24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Maji Marefu afunguka ukwepaji kodi

1NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani (CCM), amesema hajawahi kukwepa kodi na wala hatarajii kufanya hivyo kwa kuwa anajua umuhimu wake.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Ngonyani ambaye ni maarufu kwa jina la Profesa Maji Marefu, alisema yeyote anayemtuhumu kuwa ni mkwepa kodi, anataka kumchonganisha na Serikali katika kipindi hiki ambacho Rais Dk. John Magufuli anahimiza wananchi kulipa kodi.

Profesa Maji Marefu alitoa kauli hiyo baada ya chombo kimoja cha habari kuripoti, kwamba anamiliki gari la kifahari lenye thamani ya Sh milioni 300 ambalo hakulilipia kodi.

“Kuna gazeti moja limeandika nimekwepa kodi ya gari langu la kifahari ninalolimiliki kwa sasa. Nimesikitishwa na habari hiyo kwa sababu gari hilo nililinunua kwa shilingi milioni 173.612, nikalilipia kodi ya shilingi milioni 69.3, nikalilipia bima ya shilingi milioni 8.5 na kisha nikalilipia namba maalumu za jina langu la Maji Marefu kwa gharama ya shilingi milioni tano.

“Kabla ya kulipia namba maalumu, awali gari hilo aina ya Land Cruiser Super Challenger lilikuwa na namba T 666 DFS ambazo nilikuwa nimezilipia bila kukwepa kodi.

“Sasa inapotokea mtu anasema namiliki gari ambalo nimekwepa kulilipia kodi, naumia kwa sababu naonewa bila sababu za msingi.

“Kwahiyo, nitalifikisha suala hili mahakamani ili wanaosema nilikwepa kodi, waje na ushahidi wao na mimi nitapeleka ushahidi wangu wa nyaraka zote nilizonazo.

“Kimsingi nchi lazima ikusanye kodi na kodi inapokusanywa haiangalii huyu ni Maji Marefu au huyu ni nani, lazima kodi ikusanywe ili hatimaye mwakani watoto wasome bure kama alivyoagiza Rais Magufuli,” alisema Profesa Maji Marefu.

Akizungumzia utendaji kazi wa Rais Magufuli, mbunge huyo alisema anamuunga mkono kwa kuwa anaonekana kurejesha heshima ya Chama Cha Mapinduzi iliyokuwa imepotea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles