27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa: Wanaochafua wenzao washughulikiwe

 BENJAMIN MASESE Na RAMADHAN HASSAN– MWANZA/DODOMA

WAKATI joto la Uchaguzi Mkuu likizidi kupanda kwa vyama vya wagombea mbalimbali wa vyama vya siasa wakiendelea kuchukua fomu za kuteuliwa kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ofisini za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Serikali imetoa onyo kwa wanasiasa wanaotumia majukwaa ya kisiasa kuchafua wenzao badala ya kunadi sera.

Kutokana na hali hiyo, vyombo vya ulinzi na usalama vimetakiwa kuwa macho wakati wote ikiwamo kuwakamata na kuwachukulia hatua wanasiasa watakaokwenda kinyume na agizo hilo.

Akitoa agizo hilo jana jijini Mwanza, Majaliwa, alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha vinawashughulikia ipasavyo wanasiasa na wagombea wa nafasi mbalimbali wanaopanda majukwaani na kuwashambulia wenzao, badala ya kunadi sera za vyama vyao na watakachokifanya iwapo wataaminiwa na wananchi kupitia sanduku la kura.

Akizungumza baada ya kukagua miradi minne ya ukarabati wa meli ya New Victoria, New Butiama, ujenzi Chelezo na meli mpya ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu, alisema lazima Tanzania iendelee kuwa nchi ya amani kwa mustakabali wa Watanzania wote ikiwamo kizazi cha sasa na vijavyo.

Alisema vyombo vya ulinzi na usalama vina jukumu la kuhakikisha amani inatawala kipindi chote cha kampeni hadi kutangazwa kwa mshindi wa nafasi ya urais, wabunge na madiwani.

Alisema yeyote atakayejaribu kuleta siasa za kuwagawa Watanzania na kuchafua wagombea wenzake anapaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Hii miradi yote minne imetekelezwa kwa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), haya yote yamefanyika kwa sababu ya uwepo wa amani, tuvishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi wanayofanya lakini mwaka huu kuna uchaguzi, sasa isitokee mtu anapanda jukwaani kushambulia mtu na kuleta siasa za kuwagawa Watanzania.

“Imani yangu vyombo vya ulinzi na usalama vitasimama kidete kuhakikisha nchi inakuwa salama, hatuhitaji siasa za kuchafuana majukwaani, hakuna muhimu wa kumtukana mwenzako tena kwa maneno yanayovunja sheria, kikubwa sema sera za chama chako na kitu gani cha kuwafanyia wananchi ili wakuamini na kukupa kura za kutosha.

“Bahati nzuri ilani ya CCM imetekelezeka na vitu vinaonekana kwa macho, sasa isitokee mtu anatoka huko kusikojulikana anapanda jukwaani na kuleta kashfa, kwa niaba ya Serikali naomba nisema wazi vyombo vya habari vimefanya kazi kubwa sana ya kuwaeleza wananchi kinachofanywa na Serikali, nimefika vijijini huko wananchi wanajua kila kitu na huwezi kuwadanganya.

“Serikali inatoa shukrani kwa waandishi wa habari, hakika wamebadilika na kuonyesha uzalendo kwa nchi yao na nasema hatutawaangusha kamwe, endeleeni kuwahabarisha wananchi ili imani waliyonayo kwa Rais Dk. John Magufuli iendelee kuongezeka kwa miaka mingine ijayo,” alisema Majaliwa

Aliwataka Watanzania kutokuwa na hofu ya aina yoyote, badala yake wawe watulivu na kuachana na vitisho vinavyotolewa na baadhi ya wanasiasa kwani Serikali imejipanga kuwahudumia wananchi kwa usawa ili kila mmoja aweze kupata maendeleo kupitia biashara zao.

Mbali ya siasa, aliwataka Watanzania ambao wamepata fursa ya kufanya kazi na wakorea wanaojenga meli ya MV Mwanza Hapa Kazi, kujiandaa kuwa mafundi wa baadaye baada ya wakandarasi hao kuondoka.

DODOMA

Baada ya kutoka jijini Mwanza, Kassim Majaliwa, alitua jijini Dodoma na kutoa wiki moja Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kuhakikisha anafuatilia madai ya wanafunzi wa vyuo vikuu yakutopewa vitambulisho vya bima ya afya, licha ya kulipia gharama za bima hiyo.

Majaliwa alietoa maagizo hayo jana jijini hapa,wakati akifungua mkutano mkuu wa kwanza wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO).

Alisema lengo ni kuhakikisha suala hilo linapatiwa ufumbuzi kwa haraka kwa wanafunzi hao.

Kuhusu changamoto ya kupanda kiholela kwa bei ya nyumba ambazo hupanga wanafunzi wanaoishi hosteli amemuagiza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Malazi,William Lukuvi kulifuatilia suala hilo kwakutembelea katika maeneo wanayoishi wanafunzi na atalitolea ufafanuzi 

Alisema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya vijana wasomi kujiajiri kwa kufungua fursa mbalimbali za uwekezaji nchini ili kuondokana na tatizo la ajira.

Aliwataka wanafunzi kujitokeza kwa wingi wakati wa kampeni kuwasikiliza wagombea wa vyama mbalimbali vya siasa sera zao na baadaye kuzipima kama zinawafaa ndipo wafanye maamuzi wakati wa uchaguzi utakapofika.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo,Peter Niboye aliupongeza utendaji kazi uongozi wa Serikali.

Alisema changamoto zinazowakabili nipamoja na suala la kukosa vitambulisho vya bima ya afya na kupanda kwa bei za nyumba kwa wanafunzi wanaoishi.

Sambamba na hilo Jumuiya hiyo kuelekea uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu wametoa msimamo wao kuungana na Rais John Magufuli kuhakikisha anashinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu.

WAGOMBEA WALIOCHUKUA FOMU

Jumamosi mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, alikuwa mgombea wa 10 kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kugombea urais wa Tanzania.

Kabla ya Lissu kuchukua fomu hizo kwenye ofisi za NEC jijini Dodoma, alitanguliwa na mgombea wa Chama cha Demokrasia Makini, Cecilia Mmanga ambaye alifika ofisi za NEC na bajaji, huku akisema ametumia usafiri huo kuonyesha chama chao kitajali watu wa hali ya chini.

Baada ya Lissu kuchukua fomu, Chadema walisema wataanza kuchutafuta wadhamini mjijini Dodoma, huku Demokrasia Makini wakisema wataanzia Mkoa wa Kilimanjaro.

Fursa hiyo ya kutafuta wadhamini ni uwanja mwingine wa wanasiasa hao kuuza sera zao kabla ya kipenga rasmi cha kampeni kupulizwa na NEC. 

 LISU

Lissu alifika NEC saa 5 asubuhi, akiwa na msafara wa magari zaidi ya 50 akiwa ameongozana na mgombea mwenza Sulum Mwalimu Juma na baadhi ya viongozi wa juu wa Chadema wakiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika.

Wakati Lissu akiingia e ofisi hizo kuchukua fomu, wafuasi wa Chadema waliokuwa katika magari zaidi ya 50 wakibaki nje.

Lissu ambaye alikuwa akilindwa na walinzi ambao walivalia suti nyeusi huku yeye akishuka katika gari aina ya Benz.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles