24.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 30, 2023

Contact us: [email protected]

Majaliwa’Maafisa madini ondoeni urasimu upatikanaji leseni kwa wachimbaji wadogo’

Na Clara Matimo, Mwanza

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka maafisa madini kuondoa urasimu wa upatikanaji wa leseni kwa wachimbaji wadogo wanapovumbua maeneo yenye madini.

Ametoa agizo hilo jijini hapa leo Mei 9, 2023 alipokuwa akifungua kongamano la madini pamoja na Mkutano mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania(FEMATA) lililoshirikisha wachimbaji wadogo wa madini na wadau wa madini.

Sehemu ya washiriki.

Ameeleza kwamba baadhi ya maafisa madini wamekuwa na tabia ya kuwadanganya na kuwanyang’anya maeneo wanayoyavumbua wananchi ama wachimbaji wadogo wa madini kwa kuwaambia kwamba maeneo hayo yamekwishakatiwa leseni miaka mingi.

“Mwananchi anapitapita huko anagundua kwamba eneo hili linapatikana madini anakuja kwa afisa madini anamwambia nataka kumiliki eneo hili anaambiwa lete coordinate anakabidhi anaambiwa njoo kesho.

“Akija kesho kwa kuwa afisa madini anakuwa analitaka na yeye eneo hilo kwa kuwa kaambiwa lina madini anacheza na computer anabadilisha anavyojua kisha anamwambia mwananchi huyo eneo hili liliishakatiwa leseni miaka mingi tena anataja kiongozi mkubwa kwamba ndiye anayelimiliki,” amesema na kuongeza:

“Afisa madini anamwambia mwananchi kwamba aaa eneo hili mbona linamilikiwa na Majaliwa miaka mingi, hali hii inasababisha wananchi wanabaki kuilalamikia serikali, wewe mtumishi wa madini usiwe mchawi wa kugombanisha wananchi na serikali yao,”ameagiza.

Awali akizungumza kwenye kongamano hilo, Rais wa FEMATA John Bina alitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo nchini kuwa ni pamoja na Tozo na ushuru kutoka mamlaka mbalimbali zikiwemo halmashauri, ruzuku, utafiti, vifaa duni vya kuchimbia, kutokuwa na elimu ya ufahamu wa sheria ya madini kanuni na taratibu za biashara ya madini na kutokuwa na taarifa sahihi za jemolojia.

“Ili tuweze kutatua changamoto ya utafiti tunaomba Stamico waongezewe nguvu ili waweze kuleta mitambo kwa ajili ya kufanyia tafiti ili tuchimbe kwa uhakika na kuaminika kwenye taasisi za fedha.

“Sisi wachimbaji wadogo hatukatai kulipa kodi tunalipa na tunahamasishana sana kulipa kodi serikalini kwa maendeleo ya nchi yetu lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu ushuru na tozo zimekuwa ni kero kubwa sana, tunalipa lakini serikali za mitaa zinatupa kodi ambazo ziko juu na zinatungwa bila kushirikisha wachimbaji, hii ni kero sana tunaomba wizara ya Tamisemi pamoja na Madiwani washirikiane ikiwezekana Wizara ya madini ibebe kodi zote tulipe huko iwe za NEMC, OSHA na TRA,”amesema Bina.

Akijibu changamoto hizo za FEMATA, Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Dk. Steven Kiruswa amesema: “Wizara inatambua changamoto za wachimbaji wadogo na imeendelea kubuni mbinu na mikakati mbalimbali ya kuzishughulikia ikiwemo kushirikiana na TAMISEMI kuona namna bora ya kila halmashauri kutengeneza sheria ndogo ambazo hazikinzani na sheria mama ya madini,” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima amesema kwa kutumia amani iliyopo mkoani humo, mkoa unaendelea na uwekezaji wa viwango mbalimbali katika sekta ya madini ili kuinua uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.

Nao baadhi ya wachimbaji madini akiwemo Jenipha Lulahobotse na Salum Sanga wameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwatatulia changamoto zinazowakabili na kubainisha kwamba hatua hiyo itavutia wawekezaji wa sekta ya madini kutoka nje ya nchi na kukuza uchumi wa taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,198FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles