Majaliwa: Wanafunzi wote waanze masomo pamoja

0
1028

MWANDISHI WETU-RUANGWA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema miradi yote ya ujenzi wa miundombinu ya shule ikamilike mapema na kama kuna watendaji walioko likizo warudi kwani Serikali inataka wanafunzi wote waanze masomo pamoja.

Hayo aliyasea jana wakati alipofanya ziara kukagua ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Ruangwa, ambapo alisisitiza ukamilishwaji wa miradi hiyo ili wananchi waanze kuitumia.

Waziri Mkuu alisema agizo alilolitoa kwa wakuu wa mikoa Desemba 29, 2019 kuhusu usimamizi wa miundimbinu ya shule ikiwamo ujenzi wa madarasa liko palepale kwa sababu Serikali haitaki kuona wanafunzi wakipishana katika kuanza masomo.

Miradi ambayo Waziri Mkuu ameitembelea ni ujenzi wa Shule ya Msingi Ng’au ambayo ipo katika hatua za mwisho kukamilika, ujenzi wa Chuo cha Veta, Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa na Shule ya Sekondari Lucas Maria.

Waziri Mkuu alisema Serikali inatoa fedha kugharamia miradi ya maendeleo, hivyo ni lazima viongozi katika maeneo husika wahakikishe wanashirikiana kusimamia utekelezaji wake.

“Wanafunzi wanatakiwa kuanza masomo mwanzoni mwa mwezi Januari, 2020, hivyo ni lazima usimamizi ukaongezwa katika baadhi ya maeneo ambayo miundombinu yake bado haijakamilika ili kuwahi masomo,” alisema.

Akiwa katika Shule ya Sekondari Lucas Maria, Waziri Mkuu amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Andrea Chezue ahakikishe mafundi wanafanya kazi usiku na mchana.

“Shule zinakaribia kufunguliwa na baadhi ya majengo kama bwalo, maabara, nyumba za walimu hayajakamilika mafundi hawapo eneo la ujenzi na Serikali imetoa fedha. Nataka kazi hii ikamilike mapema kwani hakuna sababu,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here