AMON MTEGA Na LEORNAD MANG’OHA-RUVUMA
JESHI la Polisi limefanikiwa kuwauwa watu nane wanaodaiwa kuwa majambazi katika mikoa ya Dar es Salaam na Ruvuma.
Wakati Polisi Mkoa wa Ruvuma wakiwaua watu watano kwa kujibizana kwa risasi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imewauwa watatu akiwamo mwanamke ambaye naye anadaiwa kuwa jambazi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Songea, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Simon Maigwa, alisema jeshi hilo limefanikiwa kuwauwa watu watano huku wengine wakitoroka kwa kutumia pikipiki katika machimbo ya dhahabu ya Dapori yaliyopo katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji.
Kamanda Maigwa, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa moja usiku huko katika eneo la Momba Mtaa wa Lusaka wilayani Mbinga.
Alisema majibizano hayo ya risasi yalisababisha majambazi hayo matano kuuawa baada ya msamaria mwema kutoa taarifa polisi kuhusu uwepo wa majambazi hayo ambayo yalikuwa yanakwenda kufanya uhalifu katika eneo hilo la machimbo ya dhahabu.
POLISI DAR
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es salaam, limewaua watu tatatu akiwamo mwanamke mmoja kwa tuhuma za ujambazi na kufanikiwa kukamata bastola mbili aina ya Browning zilizofutwa namba na risasi tatu .
Akizungumza na waandishi wa habari jana Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema tukio hilo lilitokea Mei 25, mwaka huu maeneo ya Kigogo Fresh Mtaa wa Seremala jijini hapa.
Mambosasa alisema siku ya tukio jeshi hilo lilipata taarifa kutoka kwa msiri kuwa kuna kikundi cha majambazi wapatao watano wamepanga kuvamia nyumba ya Ally Dastan, mkazi wa Kigogo Fresh ambaye mke wake aitwaye Moshi Said (56) ni Mwenyekiti na ni mtunza hazina wa kikundi cha Umoja Group.
“Jeshi la polisi kupitia kikosi kazi maalumu cha kupambana na ujambazi kiliweka mtego katika nyumba ya Ally na ilipofika saa nane usiku majambazi hao wapatao watano walivamia nyumba hiyo na baada ya kugundua kuwa kuna mtego wa polisi walianza kurusha risasi na ndipo askari wakajibu mapigo na kufanikiwa kuwajerui majambazi watatu akiwemo mwanamke mmoja na majambazi wawili walikimbia.
“Majambazi hao walifariki dunia wakiwa njiani wakipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili,” alisema Mambosasa.
Katika hatua nyingine jeshi hilo limekusanya zaidi ya Sh bilioni 1.794 kutokana na tozo mbalimbali za makosa ya usalama barabarani kuanzia Mei Mosi, hadi 26 mwaka huu.