Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM
KUNDI la vijana wanaodaiwa kuwa majambazi, wamevamia maduka katika eneo la Msewe, Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam na kupora.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 2:30 usiku.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo aliyejitambulisha kwa jina mola la Massawe, aliliambia MTANZANIA Jumapili kuwa vijana hao walikuwa kundi kubwa kati ya 15 na 16.
Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Juma Makang’a, alithibitisha kutokea tukio hilo.
Alisema majira ya saa 2:30 usiku vijana wapatao sita wakiwa na pikipiki mbili, walivamia eneo hilo na kuanza kupiga milio ya pikipiki (bust) hali iliyozua taharuki miongoni mwa watu waliokuwa eneo hilo.
“Vijana wawili waliingia katika duka la Rosina Prosper, mfanyabiashara ya vyakula na kumpora simu.
“Baada ya hapo wakaingia kwenye duka la Rosemary, huyu ni mfanyabiashara ya M-Pesa, walimpora simu tatu, moja ni ya matumizi yake ya kawaida na mbili za kazi anayofanya, hizo ndiyo taarifa za awali nilizopata hakuna madhara ya kibinadamu.
“Uchunguzi unaendelea kufahamu kiasi gani cha fedha kilikuwa kwenye hizo simu na mali nyingine zilizoporwa,” alisema ACP Makang’a.