NA FARAJA MASINDE, DAR ES SALAAM
MWILI wa Mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Dk. Emmanuel Makaidi aliyefariki dunia juzi kwa shinikizo la damu unatarajiwa kuzikwa wiki ijayo.
Taarifa ambazo gazeti hili limezipata kutoka ndani ya familia ya marehemu Makaidi, zinaeleza kuwa atazikwa kati ya Jumatatu au Jumanne.
Mke wa marehemu, Modesta Makaidi ambaye jana jioni alikuwa njiani kuelekea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuupeleka mwili wa marehemu, aliliambia gazeti hili kuwa taratibu za mazishi zinatarajiwa kufanyika kati ya Oktoba 20, mwaka huu nyumbani kwake Sinza.
Awali MTANZANIA Jumamosi ambalo lilifika nyumbani kwa marehemu, Sinza, Dar es Salaam lilizungumza na mtoto mkubwa wa marehemu aitwae Hilda Makaidi ambaye alisema taratibu za mazishi zitatangazwa mara baada ya mwili wa marehemu kuwasili nyumbani kwake Dar es Salaam.
“Mwili wa marehemu baba unatarajiwa kusafirishwa kuanzia leo jioni (jana), hivyo tunatarajia utawasili kesho alfajiri (leo) na ukishawasili ndipo hapo taratibu za mazishi zitakapofahamika baada ya wanafamilia kukaa kikao japo tunatarajia yatakuwa Jumatatu au Jumanne,” alisema Hilda.
Alisema mbali na kuusubiri mwili huo, pia wanawasubiri wasemaji wa familia ambao mmoja atasafiri na mwili kutoka mkoani Mtwara na mtoto mwingine wa marehemu Makaidi ambaye alikuwa akitarajiwa kuwasili jana jioni akitokea mkoani Arusha.
Wakati huo huo, Chama cha National League For Democratic (NLD), ambacho marehemu alikuwa akikiongoza kimetangaza siku saba za maombolezo kuanzia leo kutokana na kifo cha mwasisi wake huyo.
Taarifa hiyo ilitolewa jana nyumbani kwa marehemu Sinza jijini Dar es Salaam, kupitia kwa Katibu Mwenezi wa NLD Taifa ambaye pia ni msemaji wa chama hicho, Khamis Hamadi.
Alisema kufuatia kifo cha Dk. Makaidi, bendera za chama hicho kote nchini zitapepea nusu mlingoti kwa muda wa siku saba za maombolezo.
“Tumeondokewa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama, hivyo bendera za NLD zitapepea kwa nusu mlingoti kwa muda wa siku saba kuanzia kesho (leo) nchi nzima kama ishara ya maombolezo,” alisema Hamad.
Kuhusiana na taratibu za mazishi alisema msiba huo unahusisha pande tatu ambazo ni familia, chama pamoja na Ukawa hivyo wanasubiri taratibu hizo kukamilika mara baada ya familia kutoa tamko rasmi.
“Taratibu za mazishi bado hatujazipanga kwasababu msiba huu unahusisha pande tatu ambazo ni familia, chama na Ukawa, hivyo mpaka pande zote hizo zikubaliane kisha taarifa itatolewa na kufikia mapema wiki ijayo ufumbuzi utakuwa umekwishapatikana.
“Kama inavyofahamika, Makaidi alikuwa ni miongoni mwa viongozi ambao vyama vyao vinaunda Ukawa, tunatarajia hata eneo la mazishi linaweza lisiwe hapa kutokana na wingi wa waombolezaji, hii ni kutokana na umoja huo kuwa na wafuasi wengi,” alisema Hamad.
Kwa upande mmoja wa wenyeviti wa Ukawa, Freeman Mbowe, alisema msiba huo umewashtua sana na wao kama Ukawa walikuwa wakijipanga kuona namna ambavyo watashiriki.
“Makaidi ameondoka katika kipindi muhimu mno, ukizingatia huu ni wakati wa uchaguzi na alikuwa mmoja kati ya viongozi shupavu wa Ukawa, hivyo tutashiriki kwa sababu huu ni msiba na hauangalii itikadi za vyama,” alisema Mbowe.
JK amlilia
Rais Jakaya Kikwete, naye alituma salamu za rambirambi kwa Chama cha NLD, akieleza namna alivyoguswa na msiba huo.
Rais Kikwete alimuelezea marehemu kuwa alikuwa kiongozi shupavu na mhimili mkubwa kwa chama chake na Taifa hasa katika nyanja ya siasa.
“Nimepokea kwa huzuni na masikitiko taarifa za kifo cha Mwenyekiti wetu wa NLD, Mheshimiwa Emmanuel Makaidi…NLD imepoteza mhimili wake. Taifa letu pia limepoteza kiongozi mzuri na shupavu wa siasa katika kipindi ambacho alihitajika zaidi kuliko wakati mwingine wowote,” alisema Rais Kikwete.
Alisema Makaidi kwa kipindi chote cha uongozi wake, alionyesha uongozi wa hali ya juu na uzalendo kwa taifa lake.
“Wakati wote wa maisha yake ameonyesha uongozi wa hali ya juu na uzalendo kwa nchi yake tokea alipokuwa kiongozi hodari wa michezo hadi alipolitumikia taifa letu kama Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba,” alisema Rais Kikwete.
“Naungana nanyi katika maombolezo na pia nawaombeni mnifikishieni pole zangu nyingi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Dk. Makaidi kwa kuondokewa na mhimili wa familia na rafiki mzuri. Aidha, naungana nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi roho ya marehemu Dk. Emmanuel Makaidi,” alisema Rais Kikwete.
Dk. Makaidi ambaye alikuwa akigombea ubunge katika Jimbo la Masasi mkoani Mtwara kupitia Chama cha NLD, alifariki dunia juzi saa 7:15 mchana katika Hospitali ya Nyangao, mkoani Lindi alikokuwa akitibiwa.