25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

Majaliwa: Wafanyabishara changamkieni fursa usambazaji chakula

Anna Potinus

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wafanyabiashara nchini kuchangamkia fursa ya kusambaza vyakula kwenye maeneo ambayo hayana chakula ili kujikwamua kiuchumi.

Ametoa wito huo bungeni leo Alhamisi Novemba 14, katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia aliyetaka kujua mkakati wa serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata chakula kwenye maeneo yenye uhaba.

“Baadhi ya mikoa ikiwemo Dodoma na Wilaya zake zote, Manyara, Singida na baadhi ya mikoa mingine hapa nchini inakabiliwa na tatizo kubwa la chakula, baadhi ya wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama kwenye Wilaya na mikoa inawezekana hawatoi taarifa sahihi kwa uoga kutokana na pengine kutoelewa vizuri kauli ya rais, je serikali iko tayari sasa kuunda tume au kamati maalum ifanye utafiti na kuja na data zinazoonesha upungufu gani wa chakula katika maeneo hayo ili wananchi wapelekewe chakula tena cha bei nafuu kwasababu hali sio shwari,” amehoji.

Akijibu swali hilo Majaliwa amekiri kuwepo kwa uhaba wa chakula katika baadhi ya maeneo akisema inatokana na tatizo la hali ya hewa ambapo baadhi ya maeneo hukosa chakula kutokana na kutokuwa na mvua za kutosha.

“Upungufu wa chakula upo kwa baadhi ya Wilaya na maeneo kadhaa na hii inatokana na tatizo la hali ya hewa kwasababu yapo maeneo msimu uliopita hatukupata mvua za kutosha jambo hili linapotokea kule kwenye ngazi hiyo wapo viongozi na tumeweka utaratibu wa viongozi hao kuratibu shughuli zote, tunacho chombo kinachonunua vyakula na kinahifadhiwa kwaajili ya maeneo ambayo hayana chakula na kurudisha zile fedha ili ziendelee kununua vyakula ili benki iweze kuendelea kuwepo, tunachosubiri sasa ni viongozi wa maeneo hayo kuandika kuonesha kuwa wana upungufu wa chakula ili Wizara ya Kilimo iratibu utaratibu wa kuwafikishia chakula.

“Nitoe wito kwa wafanyabiashara wetu nchini, Tanzania maeneo yote haya yana hali ya hewa tofauti yako ambayo yalipata mvua nyingi na walizalisha chakula cha kutosha na yapo ambayo hayakuwa na mvua za kutosha na hakuna chakula cha kutosha hivyo ni jukumu la wafanyabishara wetu kutumia fursa hiyo kwa kuhamisha chakula kutoka maeneo yenye chakula cha kutosha na kupeleka kwenye maeneo ambayo hakuna ili waweze kujipatia uchumi,” amesema Majaliwa.

Aidha amesema kuwa bado kuna umuhimu wa mkuu wa wilaya kuiandikia wizara ya kilimo kueleza mazingira hayo na kwa utaratibu wa wizara ya kilimo wanaweza kwenda kwenye maeneo hayo kujionea na kujiridhisha takwimu iliyotolewa halafu waruhusu chombo chao kupeleka mahindi kwa kuuza ili wananchi wapate fursa ya kununua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,695FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles