Na NORA DAMIAN
DAR ES SALAAM
SERIKALI za Tanzania na Misri zimekubaliana kuendelea na mazungumzo ya kuhakikisha matumizi ya Mto Nile ambayo chanzo chake ni Ziwa Victoria, kwa kuhakikisha yanazifaidisha nchi zote zinazotakiwa kupata maji hayo.
Maji hayo ya Ziwa Victoria ambayo mbali na kutumiwa na Mkoa wa Mwanza na Shinyanga kupitia mradi wa Iherere sasa yanasambazwa katika Mkoa wa Tabora, jambo ambalo litasaidia kuondoa adha ya maji kwa wananchi wa maeneo hayo.
Makubaliano hayo yalifikiwa jana wakati wa mazungumzo baina ya Rais Dk. John Magufuli na mwenzake wa Misri, Abdel Fattah Al Sisi, ambaye aliwasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.
Akizungumza baada ya mazungumzo ya siri yaliyochukua zaidi ya saa tatu Rais Magufuli alisema suala la maji ya Mto Nile wamekubaliana mazungumzo bado yaendelee ili kuweza kutafuta ufumbuzi wa kudumu kati ya pande zote mbili.
Hata hivyo Rais Magufuli hakuweka wazi mazungumzo yao yalijikita katika maeneo gani na iwapo kulikua na mvutano au laa kuhusu matumizi ya maji hayo, zaidi ya kueleza kuwa wamekubaliana kuendelea na mazungumzo.
“Ziara yake imezaa matunda mazuri na utekelezaji wake ukifanyika vizuri mafanikio makubwa ya kiuchumi yatapatikana. Tutaendelea na mazungumzo na kuzihusisha nchi mbalimbali zinazotumia Mto Nile ili ziweze kunufaika na mto huo,” alisema.
Alisema pia wamesaini makubaliano mengine ya kuisaidia Tanzania katika sekta za viwanda, kilimo, afya, utalii, ulinzi na elimu.
Katika makubaliano hayo nchi ya Misri itaanzisha kiwanda kikubwa cha nyama ili mifugo ichinjwe nchini na nyama isafirishwe Misri na nchi nyingine.
Pia nchi hiyo itatuma wataalamu na wawekezaji kwa ajili ya kuja kujenga kiwanda cha dawa kwa sababu nchi hiyo ni miongoni mwa nchi zinazotengeneza dawa zenye ubora na zinazouzwa kwa gharama nafuu.
Rais Magufuli alisema Serikali ya Misri imeahidi kuongeza fedha kuhakikisha Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) inafanya upasuaji wa figo kabla ya mwaka 2020.
Kuhusu sekta ya utalii, alisema wamekubaliana kubadilishana uzoefu ili kusaidia kuendeleza sekta hiyo.
Kwa upande wa sekta ya elimu alisema Misri itaongeza idadi ya wanafunzi wanaosoma nchini humo kutoka 115 wa sasa na kwamba Tanzania itatoa walimu wa Kiswahili wakafundishe katika vyuo mbalimbali nchini humo.
“Na wao wamekubali kutuletea walimu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, sayansi,lugha ya kiarabu na dini ili kufundisha katika vyuo vyetu,” alisema.
Rais Dk. Magufuli alisema mbali na hilo pia wamekubaliana kushirikiana katika mapambano dhidi ya rushwa kwa sababu inaweza kuwa chanzo cha saratani katika ushirikiano wan chi hizo mbili.
Awali akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Misri Abdel Fattah Al Sisi, alisema wataendelea kujenga uwezo na kubadilishana wataalamu katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Mahusiano kati ya Tanzania na Misri ni mfano wa kuigwa kwa muda mrefu kupitia Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwl Julius Nyerere na mwenzake Gamal Abdi Nasser (wa Misri )na kumekuwa na ushirika kati ya mataifa haya ambayo yameunganishwa na Mto Nile.
“Tuna matumaini makubwa ya kuwa na maendeleo endelevu, kukuza biashara na kuongeza uwekezaji,” alisema Al Sisi.
Pamoja na hali hiyo alimpongeza Rais Dk. Magufuli kwa jitihada zake za kupambana na rushwa na ufisadi na kwamba ameonyesha mfano wa uongozi mzuri kwa nchi za Afrika.
“Tutaendelea na mashauriano ya kuleta amani na utengamano katika Bara la Afrika na kuwa na msimamo mmoja katika masuala yanayohusu nchi zetu,” alisema.
Hadi sasa uwekezaji wa Misri nchini ni Dola za Marekani milioni 887 ambao umeajiri watu 959.
Alisema pamoja na hali hiyo bado Misroi itaendelea kuwa na uhusiano mzuri na Tanzania kwa kuhakikisha wananchi wa nchi zote mbili wananufaika kwa kupata maendeleo.
Rais huyo anatarajiwa kuondoka nchini leo kuelekea Rwanda.