John Stephen, Dar es Salaam
Majeruhi wa ajali ya moto iliyotokea mkoani Morogoro baada ya lori la mafuta kuanguka, wamepokelewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
Majeruhi hao wamepokelewa jana Jumamosi Agosti 10 kuanzia saa 4:30 usiku hadi saa 5:10 ambapo gari la kwanza la wagonjwa lilingia Muhimbili saa 4:30 usiku na kufuatiwa na magari manne yaliyoingia saa 5:10 usiku na ilipofika saa 6:30 tayari wagonjwa 25 walikuwa wamepokelewa na kuanza kupatiwa matibabu na wataalamu mbalimbali hospitalini hapo.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha amesema baada ya kutokea kwa ajali hiyo, MNH ilituma wataalamu mbalimbali kwa ajili ya kuongeza nguvu wakiwamo madaktari bingwa wa magonjwa ya dharura, Dk. Juma Mfinanga.
Amesema Muhimbili imetuma wataalamu wa upasuaji kwa wagonjwa walioungua moto, madaktari bingwa wa upasuaji na madaktari bingwa wa usingizi ili kushirikiana na wataalamu wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kutoa huduma kwa majeruhi pamoja na kufanya uchunguzi kwa wagonjwa wanaopaswa kuhamishiwa MNH.
“Kwa upande wetu, tumeandaa madaktari 28, wauguzi 64 na wahudumu wa kawaida 10. Pia, tumeandaa vitanda 89 na kati ya hivyo vitanda 21 ni vya wagonjwa watakaohitaji uangalizi maalumu,” amesema Aligaesha.
Mbali na maandalizi haya, vile vile MNH imeandaa dawa za kutosha vikiwamo vitendanishi vyote vinavyohitajika kuhudumia majeruhi ambao wameanza kupatiwa huduma mbalimbali za matibabu.
Ajali hiyo ilitokea jana eneo la Msamvu mkoani Morogoro baada ya lori la mafuta kuanguka na kulipuka na kusababisha vifo watu zaidi ya 60 na majeruhi 70.