Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Wakati majaribio ya treni ya mwendokasi inayotumia umeme kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro yakianza Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema limejiridhisha mifumo waliyoijenga inafanya kazi.
Kipande hicho cha kilomita 300 kilianza kujengwa Mei 2,2017 na hadi sasa ujenzi umefikia zaidi ya asilimia 98.
Akizungumza leo Februari 26,2024 wakati wa majaribio hayo Mkurugenzi wa TRC, Masanja Kadogosa, amesema wamejiridhisha bila mashaka kwamba mifumo waliyoijenga inafanya kazi.
“Tunaelekea katika hatua ya kuanza rasmi, hii ni hatua muhimu katika kutekeleza maagizo ya mheshimiwa rais kwamba mpaka mwishoni mwa mwezi wa saba tuwe tumeshaanza kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma.
“Safari ya leo sehemu kubwa vichwa vya treni ndio vilikuwa vinafanyiwa majaribio, tunafunga pia mabehewa, tutakuwa na mabehewa 14 lakini kwa kuanzia tunayo manne, mawili ya ‘business class’ na mawili ya ‘economy class’,” amesema Kadogosa.
Amesema ujenzi wa reli hiyo unahusisha vitu vingi ndio maana wamekuwa wakifanya majaribio ya mara kwa mara yakiwemo ya mawasiliano ya umeme na mifumo mbalimbali ya uendeshaji ili kujihakikishia usalama kabla ya kuanza rasmi.
Aidha amesema vipande vingine vya Morogoro – Makutupora, Makutupora – Tabora, Tabora – Isaka, Isaka – Mwanza vinaendelea na hivi karibuni watasaini mkataba wa Uvinza – Msangati kuunganisha na Burundi kisha hadi Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC).
“Kipande cha Morogoro mpaka Dodoma tunamalizia kufanya majaribio ya transfoma, tunatarajia wiki ya kwanza au ya pili ya mwezi Machi Tanesco wataanza kuingiza umeme, tukishajiridhidha kwamba tuko salama tutakuwa na treni nyingine ya kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma,” amesema Kadogosa.
Mkurugenzi huyo amesema wanaendelea kupokea vifaa mbalimbali kila mwezi hadi itakapofika Desemba ambapo wanataraji kupokea vichwa 17.
Kwa mujibu wa Kadogosa, mwishoni mwa Machi watapokea kichwa cha kuchongoka na mabehewa matano.
Amewatoa hofu Watanzania kuhusu upatikanaji wa umeme kwani kuna njia za umeme zinazojitegemea kwa ajili ya reli hiyo na ambazo haziingiliani na vitu vingine.
“Tuna ‘transmission line’ ambazo ni za kwetu tu, hatuingiliani na mtu yeyote na treni yetu inafua umeme yenyewe ndiyo maana hatuhitaji umeme mwingi,” amesema Kadogosa.
Kuhusu bei za nauli amesema walishapeleka mapendekezo katika Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ambayo yanaendelea kufanyiwa kazi hivyo utakapofika muda wa kuanza safari zitakuwa tayari.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano TRC, Jamila Mbarouk, amesema nchi mbalimbali zimenza kuja kujifunza katika sekta ya miundombinu ya reli na kuwataka Watanzania kuendelea kuiamini Serikali.
“Kinachoendelea ni mwendelezo wa majaribio katika njia ya reli, mifumo ya reli na vifaa tutakavyovitumia ambavyo ni treni. Watanzania wanatakiwa wajivunie kwa sababu kwa Afrika Mashariki sisi ndio tumeanza kufungua njia kwa kutembeza treni ya mwendokasi inayotumia umeme,” amesema Jamila.
Mkazi wa Kihonda ambaye alishushudia treni hiyo ikiwasili Morogoro, Peter Mwikalo, amesema kuanza kwa majaribio hayo ni dalili nzuri kwamba maagizo ya rais yanafanyiwa kazi.
“Tangu mradi uanze nimekuwa nikiona unavyoendelea mpaka hapa ulipofikia, niliona kama kitu cha kawaida lakini umekamilika…ni maajabu makubwa kwenda Dar es Salaam ni kama vile umepanda ndege. Nampongeza Rais Samia kwa kuupokea mradi huu na kuhakikisha unakamilika kama ilivyopangwa,” amesema Mwikalo.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, amesema majaribio hayo ni uthibitisho kwamba safari za treni kati ya Dar es Salaam – Dodoma zitaanza Julai kama ilivyoelekezwa na Serikali.
“Watanzania tuna kila sababu ya kujivunia mafanikio haya ambayo ni sehemu ya mafanikio makubwa katika nchi yetu yanayotokana na miradi mikubwa ya kimkakati,” amesema Matinyi.