuacha apofuke…siku moja akaniita akaniambia mama naona. Nakutia moyo wewe mwenye tatizo la kusikia, kuona fanya bidii lakini mtegemee Mungu,” anasema Mabile.
Kwa upande wake baba wa Joyce, Abraham Sanga, anasema watoto wenye ulemavu si mzigo kama baadhi ya jamii inavyodhani kwani wakiendelezwa wanaweza kujisaidia wenyewe na hata kusaidia familia.
KINACHOENDELEA UDOM
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Idara ya Tiba kwa Jamii kimebuni teknolojia itakayorahisisha mawasiliano kwa viziwi ambayo ina uwezo wa kubadilisha sauti ya kawaida au maandishi na kwenda katika lugha ya alama.
Mhadhiri wa Idara ya Tiba kwa Jamii kutoka Udom, Deogratius Bintabara, anasema teknolojia hiyo ambayo iko kwenye hatua za awali inatarajiwa kuanza kujaribiwa Desemba mwaka huu katika vituo vya kutolea huduma za afya.
“Mtu anaweza kuamua kuandika au kuzungumza kisha ikatafsiri maneno kwa lugha ya alama au akitoa ishara ya lugha ya alama itabadilisha kwenda kwenye lugha ya kawaida,” anasema Bintabara.