Janeth Mushi, Arusha
Watu watano wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, wameuawa katika majibizano na askari polisi mkoani Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Januari 30, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shanna, amesema majambazi hao waliuawa katika eneo la Mateves wakiwa njiani kuelekea Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara walikokuwa wakienda kufanya tukio la ujambazi.
“Majibizano ya risasi kati ya polisi na majambazi hao waliokuwa wakitumia usafiri wa pikipiki tatu, yalidumu kwa dakika 35 ambapo baada ya kuwaua katika eneo la tukio kulikutwa vitu mbalimbali ikiwamo bunduki aina ya Short Gun Pump Action iliyokuwa na namba 32265-02, Chinese pistol iliyofutwa namba za usajili, bastola moja bandia, risasi na simu tatu,” amesema Kamanda Shanna.
Amesema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa bunduki hiyo iliibiwa Januari 26 mwaka huu jijini Arusha, saa tisa usiku nyumbani kwa Jackson Msangi baada ya majambazi hao kuvunja nyumba yake iliyopo eneo la Burka ambapo pia waliiba simu ya mke wake Nikira Msangi na wote wawili walipoitwa wametambua mali zao ambazo ziliibwa siku waliyovamiwa.