28.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa: Wanafunzi China wanaendelea na masomo

Mwandishi Wetu – Lindi

WAZIRI Mkuu Kassim Mjaliwa amesema wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikuu mbalimbali nchini China waliozuiwa kutokana na mlipuko wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona wanaendelea na masomo yao kwa njia ya mtandao.

Aliyasema hayo jana katika mahafali ya 38 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT), Uwanja wa Ilulu mjini Lindi.

Alisema baada ya virusi vya corona kuikumba China, vyuo vilifungwa na sasa vimefunguliwa na wanafunzi wanasoma kwa njia ya mtandao.

“Tehama sasa imefikia katika hatua nzuri kwa sababu mhadhiri mmoja anaweza kuwafundisha wanafunzi wake wote popote walipo kwa njia ya mtandao. Tehama imewezesha wanafunzi waliozuiwa kurudi nchini China kuendelea na masomo wakiwa nyumbani kwao,” alisema Majaliwa.

Aliwataka wahitimu wa CKHT kutambua kwamba vyeti walivyotunukiwa ni tuzo halali kwa juhudi na jitihada walizoonyesha katika masomo yao, hivyo wanaporejea kwenye jamii wahakikishe wanaipatia tuzo ya utendaji bora na ufanisi itakayoakisi viwango vilivyoainishwa kwenye vyeti vyao.

“Nendeni mkaidhihirishe tuzo hii ya pili katika utendaji wenu na maisha yenu ya kila siku, iwe ni katika sekta rasmi au sekta isiyokuwa rasmi.

“Hakikisheni mnaonyesha tofauti katika kutafuta majibu ya maswali mbalimbali yanayowakabili Watanzania kuhusu mustakabali mzima wa kujiletea maendeleo,” alisema Majaliwa.

Alisema amefuatilia kwa karibu maelezo ya viongozi waliotangulia kuhusu umuhimu na hata mafanikio ya chuo hicho ambapo amewataka watambue kwamba Serikali inakiangalia kwa jicho la karibu sana kwa kuwa kimekaa kimkakati zaidi kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa.

Majaliwa alisema licha ya changamoto mbalimbali zilizopo, Serikali imeweza kuanzisha chuo hicho na kukiona kikiendelea kutanuka hadi nje ya mipaka ya nchi. 

“Haya ni mafanikio makubwa na ya kujivunia. Tunawashukuru waasisi wa taifa letu kwa maono haya makubwa kuhusu Tanzania,” alisema Majaliwa.   

Alisema mwasisi wa taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere aliona mbali wakati akianzisha mchakato wa kuanzisha chuo hicho kwa kusema angependa kuona taasisi inawawezesha watu wazima wengi waweze kuendelea na elimu ya juu pasipo kuacha kazi zao.

 “Kwa nchi masikini kama Tanzania, hakuna taasisi nyingine ya elimu ya juu inayoweza kuwa ya msaada zaidi kwa watu wetu,” alisema Majaliwa.

Alisema kuwa ukweli wa kauli hiyo unaendelea kudhihirishwa siku hadi siku kupitia mafanikio ya chuo hicho.

“Tutake tusitake, elimu ya juu inayoweza kusaidia Watanzania wengi zaidi ni hii ya kupitia mfumo wa elimu masafa na huria.

 “Kwa miaka nenda rudi, chuo kimehitimisha wataalamu lukuki, ambao wengi wameingia kwenye sekta mbalimbali za utumishi na uzalishaji na kutoa mchango muhimu sana kwenye maendeleo ya nchi yetu,” alisema Majaliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles