24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

MAJINA 21 WAVUVI HARAMU  YAKABIDHIWA POLISI

NA CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM



MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi, amemkabidhi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Suzan Kaganda, orodha ya majina ya watu 21 wanaojihusisha na uvuvi haramu.


Hapi alikabidhi orodha hiyo jana wakati akizindua kampeni maalumu ya mapambano dhidi ya wavuvi haramu sambamba na uchomaji zana zisizofaa zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 60.


Akizungumza katika shughuli ya uchomaji zana hizo katika ziara aliyoifanya jana katika Kata ya Mbweni, Hapi alisema katika orodha hiyo pia wamo viongozi wawili ambao hakutaja majina wala vyeo vyao.


"Leo nimezindua kampeni maalumu ya kupambana na uvuvi haramu, ninakabidhi majina haya kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili wafanye uchunguzi na wakibainika kuhusika kwa namna moja ama nyingine, hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao," alisema Hapi.


Katika orodha hiyo, mkuu huyo wa wilaya alisema anafahamu vinara wa matukio hayo wana nguvu kubwa lakini Serikali imedhamiria kupambana na kutokomeza vitendo hivyo.


Alisema wavuvi haramu wamekuwa wakitumia milipuko ambayo ni hatari na kama haitazuiliwa, inaweza ikachangia kujitokeza kwa matukio ya kihalifu pamoja na ugaidi.


"Sheria ya uvuvi inatamka wazi aina ya uvuvi na vipimo vya nyavu vinavyotakiwa, hivyo ni wajibu wa kila mtu kuzingatia sheria zilizopo," alisema.


Alisema wameshuhudia matukio mbalimbali yanayojitokeza kwa sababu ya uvuvi haramu ikiwamo watumiaji wa zana hizo kukatika mikono na miguu, hivyo ipo haja ya kila mwananchi kuwafichua watu wanaojihusisha na uvuvi haramu.


"Wanaowafahamu wavuvi haramu walete majina ofisini kwangu hata kama wapo wanaowafadhili na kushiriki, ninaahidi tutawashughulikia hawa wote kwa mujibu wa sheria,” alisema Hapi.


Kwa upande wake, Ofisa Uvuvi Wilaya ya Kinondoni, Grace Kakama, alisema vifaa hivyo asilimia 80 vimekamatwa maeneo ya Kawe na Kunduchi. 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles